Mwanariadha Rita Jeptoo
Kesi ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu ya bingwa mara tatu wa Boston Marathon Rita Jeptoo wa Kenya imeanza leo hii mjini Nairobi lakini chama cha riadha kimesema hakitatangaza hukumu ya Jeptoo hadi wiki ijayo.
Rita Jeptoo ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhojiwa akiandamana na shangazi yake na wakili.
Alihojiwa kwa saa tano kuanzia saa nne za Afrika Mashariki kisha kocha wa Jeptoo Claudio Bardardeli akaingia..na baada ya dakika chache Jeptoo akaitwa tena ndani.
Jeptoo amepatikana na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu lakini kabla ya chama cha riadha kumhukumu Jeptoo anapewa nafasi ya kujitetea.
Wengine walioko huko ambao watahojiwa pia ni ajenti wa Jeptoo Federico Rosa na bwanake Jeptoo Noah Busienei ambaye wametengana.
Victor Bargoria wa tume ya kupambana na dawa za kuongeza nguvu ya chama cha riadha cha Kenya ndiye anayeongoza kesi hiyo na afisa mwingine wa tume hiyo Jessica Shiraku.
Kwa upande wa chama cha riadha cha Kenya waakilishi wao ni naibu wa Rais Jack Tuwei na mkurugenzi mkuu Isaac Mwangi na serikali pia ina mwakilishi wake.
Kulingana na Rais wa chama cha riadha cha Kenya Isaiah Kiplagat kesi hiyo itamalizika kesho kisha wiki ijayo watatagaza hukumu yao.
Huenda Jeptoo akafungiwa kwa miaka miwili, adhabau ambayo itamnyima nafasi ya kupokea kitita cha dola mia tano elfu kwa kuwa mshindi mfululizo wa mbio sita mashuhuri za marathon msimu uliopita.
Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanariadha wanaotumia dawa za kusisimua misuli, serikali imeamua kuanzia msimu huu ni wao watawasajaili maajenti wa ng'ambo baadhi yao ambao wanashukiwa kuwapa wanariadha wa Kenya dawa hizo za kuongeza nguvu, huku wengine wakidai dawa hizo ziko hapa hapa Kenya.
CREDIT: BBC
No comments:
Post a Comment