KUNRADHI KWA PICHA HIZI. MATUKIO HAYA YANAZUILIKA, KWANINI WATAWALA WANAPENDA KUMWAGA DAMU?
Tazama unyama wa Polisi!
Na Daniel
Mbega
KICHWA
cha habari kilichonivutia ni ‘Kova aongeza idadi ya ‘tume’ D’Salaam’
ambacho kipo kwenye gazeti la Mwananchi toleo la Jumatano, Septemba 3,
2014.
Habari hii imefuatia hatua
iliyofanywa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova, baada ya kutangaza jopo la wapelelezi kuchunguza kifo cha mtuhumiwa Liberatus
Matemu (55) aliyefia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akidaiwa kupigwa na
polisi katika Kituo cha Stakishari na maiti yake kukataliwa na nduguze. Kabla
ya kufariki Jumapili iliyopita, Matemu alikuwa chini ya ulinzi katika kituo
hicho kilichopo wilayani Ilala ambako alikaa kwa siku nane. Jopo hilo la
wapelelezi litaongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Costantine Masawe.
Tumeshazowea
kusikia ‘tume’ zikiundwa kila yanapotokea matukio mbalimbali, mengi yakiwa
yamefanywa ama kuwahusisha hao hao wanaounda tume hizo. Mifano iko mingi, na
inadhihirishwa na vichwa vya habari kama vile… “Jeshi la Polisi launda Tume kuchunguza
mauaji ya Mwangosi!”, “Tume ya kuchunguza majuaji Morogoro yaundwa!”, “Walioua
raia Songea wachunguzwa!”, “Polisi wachunguza mauaji Nyamongo!”, “Msako waanza
utekwaji wa Kibanda!” “Aliyemteka Dk. Ulimboka hajulikani!” “Mabomu ya Arusha
yaacha maswali”.
Naam, vichwa vya habari vya aina
hii vimekuwa vikijitokeza kila wakati kwenye vyombo vya habari nchini kila mara
yanapotokea mauaji katika vurugu mbalimbali, na mauaji haya mara nyingi
yamekuwa yakisababishwa ama kufanywa na askari wa jeshi hilo hilo la polisi.
Lakini ukitazama jopo
lililoundwa na Kamanda Kova, binafsi nasema ni usanii mwingine unaoendelea kwa
sababu mpaka sasa hakuna taarifa zozote za uchunguzi zilizotolewa na kamanda
huyo kuhusu matukio kadhaa yaliyotangulia, ambayo alidai yanachunguzwa baada ya
kuyaundia ‘tume’.
Itakumbukwa kwamba, Julai
23, 2014, Kova huyo huyo aliunda timu ya wataalamu saba kuchunguza kashfa ya
viungo vya binadamu vilivyookotwa Mbweni Mpiji, wilayani Kinondoni ambavyo
vilidaiwa vilikuwa vikitumiwa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Afya
(Imtu) lakini hadi sasa wananchi hawajajulishwa kuhusu majibu ya uchunguzi huo.
Aidha, Mei 21, 2014, Kova
aliunda tena jopo la wapelelezi liliongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Jaffari Mohamed kuchunguza kifo cha aliyekuwa Meneja
Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius
Gashaza aliyedaiwa kujinyonga na hadi leo taarifa za uchunguzi huo
hazijatangazwa.
Mnamo Januari 7, 2014,
Kamanda Kova aliunda jopo la wapelelezi nane walioongozwa tena na RCO Jaffari Mohamed
kuchunguza tukio la kutekwa Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Temeke, Joseph
Yona na matokeo yake hayajawekwa wazi.
Wanahabari nchini Tanzania jana
walikuwa wanakumbuka miaka miwili ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa na askari
wa jeshi la polisi dhidi ya mwandishi wa kituo cha Chennel Ten, marehemu Daudi
Mwangosi, wakati polisi hao ‘wakipambana’ na wafuasi wa Chadema waliokuwa
katika ufunguzi wa tawi la chama hicho katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.
Lakini kutekwa na kuteswa kwa
Mhariri Mtendaji wa New Habari, Absalom Kibanda pamoja na kutekwa na kuteswa
kwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, bado kumeacha
makovu mengi yasiyofutika.
Wakati katika matukio yote ya mauaji polisi ndio
wanaohusika, bado jeshi hilo hilo linaibuka na kuunda tume ya kuwachunguza polisi
wenzao walioua, hatua ambayo kwa ujumla inaleta mkanganyiko na ndiyo maana
ninasema ni ‘Tume za Manyani kuchunguza nani kala mahindi’!
Hivi inakuwaje nyani amchunguze nyani aliyekula mahindi
wakati huyo huyo anayemchunguza mwenzake kesho naye atakwenda shambani kula
mahindi ambayo hakuyalima? Uchunguzi huo unaweza kuwa na haki kweli?
Tumeshuhudia matukio mengi ya mauaji yanayofanywa na jeshi
hilo kwa kisingizio cha kutuliza vurugu na maandamano, hasa kwenye mikusanyiko
ya kisiasa.
Agosti 27, 2012 polisi wanadaiwa kuua mtu mmoja mjini
Morogoro na kujeruhi wengine watatu. Haraka haraka wakaunda tume, siku mbili
baadaye tukasikia ripoti yao kwamba ‘eti’ marehemu Ally Nzona (38) aliuawa
baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Siku sita baada ya mauaji hayo, polisi tena wakamuua Daudi
Mwangosi, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC),
safari hii siyo kwa ‘kitu chenye ncha kali’ wala risasi ya moto, bali bomu!
Wenyewe wakasema ameuawa kwa ‘KITU
KIZITO’.
Wakati ulimwengu ukipiga kelele huku tayari jeshi hilo
likikimbilia ‘kuunda tume’, zikaanza tetesi kwamba eti bomu lililomuua marehemu
lilirushwa na wafuasi wa Chadema, tetesi nyingine ambazo katu haziingii
akilini, zikasema eti marehemu alikuwa na bomu kwenye jaketi lake! Amelitoa
wapi? Na awe na bomu ili alifanyie nini? Au kamera yake ndiyo iliyogeuka bomu?
Kesi hii iko mahakamani, lakini watuhumiwa wakuu - IGP mstaafu Said Mwema,
aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, Jasusi wa Mkoa
wa Iringa (RCO) na Mkurugenzi wa Operesheni Maalum, Paul Chagonja pamoja na
Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo Dk. Emmanuel Nchimbi, waliokuwa
wanastahili kujiuzulu na kushtakiwa kwa mauaji hayo, wako uraiani.
Tunaendelea
kushuhudia mauaji mengi ya Watanzania wasio na hatia huku jeshi la polisi
likifanya uzembe kwa kutumia silaha za moto kwa wananchi walio mikono mitupu,
ambao wangeweza kutulizwa kwa kutumia tu mabomu ya machozi.
Lakini
kutokana na askari wa jeshi hilo kuwa na uchu mkubwa wa kumwaga damu, wanaona
mabomu ya machozi hayafai, na sasa wamebadili mbinu za matumizi yake, kwamba
watayatumia lakini kwa kuwafyatulia wananchi moja kwa moja ili yawaue! Ni
unyama wa aina gani huu? Yaani usalama wa raia umegeuka kuwa uhasama wa raia?
Mwangosi aliuawa
akiwa mikononi mwa polisi waliokuwa wamemdhibiti kwa kumpa kipigo, lakini
pamoja na kelele zake, pamoja na kuonekana na zana zake za kazi, bado polisi
waliona kama kiumbe asiyestahili kuishi duniani na njia pekee ni kumfumua kwa
bomu! Jamani, hata mbuzi tunamla nyama, lakini kamwe hatujawahi kufikiria
kumcharanga mapanga ndipo tumbanike!
Huu ni
mfululizo tu wa matukio mengi yanayokwenda kinyume na haki za binadamu na
utawala bora, ambao Jeshi la Polisi limekuwa likiyafanya, tena kwa mfululizo,
huku viongozi waandamizi wa jeshi hilo, na wahusika wenyewe wakishindwa
kuwajibika.
