Dk. Antony Dialo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza
Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani hapa, kimekemea siasa za kuchafuana zinazofanywa na Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Mwanza, Dk. Antony Dialo dhidi ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Kimesema mwenyekiti huyo akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari, alisema Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, hakufanya kazi ya kuleta maji ya Ziwa Victoria na kuyasambaza mkoani Shinyanga. Akizungumza juzi na waandishi wa habari, Katibu wa siasa na uenezi mkoani Shinyanga, Emmanuel Mlimandago, alisema kauli ya Dialo ni ya ulimbukeni wa kisiasa na kujitafutia umaarufu kupitia mgongo wa Lowassa.
Alisema amekuwa akisoma taarifa mbalimbali kupitia kwenye vyombo vya habari, akimtuhumu na kumtolea kashfa waziri mkuu huyo mstaafu.
“Mimi kama katibu mwenezi wa CCM, mkoani Shinyanga nilishuhudia mradi huo wa maji kutoka ziwa Victoria na kuletwa mjini Shinyanga enzi za waziri mkuu huyo mstaafu na kipindi hicho Dialo alikuwa naibu waziri wa maji,” alisema.
Alisema kwa kawaida kazi anazozifanya naibu waziri ni maagizo kutoka kwa waziri mwenye dhamana, hivyo Dialo alikuwa mtu wa kuagizwa na Lowassa kutekeleza majukumu hayo.
“Kwa niaba ya CCM mkoani Shinyanga, tunakemea kitendo alicho kifanya Dialo cha kumchafua Edward Lowasa na tunamuonya tabia hiyo isijirudie na aache upotoshaji huko ni kujitafutia umaarufu na heshima asizo stahili kupitia mgongo wa Lowassa” alisema.
Aliongeza kwa maneno aliyoyasema Dialo, na majigambo ni dhahiri kuwa ameonyesha udhaifu wa hali ya juu na amewadhalilisha wasomi wenye elimu kama yake ya PhD, na kuonyesha elimu yake ni ya mashaka kwa kutokujua kuchambua mambo yeye kama msomi. Mlimandago, alisema kuwa inawezekana Dialo anatumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa kumchafua Lowassa kutokana na kutangaza nia ya kugombea urais mwakani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment