Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio, Nuru Kalufya akisimamia usajili wa washiriki wa mafunzo ya Maadili, Jinsia na Kuandika Habari za Migogoro yaliyoanza katika kijiji cha Uvinza, wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma tarehe 24 Septemba hadi 01 Oktoba 2014.
Na Mwandishi Wetu, Uvinza
Imethibitishwa kwamba mfumo dume ulioota mizizi katika jamii kwa kisingizio cha mila, desturi na dini unachangia kwa kiasi kikubwa katika unyanyasaji wa mtoto wa kike na mwanamke nchini.
Hayo yalithibitishwa na washiriki wa mafunzo ya maadili na jinsia yanayofanyika katika kijiji cha Uvinza mkoani Kigoma wakati wakichangia mada ya Jinsia na Vyombo vya Habari iliyowasilishwa na mkufunzi kutoka Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Bi Rose Haji Mwalimu.
Mshiriki kutoka Loliondo Joseph Munga ambae alizungumzia jinsi gani mfumo dume mgando unavyonyima haki za mtoto wa kike wa Kimasai, alisema kwamba mtoto wa kike hapaswi kwenda shule, kuna kiwango cha juu cha shinikizo la ndoa za utotoni, ukeketaji na wanawake kutokuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi.
“Ubaguzi unaanza katika familia, mtoto wa kike hana haki ya kuchagua mume anayemtaka au lini aolewe. Mtoto huyo huyo ni lazima akeketwe kwa sababu mtoto wa kike asiyekeketwa anaonekana ni laana katika familia na hawezi kupata mume. Kutokana na sababu hizo watoto wa kike huridhia kukeketwa ili waondoe laana hiyo lakini pia kwa kushinikizwa na wazazi wa kike.”
Hadi leo haijathibitishwa ni laana gani huwapata wasichana wasiokeketwa kwa maana kuna baadhi yao ambao hawakukeketwa, wameolewa na wanaendelea na maisha ya kawaida.
Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Maadili, Jinsia na Kuandika Habari za Migogoro katika maandalizi ya uchaguzi mkuu 2015.
Akizungumzia kuhusu uwakilishi kufikia 50/50 ifikapo mwaka 2015, Munga alisema kwamba bado kuna changamoto kubwa kwa mwanamke wa Kimasai kusimama na kugombea nafasi za uongozi kutokana na wanawake kutopewa nafasi ya kutoa maamuzi katika jamii ya Kimasai. Mathalani, moja ya tabia za mfumo dume mgando katika jamii hiyo ni mila na tamaduni za Kimasai ambapo mwanamke haruhusiwi kushiriki katika uongozi wa rika “laigwanang” kwa sababu jamii ya Kimasaia inamlinganisha mwanamke na kumchukulia kama mtoto mdogo “nagara, ngara au ngarai”.
“Nafasi ambazo mwanamke anaweza kufaidika nazo ni zile za kuteuliwa tu basi,” alifafanua Munga.
Naye mshiriki kutoka kisiwani Tumbatu Ali Khamis alisema kwamba katika jamii yao mwanamke hana haki ya kutoa maamuzi katika ngazi ya familia na haruhusiwi kuhudhuria vikao vya harusi na misiba. Katika uongozi hali pia hairidhishi.
“Katika kisiwa cha Tumbatu viongozi wote wa ngazi za juu katika siasa ni wanaume. Ukianzia Afisa Tawala, masheha na madiwani ni wanaume, yupo mwanamke mmoja tu ambae ni wa kuteuliwa,” alisema Khamis.
Pemba ina majimbo 18 lakini hakuna mwanamke wa kuchaguliwa kisiasa wakati huo huo kisiwa cha Unguja ambacho kina majimbo 32 kuna wanawake watatu tu wa kuchaguliwa.
Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO akisisitiza jambo katika mafunzo yanayowashirikisha waandishi wa habari na watangazaji kutoka redio jamii nane nchini.
Mshiriki mwingine kutoka Uvinza mkoani Kigoma Leah Kalokoza alisema kwamba unyanyasaji kijinsia ni wa kiwango cha juu katika jamii inayouzunguka mji huo. Alisema kuwa mgawanyo wa kazi katika familia hauna uwiano kati ya mwanamke na mwanaume maneno ambayo pia yalithibitishwa na Balozi wa Barabara ya Kasulu Bi. Tabu Ramadhani.
“Wanawake ndio wanaotafuta riziki hususan kuvuna chumvi kazi ambayo ni ngumu sana, kulima na kulea watoto. Wanaume kazi yao ni kuuza chumvi hiyo, kukaa magengeni na kula hotelini wakati watoto nyumbani hawana chakula, kwa kweli wanatunyanyasa waume zetu.”
Tegemeo kubwa la kipato cha Uvinza ni chumvi pamoja na kwamba kwa kiasi kikubwa kipato hicho kimeshuka baada ya kiwanda hicho kubinafsishwa na mwekezaji mwenye asili ya Kiasia.
