Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Na Mwandishi
Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kinadaiwa kuwa na
mpango wa kumsimamisha Dk. Ali Mohammed Shein kuwania urais wa Muungano katika
uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Hatua hiyo itatibua ndoto za urais za Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, pamoja na Waziri
Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ambao kambi zao zinatajwa kuwa na nguvu ndani ya
chama hicho.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya chama hicho
vimeeleza kwamba, hatua ya kutaka kumsimamisha Dk. Shein inatokana na Rais huyo
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutokuwa na makundi kwenye chama, hivyo
kumaliza ‘mnyukano’ unaoendelea wa makada wa chama hicho ambao wanaendelea
kumwaga fedha katika mitandao na kambi mbalimbali.
Sababu nyingine ni ile ya CCM kutafuta namna
ya kuulinda Muungano, ikiamini kwamba inaweza kupunguza munkari wa Wazanzibari
wanaoupinga Muungano huo, hivyo kujihakikishia kura za visiwa vya Unguja na
Pemba.
Taarifa hizo zimekuja wakati Kamati Kuu ya
CCM ikitarajiwa kuketi kesho Jumanne katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini
Unguja kujadili na kutathmini hali ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Ikiwa uamuzi huo utafikiwa katika vikao rasmi
vya chama, utahitimisha safari ya kwenda Ikulu ya vigogo kadhaa wa chama hicho,
akiwemo Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, ambaye licha ya yeye kutotangaza
rasmi, lakini ametajwa kwamba amejipanga vilivyo kuhakikisha anaomba kuteuliwa
kuwania nafasi hiyo adhimu.
“CCM ina wakati mgumu katika kutafuta mrithi
wa Rais Jakaya Kikwete, vigogo wengi wanatajwa na wengine wametangaza nia,
lakini suala la Muungano nalo limeleta mtikisiko mkubwa na wanatafuta namna ya
kukabiliana na mtikisiko huo.
“Wazanzibari wamekuwa wakilalamika kwamba
Muungano hauwasaidii, ndiyo maana kwenye maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, walisema wanataka Muungano wa Mkataba, ambao kimsingi hautakuwa na
nguvu, hivyo endapo Dk. Shein atateuliwa anaweza kurejesha matumaini,” kimesema
chanzo chetu kutoka ndani ya CCM.
Chanzo kingine kimesema, endapo Dk. Shein –
rais wa kwanza wa SMZ kutoka Kisiwa cha Pemba – atateuliwa, CCM ina uhakika wa
kupata kura za Unguja na Pemba.
Ingawa suala hilo halijawa wazi, lakini kitendo cha vigogo wa CCM
wanaotajwa kuwania urais kujikita Zanzibar wakati huu wa vikao vya Kamati Kuu
kinaashiria kwamba kuna hofu kubwa ya karata kugeuka wakati wowote ikiwa
hawatafanya jitihada za ziada.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, ilielezwa kwamba baadhi ya wagombea wa
nafasi hiyo wamekuwa wakipishana kwa usafiri wa ndege na boti kwenda Zanzibar
kutafuta kuungwa mkono na wajumbe wa NEC na waliopo visiwani humo.
Gazeti moja la kila siku liliripoti mwishoni mwa wiki kwamba, vigogo wa
urais waliofanya ziara kwa nyakati tofauti hivi karibuni visiwani Zanzibar ni pamoja
na Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano)
Stephen Wasira, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda ambaye alialikwa kuhudhuria Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW)
Jumamosi yaliyoandaliwa na Mbunge wa Mpendae na Mafanyabiasha mashuhuri, Salum
Turky.
Kadhalika Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ambaye wakati wa Sikukuu ya
Krismasi ya mwaka 2014 alikuwa Zanzibar.
Inaelezwa kwamba suala kubwa ambalo Kamati Kuu italijadili ni kuangalia
mwenendo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015 tangu
kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, lakini pia suala la akaunti ya Tegeta
Escrow.
Makada wa chama hicho wanaowania urais mbali ya Lowassa na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, ni Bernard Membe – Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa – ambaye yaonekana bado anasubiri kuoteshwa ili atangaze rasmi ingawa
taarifa zinasema wafuasi wake wamekuwa wakiendelea na kampeni hadi mitandaoni.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi, Teknolojia January
Makamba, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
No comments:
Post a Comment