Masalia ya ndege ya Kampuni ya Safari Express Limited iliyoanguka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuua watu watatu jana. Na Mpigapicha Wetu.
Dar/Moro. Ndege ya Kampuni ya Safari Express Limited imeanguka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuwateketeza watu watatu waliokuwamo ndani.
Ndege hiyo yenye namba za usajili 5Y-SXP iliruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza Jumapili saa 1:26 usiku ikielekea Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Kenya ambako ilitakiwa kutua saa 2:36 usiku.
Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete alikiri ndege hiyo kuanguka kwenye hifadhi hiyo na walikuwa katika harakati za kuitafuta.
Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini, kutoka Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, David Nyamwihura alisema ajali hiyo ilitokea takriban maili 20 kutoka Serengeti, katika eneo la Kogatembe na watu wote watatu waliokuwamo wamefariki dunia.
Meneja wa Udhibiti wa JKIA, Clever Davor aliliambia gazeti la Daily Nation la Kenya kuwa ndege hiyo ilipoteza mawasiliano na rada ya uwanja huo ikiwa imeruka angani urefu wa futi 14,000.
Awali, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KCAA) ilitoa taarifa juu ya kuchelewa kwa ndege hiyo iliyokuwa ikitarajiwa kutua katika uwanja wa JKIA saa 2 usiku.
Jana asubuhi, Kamanda wa Viwanja vya Ndege wa Kenya (KAPU), Joseph Ole Tito alithibitisha kupotea kwa ndege hiyo kabla ya kuonekana baadaye katika Hifadhi ya Serengeti.
Polisi wa Kenya hawakueleza ndege hiyo ya mizigo aina ya Fokker F-27-500 ilikuja nchini kwa shughuli gani.
Ndege zote zinazotoka Kenya kwenda nchi za jirani, huanzia safari zake katika viwanja vya JKIA, Wilson au Wajir ili kuwa na usimamizi wa karibu.
Watano wafa ajalini Moro
Katika hatua nyingine, watu watano wamefariki dunia papo hapo na mmoja kujeruhiwa baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kwenda kwenye sherehe kugongana uso kwa uso na lori.
Ajali hiyo ilitokea Jumamosi iliyopita saa 2:30 usiku eneo la Hoteli ya Tabu, Wilaya ya Gairo na kuhusisha gari dogo aina ya Toyota Corola lililokuwa likiendeshwa na Joashi Mrisho (25) na lori lililokuwa likienda Burundi.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paulo alisema gari hilo dogo lilikuwa limebeba watu sita waliokuwa wakienda kwenye sherehe.
Paulo aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Mrisho (dereva wa gari dogo), Matonya Mganule (25), Bule Siprian (30), Neli Aidani (22) na Sisemi Lesamila (23) wote wakati wa Gairo.
Alimtaja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Mang’utu Chitojo (32) ambaye amelazwa katika Hospitali ya Berega na anaendelea vizuri. Dereva wa lori alikimbia mara baada ya ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment