Na
Mwandishi Wetu
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) inadaiwa kuwa
unakusudia kumsimamisha Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba kuwania urais mwaka
huu dhidi ya wagombea wa vyama vingine, kikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM).
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Ukawa vimeeleza kwamba,
uamuzi wa kumsimamisha Jaji Warioba unazingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo
kuepuka mvutano baina ya vyama hivyo vinne vinavyounda umoja huo.
Hata hivyo, pendekezo hilo linaweza kugonga mwamba kwani
Jaji Warioba amesema amemaliza kazi aliyotumwa ya kusimamia ukusanyaji wa maoni
ya wananchi kuhusu Katiba Mpya ambayo aliifanya kwa uadilifu mkubwa.
Akizungumza na Gazeti hili kwa njia ya simu akiwa nje ya
nchi, Jaji Warioba aliomba kutohusishwa na masuala ya siasa kwa sasa, kwani
anahitaji kupumzika baada ya kumaliza wajibu wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Warioba ambaye mwaka 1995 aliwahi kuwania urais kabla ya
kushindwa katika kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi, alisema kama
angekuwa na haja hiyo, basi angegombea kupitia CCM na si vinginevyo.
“Nahitaji kupumzika sasa, nimemaliza kazi jamani. Kama
ningeutaka urais, basi ningegombea kupitia chama changu cha CCM,” alisema.
Ukawa wanatarajiwa kukutana Jumanne hii kujadili mambo
mbalimbali, ukiwemo mchakato wa kuwapata wagombea wake wa urais, ubunge na
udiwani, ingawa haijajulikana kama ajenda ya pendekezo la kumsimamisha Jaji
Warioba itakuwa mojawapo.
“Wanataka kuepuka mvutano wa nani miongoni mwao atakayegombea,
kwani imebainika huko nyuma umoja kama huo, ambao haukuwa rasmi, uliwahi
kuvunjika kutokana na kila kiongozi wa chama kutaka agombee urais,” kilisema
chanzo hicho.
Kikaongeza: “Warioba kwa sasa ni mtu huru, bado yuko CCM,
lakini anaweza kuombwa aje huku kwani pande zote zinamkubali na anaweza kuwa
chaguo sahihi kuliko viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa kwa sasa.”
Chanzo kingine kimeeleza kwamba, sababu nyingine inayowapa
nguvu Ukawa kumsimamisha Warioba ni kutokana na mchango wake mkubwa alipoiongoza
Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuandaa rasimu inayotajwa kwamba ingeweza
kuondoa kero nyingi kama siyo kudaiwa kuchakachuliwa wa wabunge wa CCM katika
Bunge Maalum la Katiba mwaka jana.
Inaelezwa kwamba, akiwa Mwenyekiti wa Tume hiyo pamoja na
wajumbe wake, Jaji Warioba alifanya kazi nzuri, lakini CCM wakampuuza,
kumtukana na hata kunusurika kupigwa na kundi la wanachama, achilia mbali
kuichakachua rasimu hiyo na kupinga muundo wa Muungano wa Serikali Tatu
uliopendekezwa.
“Uchakachuaji wa rasimu hiyo ndio uliozaa Ukawa, kwa hiyo
Jaji Warioba anakubalika kwa asilimia zote na ikiwa uamuzi huo utafikiwa na
yeye akakubali, basi ataeleta ushindani wa kutosha dhidi ya mgombea wa CCM.
“Jaji anakubalika hata na wananchi wengi ambao wanaamini
Tume yake ilikuwa inawaletea tiba ya changamoto zao za miaka mingi, hata
wanaCCM wanamkubali,” kiliongeza chanzo hicho.
Oktoba 26, 2014, vyama vinne; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na
NLD, vilifikia makubaliano saba ya muungano wao ambayo ni pamoja na kuhusisha
sera zao na kuchukua yote yanayofanana ili viwe na kauli zinazolingana na
kufanana kwa Watanzania.
Pili; kusimamisha wagombea wa pamoja kwenye chaguzi zote
kuanzia serikali za mitaa, udiwani, ubunge, uwakilishi na urais kwa Jamhuri ya
Muungano na Zanzibar.
Tatu; kuweka utaratibu wa namna gani vyama hivyo
vingeshirikiana kwenye uchaguzi wa mitaa uliofanyika Desemba 2014 na Uchaguzi Mkuu
wa mwaka huu.
Nne; kushirikiana kuelimisha umma kupiga kura ya ‘Hapana’
katika mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na
Bunge Maalum la Katiba.
Tano; kujenga ushirikiano wa dhati katika mambo yote na
hoja zote za msingi zenye maslahi kwa Watanzania.
Sita; kuulinda Muungano bila kuwa na migongano ya kimaslahi
kama ilivyojitokeza kwenye katiba inayopendekezwa, na mwisho, kuhimiza na
kusimamia ushirikiano wa pamoja baina yao na asasi nyingine.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alizitaja taarifa
hizo kama propaganda za CCM kutaka kuharibu harakati za wapinzani nchini.
“Hizi ni taarifa za uongo uliopitiliza na propaganda za
CCM, hatuna haja ya kuzungumzia suala hilo kwa sababu mara nyingi wamemhusisha
Jaji Warioba na Ukawa wakati syo kweli,” alisema.
Aliongeza kwamba, Watanzania wanatakiwa kuelimishwa kuhusu
mambo ya msingi kama kura ya maoni ya katiba, daftari la kudumu la wapiga kura,
kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na mambo mengineyo ya msingi badala ya
propaganda.
Akizungumza na gazeti moja la kila siku mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alithibitisha kuwepo kwa kikao
hicho kesho Jumanne akisema kutakuwa na ajenda nyingine lakini: “Suala la
kupata wagombea nalo huenda likajadiliwa. Kuhusu suala la mgombea urais wa
Ukawa, linaweza kuwa sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda.”
Ajenda nyingine zitakazojadiliwa ni kura ya maoni ya
Katiba, changamoto za uandikishaji wa daftari la wapigakura, hali ya uchumi na
tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika Desemba mwaka jana.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema
watajadili ajenda hizo ili kuhakikisha wanatafuta majibu ya changamoto zilizopo
kwa sasa.
Kiongozi huyo pia alithibitisha taarifa kuwa kila chama
ndani ya Ukawa kupitia vikao vyake kitateua majina ya wagombea ambao
watashindanishwa ndani ya umoja huo, na kwamba kabla ya Machi, jina la mgombea
urais ndani ya chama chake litakuwa limeshapendekezwa.
CREDIT: DIRA YA MTANZANIA
No comments:
Post a Comment