Baada ya kushusha burudani ya aina yake katika mikoa
ya Iringa na Morogoro wiki iliyopita, Tamasha la Serengeti Fiesta 2014
linaendelea na sasa limejipanga kwa ajili ya kuwasha moto kwa wakazi wa mji wa
Songea na viunga vyake kwa mara ya kwanza katika historia ya tamasha hilo
nchini. Burudani hiyo ya kihistoria itafanyika leo katika Uwanja wa Majimaji
mjini humo.
Kila kitu kipo sawa kwa upande wa kampuni ya bia ya
Serengeti ambao ndio wadhamini wakuu wa shoo na safari zote za Serengeti Fiesta
mwaka huu ambazo zimekuwa za mafanikio makubwa, ziara za tamasha hilo zinakaribia
kufika kikomo chake hapo Oktoba 18.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa waandaaji wa
tamasha hilo, wasanii wanaotarajiwa kutoa shoo katika Uwanja wa Majimaji mjini
Songea leo ni pamoja na Godzilla, TID, Linex, Mr. Blue, Madee, Stamina,
Barnaba, Ney wa Mitego, Linah, Recho, Mo Music na Baraka Da Prince.
Kabla ya wasanii hao kupanda jukwaani na kutoa shoo
usiku huu, baadhi ya shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo Serengeti Super
nyota diva. Shughuli yenye lengo la kumtafuta mwanadada mwenye kipaji cha
kuimba toka katika mji huo wa Songea ili aje kushuhudia tamasha la mwisho
jijini Dar es Salaam. Lengo la Serengeti katika shughuli hiyo ni kuwasaidia vijana
na kuendeleza vipaji vyao kama ilivyokuwa kwa Young Killer.
Wakati maandalizi ya shoo yakikaribia, Meneja wa
kinywaji mama cha Serengeti Premium Lager, Ndugu Rugambo Rodney alizungumza na waandishi
wa habari na kusema......“Songea ni mkoa ambao Serengeti Fiesta inapita kwa
mara ya kwanza katika historia ya maonyesho ya tamasha hili nchini
Tanzania..... napenda kuwajulisha wakazi wa Songea kwamba shoo zetu ni za pekee
na kwamba tupo tayari ku “Sambaza Upendo” leo katika mkoa wao. Pia nataka
kuwahakikishia kwamba tutatoa shoo bora na nzuri ambayo hamjawahi kuiona katika
mkoa wenu, tunatarajia mtajitokeza kwa wingi kushuhudia baadhi ya wasanii ambao
hawajawaji kutoa burudani katika mkoa wenu.”
Katika kuliweka wazi suala la ulinzi uwanjani hapo,
Rodney alisema “Walinzi watakuwepo kila eneo uwanjani hapo kama ambavyo ilikuwa
katika shoo zilizopita.”
Songea utakuwa mkoa wa 13 ambao tamasha hilo la
Serengeti Fiesta limepita na kufanya shoo zake kwa mwaka huu. Mtwara, Mbeya,
Dodoma na Dar es Salaam ni mikoa ambayo inasubiri kwa hamu kuonja ladha ya
tamasha hilo lililojizolea umaarufu toka kila kona ya mikoa ambayo limepita.
No comments:
Post a Comment