Akizungumzia uhuru wa kujieleza, Leah Kalokaza alisema kwamba wanawake hawaruhusiwi kuwasiliana na vyombo vya habari bila idhini ya waume zao. Tamko la Dunia la Haki za Binadamu kuwa na Haki ya Uhuru wa Kujieleza Ibara ya 19, linasisitiza uhuru wa kujieleza ni haki ya kila mtu, awe mwanamke au mwanamume.
Kutoka Mpanda mkoani Rukwa wanawake wananyanyaswa kwa kunyimwa elimu, kutokuwa na haki ya kumiliki kama ilivyo katika jamii nyingine na pia utu wao hudhalilishwa pale mabango katika nyumba za kulala wageni huwa yanakuwa na picha au ujumbe dhahiri wa mfumo dume.
Mambo mengine yanayochangia udhalilishaji wa wanawake ni nyimbo mbalimbali ambazo humsifu mwanamume na kumkashifu mwanamke hususan sehemu za Usukumani.
“Kwa mfano, kuna Wimbo unaosema, ‘kuzaa mtoto wa kiume jamii yote inafurahia, kuzaa mtoto wa kike ni maandalizi ya sherehe. Hii inaonyesha ni kwa namna gani mwanamke katika tamaduni za Kisukuma hana hadhi hata mbele ya mtoto aliyemzaa mwenyewe,” alisema Anatory John.
Mkoa wa Shinyanga umekumbwa na wimbi kubwa la mauaji ya vikongwe wanawake kwa tuhuma za uchawi, lakini ikija kwenye uganga wa jadi hawatambuliki.
“Waganga wengi wa Kisukuma ni wanaume kwa imani kwamba wanawake hawana uwezo wa kuzungumza na mizimu au miungu”, alielezea Anatory.
Vyote hivyo ni viashiria vya mfumo dume au mawazo mgandoyanayoendeleza tabia ya kumwona mwanamke ni mtu duni na mwanamume ni mtu mwenye uwezo wa pekee.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea kupata darasa kutoka Mkufunzi wao Bi. Rose Haji Mwalimu Uvinza mkoani Kigoma.
Kipengele cha Vyombo vya Habari katika Itifaki ya SADC kuhusu Jinsia na maendeleo kinaazimia kuhakikisha kuwa jinsia inaingizwa katika habari, mawasiliano na sera za vyombo vya habari, mipango, vipindi, sheria na mafunzo kulingana na Itifaki ya Utamaduni, Habari na Spoti.
Azimio la Jinsia na Maendeleo lililotolewa na Viongozi wa Umoja wa Maendeleo Kusini mwa Afrika au Serikali (SADC) linasisitiza uwakilishi wa uongozi katika ngazi ya maamuzi 50/50 ifikapo mwaka 2015.
Warsha ya Maadili na Jinsia inalenga kuwapa uwezo waandishi na watangazaji wa redio za jamii nchini kuandika habari zinatoa changamoto za mfumodume/mgando na matumuzi ya Lugha nyepesi inayohusisha jinsia zote bila kubagua hasa katika kipindi hiki tunakoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi wa raisi mwaka 2015.
Warsha hii ya siku nane ilijumuisha waandishi wa habari wa redio jamii 48 kutoka redio 8 za jamii Tanzania Bara na Visiwani.
Mradi huu unatekelezwa kwa pamoja kati ya UNESCO na Vyombo vya habari Jamii chini ya mtandao wa COMNETA na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP.
Washiriki wa mafunzo ya Maadili na Jinsia katika vyombo vya habari wakiwa katika vikundi kazi.
Mshiriki wa mafunzo kutoka Redio Loliondo FM, Joseph Munga akichangia mada ya Jinsia na vyombo vya Habari katika mafunzo ya siku nane ya kuzipa uwezo redio jamii kuandika habari chanya cha uchaguzi na migogoro.
Mshiriki kutoka Tumbatu FM Radio Kisiwa cha Tumbatu, Unguja Ali Khamis akizungumzia changamoto za mfumo dume na mawazo mgando yanayodumaza maendeleo ya mwanamke.
Pichani ni mshiriki na mwandishi wa habari Uvinza FM Radio, Uvinza- Kigoma Leah Karokaza akichanganua masuala yanayoendeleza unyanyasaji wa kijinsia wilayani Uvinza.
Anatory John kutoka Baloha FM Radio, Kahama akichanganua baadhi ya misemo na nyimbo zinazomdhalilisha mwanamke.
“Mabango yanayotundikwa katika nyumba za kulala wageni yanadhalilisha sana wanawake”, ndivyo asemavyo Sharifa Selemani kutoka Mpanda FM Radio, Mpanda mkoani Rukwa katika picha.
Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki wa mradi wa kuzipa uwezo uwezo redio jamii katika mchakato wa uchaguzi mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment