Profesa Sospeter Muhongo akitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri wa Nishati na Madini Jumamosi, Januari 24, 2015
Na Sophia Yamola
KAZI imekwisha. Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter
Muhongo amejiuzulu, Baraza la Mawaziri nalo limebadilishwa.
Haya yote yanadhihirisha kukamilika kwa kazi ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotoa mapendekezo na Bunge kutoa
maazimio ya kumtaka Rais Jakaya Kikwete amfukuze kazi waziri huyo, kutokana na
kutajwa kwenye kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow.
Lakini Profesa Muhongo naye amesema amemaliza kazi katika
wizara hiyo aliyoiongoza kwa kipindi cha miaka miwili na nusu baada ya
‘kutimuliwa’ kwa William Ngeleja.
Kujiuzulu kwa Prof. Muhongo kunaonekana kuhitimisha kilio
cha wananchi na watunga sera waliotaka waziri huyo kuwajibishwa, japo kwa muda
mrefu hakuwa tayari.
Akizungumzia kujiuzulu kwake, Prof. Muhongo alisema ameamua
kuchukua uamuzi huo ili mambo mengine ya kitaifa yasonge.
“Mambo mengi yanaonekana kusimama kwa sababu mijadala mingi
ndani ya serikali ni Escrow, ndani ya chama (CCM) ni Escrow, hata Bungeni
mjadala ni huo huo tu.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki
iliyopita, kabla hajachukua uamuzi huo alisema inatakiwa ifike mwisho juu ya
sakata la Escrow kwani wananchi wanahitaji kufanya shughuli za maendeleo kuliko
kuendeleza malumbano ambayo hayana faida.
“Inatakiwa tufike mwisho kuhusu sakata la Escrow,
inawezekana mimi ndio tatizo juu ya mambo yote haya. Yapo mambo mengi ya msingi
ambayo yanahitaji kusonga mbele, sasa nimeona bora nipishe,” alisema.
Hata hivyo, alionya kwamba Watanzania wanapaswa wajue
kwamba kwenye sakata hilo kuna mvutano wa kisiasa, ubinafsi, wivu, chuki, fitna
za kisiasa, biashara na mvutano wa mambo ya kisiasa.
Alisema baada ya kutafakari kwa kina ameamua kwamba maslahi
ya Taifa yawe muhimu kuliko cheo cha mtu mmoja.
Alisema yote hayo yamemkuta kwa sababu haingiliki kwa
rushwa, hajawahi kupewa rushwa wala sio rahisi na haiwezekani.
Akizungumzia kuhusu wafadhili kusitisha misaada ya fedha,
Prof. Muhongo alisema lazima ifike mahali nchi iache kuwa tegemezi kwa
wafadhili na badala yake isimame yenyewe.
“Ukitaka utu wako utambuliwe ni lazima ujitegemee, Mwalimu
Julius Nyerere (Rais wa kwanza wa Tanzania) aliwahi kusema lazima kama Taifa
lijitegemee, hawa wafadhili kila mwaka huwa hawakosi sababu, mwaka juzi bei ya
umeme ilipopanda walitishia kusitisha misaada, mwaka jana sakata hili la Escrow
na mwaka huu wataibuka na kitu kingine,” alisema.
Alisema hata hizo fedha ambazo wahisani wanaahidi kuzitoa
kwa miaka 10 mfululizo, hakuna hata mwaka mmoja walishatoa kwa asilimia 100,
badala yake huishia asilimia 60.
Kabla hajatangaza uamuzi wake huo wa kuachia ngazi, Prof.
Muhongo alielezea mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka miwili na nusu
aliyokaa wizarani hapo toka ateuliwe kushika wadhifa huo.
Alisema aliongoza jahazi kwa kupeleka umeme vijijini kwa
gharama za kuunganisha za Shs. 27,000 ambapo matarajio ni kwamba, hadi kufika
Juni mwaka huu vijiji 500 vitakuwa vimepata umeme huku akiamini siku za usoni
matatizo ya umeme hayatakuwepo.
Akizungumzia mafanikio mengine yaliyopatikana akiwa
wizarani hapo ni kubadili Shirika la Umeme (Tanesco), kuanza kujiendsha
kibiashara tofauti na ilivyokuwa awali, mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam kukamilika kwa asilimia 99 na tayari wameshaanza majaribio
ya awali.
Mafanikio mengine ni kusuka upya Shirika la Madini (Stamico),
ambapo hivi sasa mgodi wowote unapoanzishwa serikali inakuwa na hisa, huku
kampuni kubwa zikitakiwa kulipa kodi asilimia 30 na malipo kwa Halimashauri
(service levy) Dola za Kimarekani 200,000.
Alisema, Stamico kwa sasa ndio mlezi wa wachimbaji wadogo,
lakini kazi kubwa aliyoifanya ni kuwanyang’anya wawekezaji ambao walikuwa
hawaendelezi maeneo yao ya uchimbaji wa madini kwa miaka 15 hadi 20.
Sakata
la uchotwaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kiasi cha Shs. 306 bilioni liliibuliwa
Bungeni mwaka jana na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR), David Kafulila, ambapo
mara baada ya majadiliano makali Bunge liliazimia kuwajibishwa kwa mawaziri
Prof. Muhongo, Prof. Anna Tibaijuka, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji
Frederick Werema, kutokana na sakata la uchotaji wa fedha katika akaunti ya
Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT) kwa kutaka mamlaka ya uteuzi kutengua
uteuzi wao.
Mbali
na hao alikuwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na
Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco.
Hata
hivyo mwanasheria Mkuu alitangaza kujiuzulu, Prof. Tibaijuka alifutwa kazi, Katibu
Mkuu Nishati na Madini uchunguzi unaendelea, Bodi ya Wakurugenzi imeundwa upya,
huku wengine wakifikishwa mahakamani.
Pamoja
na kuwa mmoja kati ya watu walioshiriki kuandaa mapendekezo ya Bunge ya kumtaka
waziri Muhongo aondoke, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alimsifu
kiongozi huyo na kusema kuwa amewajibika kwa kuwa makosa yamefanyika chini
yake.
Zitto
ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), amemsifu
Muhongo kuwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kipekee ambaye amefanya mambo makubwa
yatakayomfanya akumbukwe.
Baraza la Mawaziri
Rais
Kikwete alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri saa chache baada ya kujiuzulu
kwa Muhongo, ambapo George Simbachawene ndiye aliyemrithi waziri huyo katika
Wizara ya Nishati na Madini.
Mawaziri
wengine ni Mary Nagu (Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu); Christopher Chiza
(Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Uwezeshaji); Dk. Harrison Mwakyembe (Ushirikiano
wa Afrika Mashariki); William Lukuvi (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi);
Steven Wasira (Kilimo, Chakula na Ushirika); Samuel Sitta (Uchukuzi); na
Jenista Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge).
CREDIT: DIRA YA MTANZANIA
No comments:
Post a Comment