1. Mauaji ya Mwangosi
Kama
nilivyotangulia kusema hapo awali, Mwangosi aliuawa akiwa mikononi mwa polisi Septemba 2, 2012, tena akiwa hana
silaha zaidi ya kamera yake, ambayo ndiyo zana yake ya kazi, huku RPC Kamuhanda
akiangalia! Sijui kama alikuwa amethiriwa na damu, kwani Februari 21, 2012 akiwa RPC wa Ruvuma tulishuhudia vijana wake
wakiwamiminia risasi wananchi wanne wasio na silaha, waliokuwa wakiandamana kwa
amani mjini Songea. Ni Kamuhanda huyo huyo ambaye katika tukio la Songea
alitamka bayana kwamba vijana wake walikuwa na haki ya kuwafyatulia risasi za
moto waandamanaji hao kabla ya bosi wake IGP Said Mwema (sasa amestaafu) kuibuka
na kuomba radhi kwa tukio hilo.
2. Mauaji ya raia Morogoro
Polisi wakamkamata kiongozi wa Chadema, Benson Kigaila.
Agosti 27, 2012 Polisi mkoani Morogoro
wanadaiwa kumuua Ally Nzona, mtu anayedaiwa kuwa mpiga debe katika setendi ya
mabasi ya Msamvu, kwa madai kwamba walikuwa wanatawanya maandamano ya Chadema.
Ripoti ya
haraka ya polisi ikasema eti aliuawa kwa kitu chenye ncha kali, siyo risasi.
Hawakusema nani aliyemchoma. Hili bado lina utata.
3. Mauaji ya Raia Songea
Februari 21, 2012 Mauaji ya wananchi
wanne yaliyofanyika mjini Songea pamoja na wengine 41 kujeruhiwa ni sehemu tu
ya uozo mkubwa na utumiaji wa mabavu unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini. Pamoja
na Said Mwema kuomba radhi na kuunda Tume, lakini hawezi kuiosha mikono yake na
damu isiyo na hatia ya Watanzania waliokuwa wanapeleka kilio chao kuhusu
wapendwa wao waliouawa na ‘watu wasiojulikana’ tangu Novemba 2011. Tunasikia
kwamba watuhumiwa wanne walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo ya kishirikiana
ambao ni Johari Kassim (16), Onesmo Hinju (14), Samason Haule (22) na Mussa
Fuala (20) wote wakazi wa Mtaa wa Lizaboni mjini Songea.
Polisi,
kwa makusudi kabisa, waliamua kufyatua risasi za moto kwenye umati wa
waandamanaji ambao siyo tu hawakuwa na silaha zozote, lakini pia walikuwa
wameibeba na maiti iliyouawa kikatili na ‘watu wasiojulikana’ katika matukio ya
imani za kishirikina.
Jambo baya
zaidi, na kwa mujibu wa taarifa za wananchi wa Songea, ni kwamba, mara kadhaa
walikuwa wameripoti matukio ya watu kuuawa kinyama na kunyofolewa sehemu zao za
siri, lakini polisi hao wakapuuza.
4. Wapiga Nondo Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evance Balama akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa askari Polisi PC Meshack Urasa ambaye aliuawa kwa kupigwa na nondo juzi Jijini Mbeya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi akitoa heshma za mwisho kwa mwili wa askari Polisi PC Meshack Urasa ambaye aliuawa kwa kupigwa na nondo juzi Jijini Mbeya.
skari Polisi wakitoa wakitoa heshma za mwisho kwa mwili wa askari mwenzao, PC Meshack Urasa ambaye aliuawa kwa kupigwa na nondo juzi Jijini Mbeya. (Picha kwa hisani ya kamanganamatukio.blogspot.com)
Jeneza lenye mwili wa PC Meshack Urassa, ambaye alizikwa Machame mkoani Kilimanjaro.
Tangu
katikati ya mwaka 2011, kuliibuka mauaji ya ajabu mkoani Mbeya maarufu kama
‘kupiga nondo’ yaliyokuwa yakifanywa na watu mbalimbali kwa imani za
kishirikina. Wananchi wengi walijeruhiwa na wengine kupoteza maisha yao katika
matukio hayo.
Pamoja na
wananchi kujitahidi kupiga kelele, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya halikuchukua
hatua zozote za makusudi kukabiliana na hali hiyo hadi Septemba 27, wakati
askari wao, PC Meshack Urassa (28) mwenye namba G.2795 alipouawa na wapiga
nondo hao katika eneo la Mabatini majira ya saa 5.15 usiku.
Hii ilidhihirisha wazi kushindwa kwa Jeshi la Polisi kulinda
amani ya wananchi wake na waliirejesha Mbeya enzi za uchunaji ngozi katika
miaka ya 1998 – 2000.
5. Mauaji Arusha
Kijana huyu alijeruhiwa kwa risasi na polisi jijini Arusha katika maandamano ya ChademaMwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema wakiwa wamebeba jeneza la mmoja wa vijana waliouawa na polisi Januari 5, 2011
Mke wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbusi akiwa amejeruhiwa katika vurugu jijini Arusha
Hakuna
asiyekumbuka mauaji ya raia wasio na hatia yaliyotokea Januari 5, 2011 jijini
Arusha wakati wa maandamano ya Chadema. Jeshi la Polisi, kwa makusudi kabisa
kama wanapopoa mbwa koko, waliamua kufyatua risasi za moto kwenye umati wa
waandamanaji.
Siku hiyo Jeshi la Polisi lilitumia silaha kubwa – risasi za moto,
mabomu ya machozi na magari ya maji ya kuwasha – dhidi ya raia waliokuwa na
vitambaa vyeupe vyenye kuashiria amani. Watu wawili wakapoteza maisha yao siku
hiyo na kuwakumbusha Watanzania matukio ya tarehe 26 na 27 Januari 2001 kule
Zanzibar wakati Jeshi la Polisi lilipomwaga damu ya wananchi wasio na hatia
waliotaka kulinda wizi wa kura na unyongaji wa demokrasia unaofanywa na
watawala wa Chama cha Mapinduzi.
Pamoja na kuwaua raia hao, katika tukio ambalo pia askari
mmoja aliuawa, bado viongozi wa juu wa Chadema walikamatwa na kushtakiwa kwa
madai kwamba waliandamana kinyume cha sheria.
6. Mauaji Tarime
Polisi
waliendelea kuwa vibaraka wa watawala na wenye fedha wakati jeshi hilo
lilipowaua watu watano kwa risasi Mei 15, 2011 na kuwajeruhi wengine kadhaa
kati ya watu 800 waliovamia mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo kwa
lengo la kuchukua mchanga wa dhahabu.
Polisi
wanaolinda mgodi huo, ambao walisema walikuwa wanajihami, walikabiliana na watu
hao waliokuwa na silaha za jadi majira ya saa 11.00 alfajiri katika eneo la
Kinu cha Dhahabu. Kwa hiyo, watu watano - Chacha Ngoko (25), Emmanuel Magige
Ghati (19), Chacha Mwasi (23), na wengine wawili wakapoteza maisha.
Lakini
ukifuatilia kwa makini tukio hilo, utagundua kuwa taarifa zilizotolewa na
serikali na polisi zinaonyesha kwamba kulikuwa na jambo lililofichika. Maelezo
ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo Balozi Hamisi Kagasheki na RPC
Massawe wa Tarime yalitofautiana kwa mbali na yale ya Kamishna wa Oparesheni na
Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja.
Chagonja
alipinga taarifa zilizotolewa na RPC Massawe kuwa waliouawa walikuwa majambazi,
akisema hizo zilikuwa taarifa za mtu wa chini yake na wananchi wamwamini yeye kuwa
waliouawa walikuwa ni wavamizi wa mgodi.
Sishabikii
kabisa uvunjifu wa amani wa namna yoyote ile, lakini kimsingi ambacho kilifanyika
huko Nyamongo ni wananchi wa maeneo hayo kuchoshwa na hali ya umaskini
uliokithiri huku ardhi yao ya tangu enzi za mababu ikitema dhahabu
inayowanufaisha wageni wakati wao wakipata madhara ya kiafya pamoja na kuachiwa
mashimo. Wananchi wa Nyamongo, pamoja na maeneo mengine yenye madini nchini,
hawanufaiki na rasilimali zao.
Kabla ya
mgodi huo kupewa wawekezaji ulikuwa ukimilikiwa na wachimbaji wadogo wadogo
waliokuwa wakijipatia mahitaji yao. Lakini baada ya mwekezaji kuchukua maeneo
yote, wachimbaji wadogo hawakuwa tena na kipato cha uhakika, kwa sababu hata
mashamba yao nayo yalichukuliwa na mwekezaji huyo.
