Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana, amesema Benki ya Dunia (WB) imekithiri kwa urasimu ambao badala ya kuzisaidia nchi masikini duniani imekuwa ikizinyonya.
Aidha, ameitaka serikali kuongeza juhudi za kuwa na uwezo wa kujitegemea kuliko kusubiri misaada kutoka nje ya nchini.
Kinana alitoa kauli hiyo juzi wilayani Handeni, mkoani Tanga wakati akizindua mradi wa maji, unaojengwa na serikali kwa ufadhili wa WB ambao umeshindwa kukamilika kwa zaidi ya miaka 10.
Alisema Tanzania pekee haiwezi kupinga sera, kanuni na taratibu za WB zinazoinyonya bali nchi masikini zikiungana zinaweza kuifanya Benki hiyo kubadili mifumo yake.
“Mradi wa maji wa serikali ulianza tangu mwaka 2008 ambao unalenga vijiji 10 kwa kila wilaya, lakini hadi sasa hakuna mafanikio yoyote na ni mwaka wa 10 huu, sababu kubwa ni urasimu uliokithiri,” alisema Kinana.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa mkopo ambao utalipwa na fedha za Watanzania wenyewe na hakuna sababu ya kuuita mradi wa msaada wa Benki ya Dunia.
Alifafanua kuwa, benki hiyo ina uwezo wa kuondoa umasikini kwa nchi masikini duniani kama itaamua ila kwa sasa inachokifanya ni kunyonya nchi masikini kwani wamekuwa hawatimizi sera ambazo ziko kwenye mkataba wa mikopo wanayotoa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment