Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu akimtambulisha Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (katikati) alipoitishia mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza mara baada kuhitimisha ziara zake Kanda ya ziwa. Kushoto ni Mshauri wa masuala ya haki za binadamu kutoka ofisi ya mratibu mkazi wa UN Tanzania, Bi. Chitralekha Massey.
Na Mwandishi wetu, Mwanza
MRATIBU wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la maendeleo la Umoja huo, UNDP, Alvaro Rodriguez ameutaka uongozi mkoa wa Mara kuanzia Polisi hadi serikali ya mkoa kuweka kipaumbele kumtafuta binti albino ambaye ametekwa na watu wasiojulikana siku 14 zilizopita.
Hayo aliyasema jana kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini
Mwanza baada ya kutembelea mkoa ya kanda ya ziwa ikiwemo Mara, Shinyanga na Mwanza kuangalia miradi inayotekelezwa na Umoja wa Mataifa pamoja na masuala ya haki za binadamu.
Alisema serikali kupitia Mkuu wa mkoa na Kamanda wa polisi mkoa wahakikishe wanaendelea kumtafuta na kulipa suala la Pendo Emmanuel (4) kipaumbele .
Pendo alitekwa na watu wasiojulikana baada ya mlango wa nyumba yao kuvunjwa Desemba 27,2014 kwa jiwe la fatuma katika kijiji cha Ndami tarafa ya Mwamashinda,wilayani Kwimba mkoani hapa ambapo hadi sasa bado hajapatikana.
Aidha aliwataka wananchi na viongozi kuhakikisha usalama wa watu wenye ulemavu kwani wao ni binadamu kama binadamu wengine na wanahitaji haki yao ya msingi ya kuishi bila hofu na manyanyaso kutoka kwa jamii inayowazunguka.
Mwakilishi huyo wa Umoja wa mataifa alisema katika mkutano huo kwamba hata kurundikana kwa watoto walemavu wa ngozi katika kituo cha Buhangija kilichopo Shinyanga ni matokeo ya mauaji yanayoendeshwa dhidi yao na kusema suluhisho la tatizo hilo ni jamii kuwakubali watu wenye ulemavu wa ngozi.
Tayari watu 15 wanashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi wa kuhusika na uporwaji wa mtoto huyo akiwemo baba mzazi, Emmanuel Shilinde.
Pamoja na kuzungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza, kuelezea ziara yake katika Ukanda wa Ziwa, Mwakilishi huyo pia alizuru wilaya ya Magu na kukagua mradi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ,UNICEF, wenye lengo la kuhakikisha haki inatetendeka dhidi ya wale wanaonyanyasa watoto na haki zao za kibinadamu zinahesmiwa.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza.
Akiwa Magu alifurahishwa na mashikamano unaoneshwa na serikali na wadau wengine kuhakikisha kwamba mradi huo unafanikiwa hasa katika kuwezesha watu kutambua haki za msingi za watoto na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto waliofanyiwa unyanyasaji na kuanzishwa kwa dawati la watoto na jinsia vituo vya polisi.
Hata hivyo aliambiwa changamoto zinazoambatana na ukusanyaji wa taarifa hasa katika maeneo ya ndani zaidi.
Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magese Mulongo, Umoja wa Mataifa na Serikali ya Mkoa walikubaliana kwamba usalama wa wananchi hasa watoto nay ale makundi maalumu ndio suala la msingi ambalo pande zote hizo mbili itatilia maanani.
Akiwa Shinyanga, Mwakilishi huyo Alvaro Rodriguez nalea kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa ngozi , wasiiona na viziwi Buhangija na kujionea hali halisi ya mrundikano wa watoto.
Kituo hicho kina watoto 220 wenye ulemavu wa ngzoi ambao walikimbiziwa hapo baada ya usalama wao kuwa shakani.
Alifurahishwa na juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali kuimarisha hali ya ustawi katika kituo hicho ambacho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mrundikano wa watoto, afya na lishe.
Mkutano na waandishi wa habari uliotishwa na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez ukiendelea.
Alisema akiwa hapo kwamba kama sehemu ya ajenda ya Umoja wa mataifa kusaidia kulinda haki za binadamu na kuhakikisha wale wanaoishi na ulemavu wa ngozi wanaendelea kustawi na haki zao zinaoheshimiwa, mwakilishi huyo alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kutoa msaada kwa kundi hilo.
Pia alifanya mazungumzo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na mkuu wa wilaya hiyo Anna Rose ambapo walikubaliana kwamba suluhu ya mwisho ni kwa watanzania kuwakubali wenye albinizim kama wenzao na kuacha kuwatafuta kuwaua kwa imani za kishirikina.
Akiwa mkoani Mara alishiriki katika hafla ya kutunuku vyeti wasichana na wavulana waliofuzu mafunzo ya miezi miwili yenye lengo la kuwaingiza katika jamii bila kukutwa au kufanyiwa tohara yenye maumivu (kwa wavulana).
Mafunzo hayo ni mchango wa Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la UNFPA wenye lengo la kukabiliana na mila potofu ikiwamo ya ukeketaji na mimba za utotoni zinazotokana na mabinti kuolewa wakiwa wadogo.
Katika mazungumzo na mkuu wa mkoa wa Mara, kapteni mstaafu Asery Msangi, Umoja huo ulikubaliana na serikali ya mkoa kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha haki za msingi za binadamu zinaheshimika na wananchi kuelimishwa kuhusu haki hizo.
No comments:
Post a Comment