Dodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu, Said Arfi amelitikisa Bunge jana baada ya kuwasilisha hoja sawa na zile zinazosimamiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), alilitikisa Bunge hilo, alipowasilisha maoni ya wajumbe wachache wa Kamati Namba 10 inayoongozwa na Anna Abdallah.
Alisema wajumbe wengi wamependekeza marekebisho ya sura ya saba kwa kuweka Makamu wa Rais watatu yaani mgombea mwenza, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema wachache wamependekeza sura hiyo kubaki kama ilivyopendekezwa kwenye Rasimu kwa sababu muundo wa serikali tatu uliopendekezwa hauhitaji kuwa na makamu wa rais watatu wala ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Rasimu hiyo, Ibara ya 70 inasema kutakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano itayokuwa na Rais, makamu na mawaziri wa Jamhuri ya Muungano.
Tofauti na walio wengi ambao wamependekeza mawaziri na naibu mawaziri watokane na Bunge, wachache katika kamati hiyo wametaka ibaki kama ilivyo katika Rasimu ya kuwa mawaziri wasitokane na wabunge.
Alisema mapendekezo hayo yataleta ufanisi zaidi katika utendaji wa mawaziri katika wizara husika.
“Sababu nyingine ni kuondoa uwezekano wa waziri ambaye ni mbunge kupendelea jimbo lake la uchaguzi ili aweze kuchaguliwa tena katika chaguzi zinazofuata,” alisema.
Pia alisema wajumbe wengi wameondoa dhana ya Serikali ya Tanganyika na kufuta mapendekezo yanayoweka utaratibu wa viongozi wa serikali hiyo kushiriki katika chombo cha uhusiano na uratibu wa Serikali kinachoanzishwa na Rasimu.
Hata hivyo, alisema wajumbe wachache wamependekeza ibara hizo zibaki kama zilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba kwa sababu maudhui yaliyowekwa yanakidhi muktadha na majukumu ya chombo husika katika muundo wa serikali tatu.
Arfi alisema wajumbe wengi walipendekeza kuingizwa kwa sura na sehemu mpya zilizopendekezwa kuhusu mamlaka ya umma, ardhi, maliasili na mazingira na sehemu ya Taasisi ya Kuzuia Rushwa katika sura ya 13.
Alifafanua kuwa wajumbe wengi pia walipendekeza sura ya ardhi, maliasili na mazingira.
“Wajumbe wachache hawazikubali sura na ibara mpya zote zilizopendekezwa kwani zinalenga katika kuongeza mambo ya muungano katika Rasimu ya Katiba,” alisema.
Katika kamati hiyo, wajumbe wengi wamependekeza kuwapo na uraia wa nchi zaidi ya moja kwa sababu Watanzania walioko nje ya nchi wangependa kurudi na kuwekeza nyumbani kwao.
Hata hivyo, alisema wajumbe wachache wamependekeza sura hiyo ibaki kama ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba kwa sababu kuna hatari nyingi zinazoambatana na uraia pacha ikiwa ni pamoja na kuhatarisha usalama wa nchi.
No comments:
Post a Comment