KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wajumbe wa halamshauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Meru wamekataa kupokea taarifa ya sekta ya barabara huku wakimkataa mhandisi wa ujenzi na barabara ambaye ni Mhandisi Peter Mikimba hadi hapo serikali itakopoleta mhandisi mwingine wa sekta hiyo.
Wajumbe hao wameweza kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa sekta zote isipokuwa sekta hiyo kutokana kile walichodai kuwa mhandisi huyo amekuwa akikwamisha miradi ya barabara na hivyo kufanya baadhi ya shughuli kusimama kwa muda kutokana na kuwepo kwa ubovu wa barabara.
Akizungumza katika kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, Katibu wa CCM Wilaya ya Meru, Langaeli Akyoo, alisema kuwa kamwe hawataweza kupokea taarifa ya sekta hiyo kwa kuwa ina mapungufu makubwa sana ambayo yanahitaji ufafanuzi wa kina.
Alisema kuwa hali ya barabara ni mbaya sana kwa miaka mitatu mfululizo na tatizo likiwa lipo kwa mtaalamu wa sekta hiyo kushindwa kuisaidia halmashauri hiyo suala hilo.
“Sisi tunasema hii taarifa hatuikubali kabisa na hatumuhitaji tena mhandisi wa sekta hii hadi hapo tutakapoletewa mwingine na serikali huyu amekuwa akitucheleweshea sana maendeleo yetu ya ukarabati wa hizi barabara zetu,” alisema Akyoo.
Alifafanua kuwa bado wataendelea kuwa na msimamo wa kumkataa mhandisi huyo kwa kuwa haiwezekani ashindwe kutoa majibu sahihi mbele ya Halamshauri Kuu ya chama hicho yanayomfanya kushindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati husika angali fedha za kuendesha zilishatengwa na halmashauri.
Naye Elipokea Masaua ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM alisema kuwa wao hawamtaki mhandisi huyo kwa kuwa amekuwa na kauli ambazo hazifai na amekuwa akikwamisha shughuli za maendeleo na hivyo wanamtaka aondoke mapema na asipoondoka watamfungia nje ndani ya siku saba.
Hata hivyo wajumbe hao waliweza kuwa na msimamo wa pamoja wa kumkataa mhandisi huyo hadi hapo serikali itakapoleta mtaalamu mwingine na endapo zitapita siku saba bila kuondoka watalazimika kuchukua hatua nyinginezo.
Nae mhandisi Peter Mikimba akiongea katika kikao hicho alisema kuwa yeye yupo tayari kuhama na kwenda kukaa kwenye dawati la Tamisemi huku akiwa anazisaidia shughuli za Meru.
“Nimeshaenda tamisemi kufanya mipango ya kuhama halamshauri hii na nitaenda kufanya kazi nikiwa kule kule kwa kuwa ninachoamini mimi sina shutuma zozote dhidi yah ii miradi ya ujenzi wa barabra,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment