Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 28 January 2015

WANASAYANSI ‘BONGO’ KUSAFISHA MAJI YA KINYESI KUWA YA KUNYWA


Na Florence Majani, Mwananchi
Dar es salaam. Umeshikwa na kiu? Unaingia katika duka lililo jirani na kununua maji ya chupa kwa ajili ya kunywa. Lakini ukapatwa na udadisi kutaka kujua maji hayo yametengenezwa na nini. Unaposoma kilichotumika kutengeneza maji hayo, unagundua kuwa yametengenezwa kwa kinyesi.
Je, utakunywa au kiu yako ya maji itakatika kwa kinyaa na mshangao.
Kama ilivyowezekana Marekani katika Kampuni ya Janicki Bioenergy, ndivyo itakavyowezekana hapa nchini, baada ya wanasayansi kuwa katika mpango wa kusafisha maji yenye kinyesi kuwa ya kunywa.
Baada ya Kitengo cha Utafiti cha Idara ya Uhandisi, Teknolojia na Madini (COET) kufanikiwa kusafisha majitaka kuwa maji yanayofaa katika kilimo cha umwagiliaji na kunywesha mifugo, sasa wanasayansi hao wanajiandaa kusafisha maji ya kinyesi kuwa ya kunywa.
Mkuu wa COET, Profesa Jamidu Katima anasema idara ya utafiti ya chuo hicho inatarajia kukamilisha utafiti huo katika siku za usoni.
“Tupo katika mchakato baada ya kuwa tumemaliza awamu hii ya kwanza na kufanikiwa. Baadaye, tutasafisha maji haya ya kinyesi kuwa maji safi kabisa yanayofaa kunywewa na binadamu,” anasema Profesa Katima.
Wanasayansi hawa hawakufanya kazi hii kimzaha, bali walianza kwa mifano hai kwa kukitumia Kiwanda cha Mvinyo wa Banana kilichokuwa kinazalisha majitaka zaidi ya lita 80,000 kwa wiki.
Teknolojia hiyo ilisafisha majitaka hayo yaliyokuwa na kemikali na ndizi zilizotumika katika kutengeneza mvinyo na kuyasafisha.
“Ipo mitambo maalumu ya kusafisha majitaka hayo. Maji hayo husafishwa na kuwa masafi kiasi cha kuweza kutumika katika umwagiliaji wa mazao na hata wanyama kunywa,” anasema Profesa Katima.
Hata hivyo, kwa sasa wanasayansi hao bado hawajafikia hatua ya kusafisha majitaka haya kuwa salama yanayofaa kunywa.
Akizungumzia Teknolojia hiyo, Mkurugenzi wa Costech, Dk Hassan Mshinda anasema huu ni wakati wa taifa kutumia sayansi na teknolojia katika kukuza uchumi wa kilimo na viwanda.
“Huu ni mradi muhimu sana kwa sababu teknolojia hii inasaidia si tu kupata maji masafi yanayofaa kwa matumizi mengine, pia yanasafisha mazingira,” anasema.
Dk Mshinda anaongeza kuwa majitaka ya viwandani yanaharibu mazingira na kusema kuwa iwapo yatasafishwa, yataepusha mambo mengi ikiwemo maradhi.
Anasema kuwa Costech inajivunia kufanya kazi za kisayansi kwa kushirikiana na sekta binafsi na zile za Serikali huku akiisisitiza Serikali kutumia tafiti za wanasayansi. Profesa Katima anaeleza kuwa watu hawajaona umuhimu wa kutibu majitaka yanayozalishwa viwandani kwa sababu wanaona ni gharama kubwa.
“Wenye viwanda wanatakiwa kuwa na mwamko katika kuifanya teknolojia hii,” anasema Profesa Katima
Teknolojia hii si kwa sababu ya kuzalisha maji safi tu, bali inalenga pia kusafisha mazingira kwa sababu majitaka haya yanapozagaa huingia katika vyanzo vya maji na pengine kutumiwa zaidi.
