Jeshi la Nigeria limekanusha taarifa ya awali kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule waliotekwa nyara kutoka Chibok na wapiganaji wa Boko Haram, wameachiliwa.
Msemaji wa jeshi nchini Nigeria, Meja Generali Chris Olukolade, ameambia BBC kuwa wanawahifadhi wasichana kadhaa lakini akakana kuwa wasichana hao ni baadhi ya wale waliotekwa nyara na wapiganaji wa Boko Haram kutoka Chibok.
Zaidi ya wasichana 200 walitekwa nyara na Boko Haram kutoka shule ya mabweni Kaskazini Mashariki mwa jimbo la Borno.
Utekaji nyara huo ulisababisha ghadhabu kote nchini Nigeria na duniani kote kiasi cha kusababisha kampeini ya kutaka kuokolewa kwa wasichana hao kwenye mitandao ya kijamii.
Maandamano yenye kauli mbiu, (#BringBackOurGirls) yaliandaliwa kutoa wito kwa watawala kuongeza juhudi za kuwanusuru wasichana hao,
Muda mfupi baada ya kuwateka nyara,Boko Haram, ilitoa kanda ya video wakisema kuwa wasichana hao wataachiliwa tu ikiwa serikali itakubali kuwaachilia wapiganaji wa kundi hilo ambao wanazuiliwa.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ripoti ambazo hazijathibitishwa zikisema kuwa serikali ya Nigeria imekuwa ikifanya mazungumzo na Boko Haram, kubadilishana wasichana hao na wapiganaji wao wanaozuiliwa.
Tangu kutolew kwa amri ya kutotoka nje nyakati za jioni, katika eneo la Kaskazini Mashariki kwa lengo la kutatiza harakati za Boko Haram, kundi hilo limekuwa likiendeleza mashambulizi.
Wanawake wengi na watoto, wakiwemo wasichana wamekuwa wakitekwa nyara.
Awali, Generali Olukolade aliambia BBC kuwa shughuli inaendelea ya kuwaokoa wasichana hao na kwamba baadhi ya wasichana haio wako salama katika kambi za jeshi.
Hata hivyo msemaji huyo baadaye alisema kuwa jeshi linajaribu kuwatambua wasichana hao ambao wako chini ya ulinzi wa jeshi lakini hawakurejea kutoka Chibok.
CREDIT: BBC/SWAHILI
No comments:
Post a Comment