Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 25 September 2014

WANAFUNZI WA CHEKECHEKEA TUNDURU WASOMEA CHINI YA MTI

Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakiwa wamekaa chini na mwalimu wao pembeni kuonesha sehemu ambayo hutumika kama darasa wawapo masomoni.

WANAFUNZI wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wanasomea chini ya mti kutokana na darasa hilo kuendeshwa bila ya kuwa na chumba maalum kwa ajili ya kusomea wanafunzi hao.

Hali hiyo imebainika baada ya mwandishi wa habari hizi kuitembelea shule hiyo hivi karibuni na kuwakuta wanafunzi wakiwa wamekaa chini huku wakiendelea na masomo hayo nje chini ya mti ulio na kivuli cha kuwahifadhi wakati wa jua kali.

Akizungumza shuleni hapo Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nakayaya, Christina Mhowera alisema watoto hao wamelazimika kusomea nje baada ya huduma ya elimu hiyo kuanzishwa shuleni hapo bila ya kuwa na jengo maalum kwa wanafunzi wa awali.

Alisema awali wanafunzi hao walikuwa wakisomea kwenye gofu (jengo mbovu) lililokuwa jirani na shule, lakini walilazimika kuondolewa baada ya jengo hilo kutwaliwa kwa matumizi mengine. Aliongeza kuwa baada ya hapo walihamishiwa kwenye nyumba ya mwalimu kabla ya kukamilika lakini waliondolewa tena na kuanza kusomea nje (chini ya mti) hadi sasa.

Alisema darasa hilo lenye jumla ya wanafunzi 92 linaendeshwa bila ya kuwa na chumba cha darasa maalum wala madawati kutokana na shule hiyo kukabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa hadi hapo watakapopata darasa maalum kwa ajili ya wanafunzi hao.

Kwa upande wake mwalimu wa darasa hilo, Teckla Milanzi alisema mbali na darasa hilo kutokuwa na chumba cha darasa, linakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ya uhaba wa vitendea kazi kama vitabu na vyenzo zingine za kufundishia na hakuna bajeti yoyote inayotumwa kuliwezesha darasa hilo.

Aidha uchunguzi uliofanywa katika shule nyingine tatu za Wilaya ya Tunduru, yaani Shule ya Msingi Nanjoka, Majengo na Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko kuangalia mazingira ya utoaji elimu ya awali katika shule hizo umebainisha kukabiliwa na changamoto nyingi hali ambayo inahatarisha msingi wa elimu kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka, Batadhari Mkwela alisema licha ya usajili wa wanafunzi wa awali kuongezeka kila mwaka kumekuwa hakuna bajeti ya kuendesha elimu hiyo.
“…Darasa la awali linahitaji vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha, vyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini, hatuna madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” alisema Mkwela.

Akizungumzia hali hiyo, Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe alisema vyumba vya madarasa ni changamoto kubwa eneo hilo licha ya msisitizo kuendelea kutolewa wa kila shule ya msingi kuwa na darasa la awali. Alisema mwaka 2013/14 halmashauri ya wilaya hiyo ilihitaji zaidi ya milioni 366.7 lakini ililetewa zaidi ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu tu ya kiasi kilichopitishwa kwenye bajeti hiyo. 

“…Kwa hiyo unaweza kuona kwamba ni ngumu kuigawa fedha hii katika matumizi maana kwanza haitoshi na pili hata kilichotegemewa kuja ni pungufu zaidi tena sana, sasa sijui unaweza kugawa kila shule ipate shilingi ngapi…kwani haitoshelezi,” Abdul Kazembe.

Akifafanua zaidi Kaimu Ofisa Elimu huyo alisema miundombinu ya madarasa ni changamoto kubwa, kwani mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa wilaya nzima ilikuwa ni 1,715 lakini madarasa yaliopo ni 900 na kitu huku mengine yakiwa ni ya muda mrefu na yanaelekea kuchakaa.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com

No comments:

Post a Comment