Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 3 September 2014

RPC KOVA AUNDA TUME KUCHUNGUZA KIFO CHA MTUHUMIWA ANAYEDAIWA KUUAWA NA POLISI



Dar es Salaam. Wakati kukiwa hakuna taarifa za majopo ya uchunguzi yaliyowahi kuundwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu wa Dar es Salaam, Suleiman Kova katika matukio mbalimbali, jana aliunda jopo jipya kuchunguza kifo cha mtuhumiwa kinachohusishwa na kipigo cha polisi.
Jana, Kamanda Kova alitangaza jopo hilo la wapelelezi kuchunguza kifo cha Liberatus Matemu (55) aliyefia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akidaiwa kupigwa na polisi katika Kituo cha Stakishari na maiti yake kukataliwa na nduguze.
Kabla ya kufariki Jumapili iliyopita, Matemu alikuwa chini ya ulinzi katika kituo hicho kilichopo wilayani Ilala ambako alikaa kwa siku nane.
Jopo hilo linaundwa huku kukiwa hakuna taarifa zozote za uchunguzi zilizotolewa na kamanda huyo kuhusu matukio yaliyotangulia.
Majopo mengine
Julai 23, mwaka huu, Kova aliunda timu ya wataalamu saba kuchunguza kashfa ya viungo vya binadamu vilivyookotwa Mbweni Mpiji, wilayani Kinondoni ambavyo vilidaiwa vilikuwa vikitumiwa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Afya (Imtu) lakini hadi sasa wananchi hawajajulishwa kuhusu majibu ya uchunguzi huo.
Mei 21, mwaka huu, Kova aliunda jopo la wapelelezi liliongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jaffari Mohamed kuchunguza kifo cha aliyekuwa Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza aliyedaiwa kujinyonga na hadi leo taarifa za uchunguzi huo hazijatangazwa.
Januari 7, mwaka huu, Kamanda Kova aliunda jopo la wapelelezi wanane walioongozwa na Mohamed kuchunguza tukio la kutekwa Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Temeke, Joseph Yona na matokeo yake hayajawekwa wazi.
Uchunguzi mpya
Akizungumza jana, Kova alisema jopo la kuchunguza kifo tata cha Matemu litaongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Costantine Masawe.
Alisema taarifa za awali zinaonyesha kwamba marehemu alikuwa na ugomvi mkubwa kati yake na mtu mwingine ambaye wamekuwa wakishambuliana kila wanapokutana.
Kamanda Kova alisema ameona ni bora uchunguzi huo ufanyike ili kuondoa utata na kupata taarifa kamili kuhusu ugomvi uliosababisha kushambuliana mara kwa mara.
Kova alisema uchunguzi huo unafanywa ili kuangalia Matemu alivyokamatwa, alivyokaa mahabusu, alivyopelekwa katika Hospitali ya Amana na baadaye katika Hospitali ya Muhimbili.
“Uchunguzi huu utahusisha madaktari bingwa wanaohusika na uchunguzi wa miili ya watu waliokufa katika mazingira yenye utata,” alisema.
Alisema jopo hilo pia litamhusisha mwanasheria wa familia ya Matemu na mwanasheria mwingine kutoka serikalini ili kuhakikisha kunakuwa na ukweli na uwazi.
Uchunguzi wa mwili leo
Mwanasheria wa familia ya marehemu Matemu, Benedict Baligiye alisema mwili wa marehemu utafanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Muhimbili leo.
“Tukipata taarifa ya uchunguzi ndipo ndugu wataanza kufanya maandalizi ya mazishi,” alisema.

CREDIT: MWANANCHI: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Kova-aongeza-idadi-ya--tume--D-Salaam/-/1597296/2439458/-/12neje7/-/index.html

No comments:

Post a Comment