
Maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Rose Kitambi na Michael Sanga (katikati) wakikagua mbolea iliyorundikwa nje ya Kampuni ya Obo Investment jijini Mbeya juzi. Kushoto ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ole Senga. Picha na Lauden Mwambona
Na Lauden Mwambona, Mwananchi
Mbeya. Kampuni tatu zinazouza mbolea jijini hapa, juzi zilitishiwa kufungiwa maduka yao na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) baada ya kuvunja sheria za mauzo.
Mtaalamu wa mbolea kutoka TFRA, Rose Kitambi alisema
jana kuwa kampuni hizo zilikutwa na makosa tofauti walipofanya ukaguzi katika maduka na maghala yao.
Miongoni mwa kampuni ‘zilizoonja’ ukali wa TFRA ni Export and Trading Ltd ambayo wafanyakazi wake walikuwa wakihamisha mbolea kutoka kwenye mifuko iliyodaiwa ya zamani kuingiza kwenye mifuko mipya.
Mwakilishi wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Minoj S alisema walihamisha mbolea kwenye mifuko 50 ya zamani na kuiweka kwenye mipya kwa kufuata masharti ya mteja.
Akizungumzia hilo, Kitambi alisema kitendo cha kuhamisha mbolea kwenye mifuko ni kuvunja sheria inayowataka wauzaji wafanye kazi hiyo chini ya uangalizi wa maofisa maalumu wa Serikali.
Alisema mbolea lazima itunzwe mahali pazuri bila kuchanganywa na mbegu au dawa za aina yoyote, pia hairuhusiwi kuuza kwa kilo kama sukari.
Nao wamiliki wa Kampuni ya Obo Investment walipata onyo baada ya kushindwa kuonyesha leseni inayowaruhusu kuuza mbolea ambayo pia walikuwa wameiacha juani.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ole Senga alisema anayo leseni, lakini hakumbuki alipoitunza na kwamba aliweka mbolea nje kwa sababu alikuwa akifanya marekebisho ndani ya jengo lake.
Maofisa wa Kampuni ya Tanzania Farmers Association (TFA) walionywa kuuza mbolea isiyosajiliwa.
Kutokana na hilo, wauzaji wametakiwa kutouza mbolea hiyo ya maji inayoitwa Booster kwa kuwa Serikali haiitambui.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment