Suala la ugawaji wa madaraka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania na Rais wa Zanzibar kwenye Rasimu ya Katiba inayopendekezwa limewagawa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba (BMK).
Mgawanyiko huo umehusu zaidi eneo la kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine ya kiutawala.
Baadhi ya wajumbe wanataka Rais wa Zanzibar apewe mamlaka kamili ya kuigawa Zanzibar, huku wengine wakitaka asifanye hivyo mpaka pale atakapokuwa amekasimishwa mamlaka hayo na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Hayo yalidhihirika wakati Kamati 12 za BMK zikiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya rasimu ya Katiba inayopendekezwa, iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge.
Maoni ya kamati hizo yalionekana kukinzana kuhusiana na Ibara ya 2 (2) inayohusu mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine ya kiutawala.
Ibara hiyo ya 2(2), ya rasimu inayopendekezwa inasomeka hivi: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa na mamlaka ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine na kwa upande wa Zanzibar Rais anaweza kukasimisha mamlaka hayo kwa Rais wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa kamati namba mbili, Shamsa Mwangunga, alisema maneno ‘anaweza’ na neno `kukasimu’ yaondolewe na badala yake ibara hiyo isomeke kuwa Rais atakasimu mamlaka hayo kwa Rais wa Zanzibar.
Aidha maoni ya Kamati namba saba yaliyowasilishwa na Merina Thomas, yalipendekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa na mamlaka ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine kwa upande wa Tanzania Bara pekee.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, mamlaka hayo yawekwe chini ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Hata hivyo, maoni hayo yalipingwa na Kamati namba tatu na kamati namba 10 zilizopendekeza kuwa mamlaka hayo yawe ya Mkuu wa nchi pekee ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Walipendekeza kuwa anapohitaji kufanya hivyo kwa upande wa Zanzibar, kwanza ashauriane na Rais wa Zanzibar.
Mwenyekiti namba tatu, Dk. Francis Michael, alipendekeza hata upande wa Zanzibar, Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye awe na mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika maeneo ya kiutawala.
Alisema kuwa suala hilo linapaswa kufanywa kwa idhini ya mkuu wa nchi ingawa katiba inaweza kutoa fursa ya Rais wa Jamhuri kushauriana na Rais wa Zanzibar kabla ya kufanya hivyo.
Mwenyekiti wa Kamati namba 10, Anna Abdallah, alisema suala hilo linapaswa kuwa la Rais wa Jamhuri hata kwa upande wa Zanzibar kwa kuwa baada ya kugawanywa kuna mambo ya Muungano ambayo yatahitajika.
Alisema siyo busara kumwacha Rais wa Zanzibar aigwe Zanzibar katika maeneo mbalimbali ya kiutawala ambapo baada ya kufanya hivyo kuna mambo yanayohitajika kufanyika ambayo yatahitaji gharama kutoka kwenye Serikali ya Muungano.
Suala lingine ambalo `lilivaliwa njuga’ na kamati nyingi kutaka liingizwe kwenye rasimu ya Katiba inayopendekezwa ni uanzishwaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment