Na Mwandishi Wetu
KASHFA ya kuuzwa kwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa bei ya
kutupwa inayotarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa 18 wa Bunge unaoanza kesho Mjini Dodoma, inatajwa kuwa moja ya ajenda ambazo zitatawala mwenendo wa
mjadala wa vikao vya Bunge.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Bunge waliokuwa wakihudhuria
vikao vya kamati hizo jijini Dar es Salaam, vilivyoketi kwa muda wa wiki mbili
wamesikika wakieleza kuwa wamejipanga kwenda kuibana serikali ili itoe maelezo
ya kina ya jinsi NBC ilivyobinafsishwa kwa bei ya chee na pia iwataje maofisa
wa serikali waliohusika na ubinafsishaji huo.
NBC iliuzwa kwa Shs. 15 bilioni, fedha ambazo ni ndogo kuliko
thamani halisi, kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya fedha.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, zimeeleza kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati
hiyo hawajaridhishwa na maelezo ya serikali iliyoyatoa kuhusu ubinafsishaji wa
NBC, jambo ambalo limeibua hali ya mashaka kuwa huenda wapo viongozi wa
serikali waliohusika na sakata hilo ambao wameamua kuficha ukweli.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyezungumza na gazeti hili kwa
sharti la jina lake kutotajwa gazetini kwa sababu yeye siyo msemaji, alidokeza
kuwa kuna hali ya sintofahamu kuhusu chanzo cha kufisilika kwa NBC kabla ya
kubinafsishwa kwa bei ya kutupwa kwa Benki ya ABSA ya Afrika Kusini.
Alisema, wabunge wamehoji na kuomba maelezo ya kina kutoka
serikalini kwa muda mrefu pasipo mafanikio huku kwa upande mwingine hali ya
uchumi wa taifa ikizidi kuwa mbaya.
“Suala la kuuzwa NBC kwa bei ya kutupwa bado halijafa, serikali
imeshindwa kutupa maelezo ya kina ingawa tumekuwa tukiyaomba kwa muda mrefu,
sasa tumeamua kwenda na ajenda hii kwenye Mkutano wa 18 wa Bunge kwa sababu
mjadala wake haustahili kufa mpaka ukweli halisi ufahamike kwa umma,” alisema
Mbunge huyo.
Taarifa nyingine kutoka ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) zimeeleza kuwa wajumbe wa kamati hiyo wameshtushwa na
habari walizozipata serikalini zinazoonyesha kuwepo kwa uwezekano wa serikali
kupoteza asilimia 30 ya hisa zake inazozimiliki kwenye NBC.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa
agizo la kuongezwa kwa mtaji wa NBC ili kufidia hasara iliyoipata na hivyo
kuchota akiba yake.
Zilieleza kuwa wakati NBC ikibinafsishwa baada wafanyabiashara
wa ndani kuchota mabilioni ya fedha ambayo hawakulipa baada ya kutumia njia za
udanganyifu, serikali haikuwa na fedha na ikailazimu kukopa kwa mbia mwenzake
ambaye ni Benki ya ABSA ya Afrika Kusini, Shs. 22.5 bilioni kwa riba ya
asilimia 8 kwa mwaka ili kuchangia mtaji wake ndani ya benki hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa serikali ilishindwa kulipa deni
hilo na ilipewa muda unaoishia mwezi Machi 2015 kuwa imekwishalipa deni lake,
vinginevyo itapokwa hisa hizo na hivyo kuifanya NBC kumilikiwa na wageni kwa
asilimia 100.
Kabla ya kuibuka kwa taarifa hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali, (PAC) Zitto Kabwe alitoa taarifa katika mitandao ya
kijamii akieleza kuwa kashfa ya uuzwaji NBC kwa bei ya kutupwa haitaachwa bila
kuchunguzwa na ukweli wake kuwekwa wazi.
Akiandika katika mitandao hiyo, Zitto alisema wakati akiwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye uchunguzi maalumu kuhusu benki hiyo
jambo ambalo halikuchukuliwa kwa uzito.
Katika andishi lake hilo, Zitto alieleza kuwa mwishoni mwa mwaka
jana, Kamati ya PAC anayoiongza ilikutana na watendaji wa Ofisi ya Msajili wa
Hazina ambaye ndiye mmiliki wa mali zote za Serikali kwenye Mashirika ya Umma
na kampuni binafsi ambazo Serikali ina hisa na kujadili uwezekano wa
Serikali kupoteza hisa zake katika NBC lakini ufumbuzi wa uhakika
haukupatikana.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa wabunge, bado haijafahamika iwapo
mjadala kuhusu kashfa ya ubinafsishaji NBC utakuwa katika ratiba ya shughuli za
mkutano wa 18 wa Bunge.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamati ya Uongozi ya Bunge chini ya
Spika wa Bunge, Anne Makinda, ilikutana Ofisi Ndogo ya Bunge jijini Dar es
Salaam kupanga ratiba ya mkutano wa 18 wa Bunge ambayo inatarajiwa kufahamika
kesho.
CREDIT: DIRA YA MTANZANIA
No comments:
Post a Comment