Dk. Fenella Mukangara, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Na Benjamin Sawe, WHVUM
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara amewasihi wadau wa filamu kuongeza ujuzi na kubadilika ili kuendana na mabadiliko yanayotokea ulimwenguni katika masuala yanayohusu tasnia hiyo hasa katika suala zima la teknolojia ya uandaaji na usambazaji wa filamu.
Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa uuzaji wa filamu za Kitanzania kwa njia ya mtandao ambao mfumo huo umebuniwa na kampuni ya Proin Promotion Limited ya nchi.
Dr. Mukangara alisema hatua hiyo ni fursa muhimu katika kupanua wigo wa soko na kuendana na mabadiliko yanayotokea duniani katika kila nyanja ikiwemo mauzo ya filamu kwa nja ya mtandao.
“Ipo aja kwa wadau wetu kupanua eneo la mauzo ya kazi za filamu kwa kutumia mifumo ya kisasa katika usambazaji na uuzaji wa kazi ikiwemo mauzo na manunuzi kwa njia ya mtandao”.Alisema Dr. Mukangara
Alisema njia hiyo ikitumiwa vizuri itakuwa na faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wadau kuongeza idadi ya wanunuzi wa kazi za filamu kwani zitaweza kuwafikia watu sehemu mbalimbali ulimweguni kwa urahisi pamoja na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kushindana na wafanyabiashara wakubwa kupitia kazi watakazozizalisha.
Alizitaja faida nyingine nia pamoja na kupata wafadhili na misaada mbalimbali kutoka kwa wadau wa filamu ulimwenguni ikiwa ni pamoja na kupata faida zaidi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanunuzi wa kazi zao.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa Kampuni ya Proin Promotion, Johnson Lukaza alisema kunachangamoto ya jinsi ya kudhibiti maharamia wanaoiba kazi za wasanii amabazo wanazifanya kwa jasho na manufaa wanayopata huwa finyu.
“Tunatumaini njia hii huenda ikaleta nafuu ya kipato zaidi kulingana na hali ilivyo sasa kwa kuongeza wigo wa mauzo ambao kwa sasa utakuwa ni wa urahisi duniani kote,” alisema Lukaza.
Alisema kampuni yake hainunui haki za msanii bali inampa mrahaba wa kila nakala ambayo inauzwa ambapo mfumo huo unaongeza kila nakala ambayo itakuwa imenunuliwa hivyo kumfanya msanii kufaidika kwa kila nakala inayouzwa na kwa wakati wowote
“Sasa hivi wasanii watapata fursa ya kuuza kazi zao kupitia mtandaoni hata kaziwalizofanya miaka ya nyuma na kuanza kufaidika tena pamoja na vizazi vyao,” alisema.
No comments:
Post a Comment