Mmiliki wa kiwanda cha mvinyo wa ndizi, Adolf Ulomi anasema kabla ya kuanza kutumia teknolojia ya kusafisha majitaka, kiwanda chake kilitumia mfumo wa kutapisha.
Walichimba mashimo ya kujaza majitaka hayo na kila shimo lilipojaa , shimo jingine lilichimbwa na kutengenezwa mfereji wa kuingiza majitaka katika shimo jipya.
Baada ya kuzungumza na wanasayansi wa COET, ndipo Ulomi alipoamua kukubali kutumia zaidi ya Sh800 milioni ili watumie teknolojia hiyo.
“Baada ya miaka miwili tu, mtambo wa kusafisha majitaka ulikuwa tayari. Tukaanza kuyatumia maji yaliyosafishwa katika kilimo cha ndizi ambazo tunalima wenyewe kwa ajili ya kutengeneza mvinyo,” anasema.
Mbali na maji hayo kutumika katika kilimo cha umwagiliaji, pia wanatarajia kutumia maji hayo kutengeneza mabwawa ya kufuga samaki. Teknolojia hiyo haikuishia hapo, kwani majitaka yanayosafishwa pia yanazalisha gesi ambayo hutumika kama nishati ya kuendesha mitambo.
Profesa Katima anasema urejelezi wa aina hiyo una manufaa zaidi kwani unasaidia kusafisha mazingira.
“Unajua viwanda vinazalisha kemikali nyingi hatari, lakini iwapo maji yanayotiririshwa kutoka viwandani yatasafishwa ni dhahiri kuwa tutapunguza hatari ya kupata maradhi,” anasema na kuongeza:
“Ndiyo maana siku hizi kuna magonjwa mengi ambayo hata hayaelezeki kwa sababu ya maji yanayotiririshwa viwandani.”
Anaeleza kuwa ni vyema majitaka yaliyosafishwa yakatumika katika umwagiliaji badala ya kutumia majisafi ambayo yangefaa kwa kunywa na katika kilimo.
Profesa Katima anaeleza kuwa, maji ya viwandani yana hatari endelevu ambayo katika mchakato wake, huwadhuru pia hata wale wenye viwanda.
Anatoa mfano kuwa, iwapo majitaka yenye kemikali yataingia kwenye vyanzo vya maji, ina maana samaki watapata kemikali hiyo na wanyama kama ng’ombe watakunywa kemikali hizo na baadaye binadamu hunywa maziwa au kula samaki.
Umuhimu wa kinyesi
Mtaalamu wa Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Fredrick Mwanuzi anasema wakati umefika sasa kinyesi cha binadamu kichukuliwe kama malighafi badala ya uchafu na kutumia mbolea hiyo kwa ajili virutubisho vya kilimo, nishati, pamoja na dawa za binadamu.
“Kilo 25 hadi 50 za kinyesi huzalishwa na mtu mmoja kwa mwaka, hii ni sawa na kilo 0.55 nitrogen, 0.18 phosphorus na 0.37 potassium, vilevile binadamu huzalisha kiasi cha lita 400 za mkojo kwa mwaka ambazo huwa na kg 4.0 nitrogen, 0.4 phosphorus na 0.9 za potassium,” anasema. Utafiti huu wa kusafisha majitaka ulianza kufanywa na COET tangu mwaka 1995.
Hata hivyo, Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kutumia teknolojia hiyo, tayari Marekani imejenga kiwanda kinachotumia kinyesi cha binadamu kwa ufadhili wa Taasisi ya Bill & Melinda Gates kikijulikana kwa jina la Omniprocesser huko Seattle, Marekani kupitia Kampuni ya Janicki Bioenergy.
Baada ya kunywa maji safi yaliyotokana na kinyesi Gates alinukuliwa akisema: Maji yalikuwa na ladha nzuri kama maji mengine ya chupa niliyowahi kunywa. Baada ya kujua siri ya uhandisi huo, nitafurahia kuyanywa kila siku.”
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment