Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 13 January 2015

UKOSEFU WA KAZI KWA VIJANA NI JANGA LA DUNIA

DSC_0499
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan akionyesha gazeti la "Tuwasiliane" linalochapishwa na UTPC na kusambazwa kwa wadau na maeneo mbalimbali ya jijini Mwanza kwa Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez aliyetembelea makao ya ofisi hizo kwa ajili ya mazungumzo na kuboresha ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa Umoja huo wa vilabu vya waandishi wa habari nchini.


Na Mwandishi Wetu
WIMBI kubwa la kuwa na vijana wasiokuwa na kazi limeelezwa kuwa tatizo duniani kote na serikali mbalimbali zinatakiwa kuliangalia hilo kwa undani na kulitatua.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez.
Mratibu huyo alisema hayo katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC) Abubakar Karsan.
Alisema ukosefu wa kazi kwa sasa ni tatizo la kijamii na kwamba, shauri hilo lisipoangaliwa kwa makini linaweza kuwa chanzo cha matatizo makubwa ya usalama na amani katika taifa.
Alvaro Rodriguez ambaye alifika katika ofisi za UTPC kuangalia mambo yanayofanyika katika ofisi hiyo wakati akiwa ziarani Mwanza wiki iliyopita, alisema kama tatizo la ajira litaendelea kuwapo, vijana wanaoathirika wanaweza kufikiria njia nyingine isiyo ya kistaarabu kufanikisha mambo yao.
DSC_0440
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan akizungumza na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto) aliyeambatana na Mshauri wa masuala ya haki za binadamu kutoka ofisi ya mratibu mkazi wa UN Tanzania, Bi. Chitra Massey (kulia) alipotembelea makao makuu ya ofisi hizo jijini Mwanza.

Alisema Umoja wa Mataifa unaendelea kushirikiana na serikali mbalimbali kuhakikisha kwamba tatizo la ajira kwa vijana linamalizwa ili jamii isiingie katika mtafaruku utakaokosesha amani na usalama na hivyo kusimamisha maendeleo yaliyofikiwa katika jamii.
Bila kutaja makundi ya kigaidi yanayotikisa dunia kwa sasa kama Al - Qaeda na washirika wake Boko Haram, Al - Shabab, Islamic State of Iraq na Levant (ISIL) alisema makundi mengi ya kigaidi duniani yanatokana na vijana kutojua wafanye nini na mazingira waliyonayo na hivyo kuwa rahisi kushawishika.
Alisema makundi ya hatari mara nyingi ni ya vijana ambao wanashindwa kupata riziki au hawajui wafanye nini kupata riziki na serikali zimewaacha bila kuwaangalia.
Aidha alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia kuhakikisha kwamba masuala muhimu yanayowezesha maendeleo kama demokrasia yanazingatiwa ili kuiwezesha jamii kufanya maamuzi sahihi ya vile wanavyotaka kupanga maendeleo yao.
DSC_0487
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu (kulia) akichangia jambo wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC) Abubakar Karsan makao makuu ya ofisi za umoja huo jijini Mwanza.

Alisema Demokrasia huwezesha wananchi kujua namna wanavyoweza kutengeneza mustakabali wao katika masuala ya ustawi wa jamii na maendeleo huku haki zao za msingi zikilindwa.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Bw. Karsan alimwambia mratibu huyo mambo ambayo yamefanywa na umoja huo na changamoto walizokumbana nazo kwa kuzingatia mpango mkakati wake wa mwaka 2011-2013.
Umoja huo ambao ulianzishwa mwaka 1996 na kusajili na wizara ya mambo ya ndani kama taasisi isiyokuwa ya kiserikali (NGO) mwaka uliofuata, umefanikiwa kuanzisha mfuko wa kusaidia vyombo vya habari kwa jina la Daudi Mwangosi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari wa Iringa (IPC).
DSC_0481
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan wakati wa mazungumzo ya kuboresha mahusiano baina ya mashirika ya umoja wa mataifa na umoja wa vilabu vya waandishi wa habari nchini Tanzania.

Aidha alimwambia kwamba wamefanikisha mafunzo ya kuongeza umahiri wa uandishi wa habari na pia kuwaelezea umma juu ya uhuru wa vyombo vya habari.
Pia alielezea mafanikio yaliyopatikana katika kampeni za kuelimisha umma na kuelewana miongoni mwa wadau mbalimbali wa sekta ya habari.
Alisema hata hivyo bado wanaendelea na kampeni yao kutaka mabadiliko ya malipo kwa waandishi wa habari wanaojitegemea ambao ndio wanatoa mchango wa asilimia 75 hadi 80 za habari zinazotangazwa au kuchapishwa.
Aidha wanaendelea kutoa mafunzo ya kanuni na maadili kwa waandishi wa habari na kuendelea kukabiliana na tatizo la usalama katika mpango mkakati wa mwaka 2015 – 2019.
Katika ziara hiyo ya kanda ya Ziwa, mratibu huyo aliambatana na mshauri mwandamizi wa masuala ya haki za binadamu Dk Chitralekha Massey na Mtaalamu wa mawasiliano wa umoja huo hapa nchini HoyceTemu.

No comments:

Post a Comment