Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 29 September 2014

MBIVU NA MBICHI ZA BUNGE LA KATIBA KUANZA KUJULIKANA LEO

Na Daniel Mjema, Mmwananchi
Dodoma. Wiki ya kufa au kupona kwa Bunge la Katiba, inaanza leo mjini Dodoma wakati wajumbe watakapoanza kuzipigia kura ibara na sura za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Shughuli hiyo itaanza huku kukiwa na hofu ya kutopatikana kwa theluthi mbili ya kura kwa wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar inayotakiwa kwa mujibu wa kanuni, sheria na Katiba ya nchi.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, upigaji kura utafanyika kwa siku nne kuanzia leo hadi Oktoba 2, mwaka huu na iwapo itapitishwa, atakabidhiwa Rais kusubiri kupigiwa kura ya maoni mwaka 2016.
Habari kutoka bungeni zinadai kuwa wasiwasi wa kutopatikana kwa theluthi mbili uko zaidi upande wa Zanzibar hasa baada ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia Bunge hilo.
Hofu nyingine inatokana na suala la Mahakama ya Kadhi kutoingizwa, jambo ambalo limewagawa wajumbe huku kundi moja likiapa kupiga kura ya hapana iwapo haitaingizwa.
Baadhi ya wajumbe wanataka Ibara ya 40 iingize vifungu vinavyotamka kuwapo kwa mahakama hiyo ili uamuzi wake kuhusu masuala ya ndoa, mirathi na talaka utambuliwe na sheria za nchi.
Hata hivyo, wajumbe wengine wanapinga suala hilo wakitaka ibara hiyo ibaki kama ilivyo ili Serikali isijihusishe na masuala ya uendeshaji wa jumuiya za dini.
Vilevile, Kifungu cha 22 (d) cha Rasimu kinachompa mwanamke haki sawa na mwanamume kumiliki ardhi kinapingwa vikali na baadhi ya wajumbe.
Pia baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wanaona kuwa pamoja na kwamba karibu asilimia 90 ya mambo waliyokuwa wakiyalilia yameingizwa kwenye Katiba, bado Zanzibar haijapewa mamlaka kamili.
Hali hiyo imeifanya Kamati ya Uongozi chini ya Sitta kufanya vikao vya mashauriano mfululizo baina yao na wajumbe wa Kamati ya Uandishi ili kujaribu kuokoa jahazi.
Jana, vikao vya kamati 12 za Bunge ambavyo vilikuwa vianze saa 8:00 mchana vililazimika kusogezwa mbele kusubiri maelekezo kutoka Kamati ya Uongozi ambayo ilikuwa inakutana saa 9:00 alasiri.
Kanuni mpya
Upigaji kura huo unafanyika chini ya kanuni mpya baada ya zile za awali kufanyiwa marekebisho ili pamoja na mambo mengine, kuruhusu wajumbe walioko nje kupiga kura kwa njia ya faksi na mtandao.
Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alipotafutwa jana kufafanua maandalizi ya utekelezaji wa kanuni hiyo inayokosolewa na makundi mbalimbali ya jamii, alisema kila kitu kitafahamika leo.
“Sasa hivi ndiyo niko kwenye kikao na wenzangu subirini kesho (leo) ratiba yote mtapewa,” alisema Katibu bila kutaka kuendelea zaidi kujibu hoja za mwandishi wetu.
Septemba 22, mwaka huu, wajumbe wa Bunge hilo walipitisha azimio la kuzifanyia marekebisho kanuni za 30,36 na 38 za Bunge ili kurahisisha upigaji huo wa kura.
Chini ya marekebisho hayo, wajumbe watakaokuwa nje ya Bunge kwa ruhusa ya maandishi ya mwenyekiti, wataruhusiwa kupiga kura kwa njia ya faksi au mtandao.
Miongoni mwa kanuni zilizofanyiwa marekebisho ni 30 (1) ambayo sasa inasomeka kuwa akidi kwa kila kikao cha Bunge la Katiba itakuwa ni nusu ya wajumbe hata kama ni kikao kwa ajili ya uamuzi, ikimaanisha kwamba si lazima leo wawepo wajumbe wote, bali nusu tu, ili upigaji kura uweze kufanyika.
Kanuni hiyo ndiyo iliongezwa fasili mpya ya 2A kuruhusu wajumbe waliopo nje ya Bunge kwa ruhusa ya mwenyekiti, wajumuishwe kwenye idadi ya wajumbe waliohudhuria kikao siku hiyo.
Kanuni nyingine iliyorekebishwa ni ya 36 kwa kuongeza fasili mpya ya 1A ili kuruhusu mjumbe kuzipigia kura ibara zote za sura moja au zaidi ya sura moja za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa badala ya kupigia sura mojamoja kama ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo mpya, endapo mjumbe atapiga kura ya wazi basi atatamka ibara anazozikubali na asizozikubali na anayepiga kura ya siri kuonyesha anazozikubali na anazozikataa.
Ili kukidhi kile kilichoelezwa na Katibu wa Bunge kwamba Bunge Maalumu litatuma Ofisa wake Saudi Arabia kusimamia upigaji kura kwa mahujaji, kanuni ya 38 ilirekebishwa.
Kanuni hiyo imeongezwa fasili mpya ya 1A na 1B ili kumpa mamlaka Katibu wa Bunge kuwa msimamizi mkuu wa upigaji wa kura na anaweza kumteua mtu yeyote kusimamia upigaji kura kwa niaba yake.
Baada ya kura zote za siri kupigwa, kura hizo zitakusanywa na kupelekwa kwenye chumba maalumu kuhesabiwa mbele ya mawakala walioteuliwa kwa ajili ya kusimamia kura hizo.
Mjumbe anayetaka kupiga kura ya wazi, ataitwa jina na Katibu au mtu aliyeidhinishwa na katibu na atatamka kwa sauti maneno “Ndiyo” au “Hapana” kuhusu Ibara husika au rasimu ya mwisho.
Mjumbe anayepiga kura ya siri au ya wazi nje ya maeneo ya Bunge, ataelekezwa kwa maandishi na katibu baada ya kushauriana na mwenyekiti kuhusu utaratibu.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment