Jaji mstaafu Joseph Warioba
Dar. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameandika waraka kumjibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira kwa kauli yake kuwa ndiye aliyemkimbiza CCM kwenda upinzani mwaka 1995.
Katika waraka wa maandishi alioutuma kwa gazeti hili, Jaji Warioba alisema maelezo ya Wasira dhidi yake katika mahojiano maalumu na gazeti hili hayakuwa sahihi na hivyo akamtaka ajifunze kusema ukweli kwa kuwa mambo anayosema yanaweza kumrudia baadaye.
Tarehe 22 Septemba 2014, Gazeti la Mwananchi lilitoa taarifa ya mahojiano kati yake na Mheshimiwa Steven Wasira. Katika mahojiano hayo, Mheshimiwa Wasira alisema mimi ndiye niliyemkimbiza CCM.
Tangu mchakato wa Katiba Mpya kuanza nilikuwa napata taarifa kwamba Mheshimiwa Wasira alikuwa amenifanya mtaji wake katika kutetea msimamo wake. Wakati mmoja kuna kiongozi mwenzake aliniuliza kama nina ugomvi binafsi na Mheshimiwa Wasira kwa sababu kila akipata nafasi kwenye vikao vyao ananishambulia. Wakati wa mabaraza ya Katiba nilipata taarifa za aina hiyo. Nilichofanya ni kuwaarifu viongozi wake wa CCM.
Mengi aliyosema Mheshimiwa Wasira siyo ya kweli. Napenda nitoe ufafanuzi kwa machache yafuatayo:-
Niligombea mara mbili na Mheshimiwa Wasira. Baada ya Uchaguzi wa 1990 ambao nilishinda kwa kura nyingi sana, uchaguzi huo ilitenguliwa kwa sababu nilifanya kampeni kwa kutumia gari la Waziri Mkuu.
Uchaguzi ulirudiwa mwaka 1992. Niliunda timu ya kampeni, Mheshimiwa Wasira akiwa kiongozi. Aliniomba atangulie jimboni kuandaa mazingira. Alipofika huko akaanza kampeni dhidi yangu na kutangaza kwamba anagombea. Wakati huo kura za maoni zilikuwa zinapigwa na wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya. Wajumbe walikuwa kama 600. Nilipata kura 400 na Mheshimiwa Wasira alipata kura chache akiwa mtu wa tatu au nne. Baada ya matokeo akatangaza anajitoa kwenye mchakato na jina lake lisipelekwe NEC. Alikataliwa kwa sababu kufuatana na kanuni, muda wa mtu kujitoa ulikuwa umepita.
Mwaka 1995, kura za maoni zilikuwa zinapigwa kwenye kata. Tulianza na Kata ya Sarama ambayo iko upande wa mashariki, siku ya tatu tulifika Nyamuswa ambacho ndicho kijiji ninachotoka. Nyamuswa ilikuwa kituo cha tano kati ya vituo 12.
Baada ya hapo tulielekea magharibi ya jimbo anakotoka Mheshimiwa Wasira. Baada ya kura kupigwa katika Kata ya Guta, Mheshimiwa Wasira alijitoa kwa sababu aliona hawezi kunishinda hata kama angepata kura zote za kata mbili zilizobaki. Siyo kweli kwamba Nyamuswa ilikuwa ya mwisho kupiga kura na siyo kweli wananchi wa kata nzima walipiga kura. Kumbukumbu zote zinaweza kupatikana wilayani na makao makuu ya CCM.
Mheshimiwa Wasira anasema kwamba nilikuwa Jaji na kesi iliyopelekwa mahakamani ni kama kesi ya tumbili kupelekwa kwa nyani, kwa maana kwamba majaji walinipendelea. Kumbukumbu za kesi hiyo zipo. Wakati huo sikuwa jaji. Isitoshe huko nyuma uchaguzi nilioshinda 1992 ulitenguliwa. Kwa nini wakati huo sikupendelewa? Kumbukumbu za kesi zinaeleza kwa nini Mheshimiwa Wasira alifungiwa kugombea kwa kipindi.
Mheshimiwa Wasira ni kiongozi wa Taifa kwa kipindi kirefu. Ni mbunge wangu na namtambua hivyo. Tunaweza kuwa na mtazamo tofauti katika baadhi ya mambo lakini hiyo si sababu ya kusema mambo yasiyo ya kweli kwa nia ya kujijenga kisiasa.
Yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM. Yeye ni Waziri mwandamizi. Yeye anafikiria kugombea urais. Ni vizuri basi akajifunza kusema kweli (ambayo ni ahadi mojawapo ya WanaCCM). Akumbuke anayosema yanaweza kumrudia mbele ya safari.
J.S. Warioba
No comments:
Post a Comment