Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetupa rufani ya timu ya Mwanza kupinga uhalali wa wachezaji wawili wa Kigoma kwenye mechi yao ya robo fainali iliyochezwa jana (Januari 26 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mwanza iliyopoteza mechi hiyo kwa mabao 2-1 iliwalalamikia wachezaji Neema Sanga na Vene Dickson wa Kigoma kuwa waliwahi kuchezea timu ya Taifa (Twiga Stars), hivyo kucheza mashindano ya Kombe la Taifa la Wanawake ni kinyume cha kanuni.
Kamati baada ya kupitia rufani hiyo, imeitupa kwa vile timu ya Mwanza haikuwasilisha vielelezo vyovyote kuthibitisha madai hayo dhidi ya wachezaji hao. Pia Kamati yenyewe ilipitia taarifa za Twiga Stars ambapo haikupata kumbukumbu za wachezaji hao katika timu hiyo.
Pia Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imesikitishwa na kitendo cha viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) Mkoa wa Mwanza kugomea uamuzi dhidi ya rufani yao, hivyo imependekeza Mwenyekiti wa TWFA Mwanza, Sophia Tigalyoma na Katibu wake Hawa Bajanguo wapelekwe Kamati ya Nidhamu kwa hatua za kinidhamu.
No comments:
Post a Comment