Ya
Nyamongo ni picha ya utangulizi wa filamu halisi ambayo inaweza kutokea hapo
baadaye, kwa sababu nguvu ya umma inaweza kuja kutumika ili ‘kugawana’
rasilimali hizo, ambazo ni wazi zinawanufaisha wakubwa wachache serikalini
wanaopenda asilimia 10.
8. Uvurugaji maandamano
Kila mtu
anayo haki ya kwenda kokote ili mradi havunji sheria, ndivyo Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inavyosema. Na Watanzania wanaruhusiwa kukusanyika na
kuandamana kwa amani, huku wakipaswa kupewa ulinzi katika mikusanyiko yao.
Lakini,
imekuwa sivyo kwa Jeshi la Polisi ambalo pamoja na kutokuwa na mamlaka kisheria
ya kuzuia maandamano isipokuwa kwa amri ya Mahakama, limekuwa likitawanya
mikusanyiko yoyote kwa kisingizio kwamba ‘inaleta uvunjifu wa amani’.
Wanafunzi
wakiandamana kudai nyongeza ya posho, wanapigwa mabomu na kutandikwa virungu;
wanasiasa wakiandamana kwa amani kuelezea kero za wananchi kwa serikali,
wanasambaratisha na kuitwa ni wachochezi. Ni kipi hasa ambacho kinaweza kuwa
sahihi kwa Watanzania kukifanya?
Jeshi la
Polisi kwa muda mrefu limetumika kulinda maslahi ya watawala badala ya
Watanzania walio wengi. Unawezaje kujivunia chombo hicho ambacho kinaendesha
shughuli zake kwa kodi za Watanzania hao hao wanaopondwa virungu? Hakuna jibu
makini hapa zaidi ya wahusika kuwajibika kwa kujiuzulu.
9. Dawa za kulevya
Mojawapo
ya kashfa mbaya zilizolikumba jeshi hilo ni kuhusu dawa za kulevya. Biashara
hiyo ambayo imeenea dunia nzima na imekuwa ikipigwa vita, katika miaka ya
karibuni imeshika kasi nchini, ambapo Tanzania inatajwa kwamba ndilo daraja la
kuvushia Cocaine na Heroine kati ya Mashariki ya Mbali, Ulaya na Amerika.
Hii ni kwa
sababu vyombo vya usalama nchini vimelala na hata pale wananchi wanapotoa
ushirikiano wa kukamatwa kwa mizigo ya dawa hizo, Jeshi la Polisi limekuwa
likitumia mwanya huo kujinufaisha.
Mwaka 2006
ilikamatwa maiti ya Kombo Siriri kwenye Mpaka wa Tunduma ikiwa na Cocaine zenye
uzito wa gramu 1,003 zenye thamani ya Sh26.7 milioni. Baadhi ya wahusika
wakatiwa mbaroni, lakini wakati kesi ikiendelea, ikaelezwa kwamba dawa hizo,
ambazo zilikuwa vidhibiti, zilipotea mikononi mwa polisi huko Mbeya. Sheria ni
msumeno, wahusika wakaachiliwa.
Mwaka 2010
zikakamtwa tena Kilogramu 42.5 za dawa za kulevya kwenye mpaka huo huo wa
Tunduma zikiwa na thamani ya Dola za Marekani 822,000 zikisafirishwa na raia
wawili wa Afrika Kusini Vuyo Jack (29) na Anastacia Cloete (Elizabeth) (25),
ambapo zilitokea Arusha zikisafirishwa kwa gari aina ya Nissan Double Cabin
lenye namba za usajili CA 508- 560.
Gari iliyokamatwa na dawa za kulevya iliyokuwa ikiendeshwa na Vuyo Jack.
Anastacia (Elizabeth) Cloete (kushoto) akiwa na bwana'ake Vuyo Jack aliyempakata binti yao Azra ambaye amezaliwa wakati watuhumiwa hao wakiwa mahabusu.
Siku 11
baadaye ikaelezwa kwamba, dawa hizo zilichakachuliwa katika harakati za
kuzibeba na kuzipeleka Dar es Salaam. Kelele za vyombo vya habari zilizofichua
mchezo huo mchafu hazikusaidia kitu kwa sababu inaelezwa kwamba biashara hiyo
imeshikiliwa na vigogo ambao wana mkono mrefu kwenye serikali.
Jambo la
kujiuliza, ni kwa vipi polisi waliohusika na upotevu wa dawa hizo wamefumbiwa
macho bila kuchukuliwa hatua zozote? Badala yake, wengine wamebadilishiwa vituo
tu huku makovu yale ya matendo yao machafu yakiendelea kubakia kwenye
kumbukumbu. U-wapi uadilifu wa Jeshi la Polisi?
Dondoo zaidi za Jeshi la Polisi kuua raia:
Novemba 16, 2007: Polisi watatu walitiwa mbaroni jijini
Dar es Salaam kwa tuhuma za kurusha risasi 18 hewani na kusababisha kifo cha
raia mmoja na kuwajeruhi wengine wawili wa familia moja katika Mtaa wa
Magodoroni, eneo la Kiwalani Minazi Mirefu baada ya askari hao kwenda mahali
hapo wakiwa katika doria ya kawaida.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana (wakati huo) aliwataja askari hao kuwa ni F 7808 PC William, F 5870 PC Rashid na F 7868 PC Marks, ambao walitumia bunduki mbili za aina ya Sub Machine Gun (SMG).
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana (wakati huo) aliwataja askari hao kuwa ni F 7808 PC William, F 5870 PC Rashid na F 7868 PC Marks, ambao walitumia bunduki mbili za aina ya Sub Machine Gun (SMG).
Mwananchi
aliyeuawa katika tukio hilo ni Thomas Mwingira (23) na majeruhi ni Consolata
Mwingira (40) ambaye alipigwa na risasi na kuvunjika mguu wa kushoto pamoja na
mwanafunzi, Joyce Mwingira (15) wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Yombo
Bwawani, jijini Dar es Salaam ambaye alijeruhiwa mguu wa kulia.
Siku
ya tukio, askari hao wakiwa katika doria za kawaida wakiwa na bunduki mbili,
walifika mtaani hapo na kukuta kundi la vijana wakicheza kamari. Walimkamata
Thomas ambaye kwa sasa ni marehemu lakini wenzake walikimbia. Wakati askari hao
wakiwa wamemshikilia Thomas, vijana wenzake waliokuwa wakicheza naye kamari,
walianza kuwashambulia askari kwa kuwarushia mawe. Hali hiyo iliyosababisha
askari hao kujibu mashambulizi kwa kuwafyatulia risasi vijana hao. Wakati tukio
hilo likiendelea, Consolata alifika kwenye eneo la tukio akitokea ndani ya
nyumba yao iliyopo karibu na hapo. Askari hao walifyatua jumla ya risasi 18
ambazo 14 kati ya risasi hizo, zilifyatuliwa na askari mmoja na nne nyingine,
zilifyatuliwa na askari mwingine.
Machi 1, 2009: Polisi wanadaiwa kuwaua kwa kuwapiga risasi vijana wawili eneo la Kijenge/Mwananama karibu na Mount Meru Petrol Station Kijenge jijini Arusha.
Tukio hilo lilitokea baada ya vijana hao kujibizana na mhudumu wa kike kwa kile
kilichosemekana ni mhudumu kudaiwa chenji na yeye kudai ameshatoa. Kijana
aliyekuwa anaendesha gari alimpiga kibao mhudumu huyo na ndipo mhudumu akaita
polisi waliokuwa karibu. Polisi waliwasimamisha vijana hao na kuwaamuru washuke
kwenye gari, ndipo walipowamiminia risasi.
Machi 5, 2012:
Kijana Hassan aliuawa na polisi mjini Urambo baada ya kuhoji ni kwa nini polisi
hao walimgonga na bhajaji. Hassan alihoji: kwanini umenigonga? Polisi akajibu:
kwani unataka nini? Hassan akasema: yaani unanigonga na baiskeli na unasema
nataka nini? Hassan akampiga kibao askari huyo ambaye alikuwa amevaa nguo za
kiraia. Kufatia hali hiyo askari huyo aliondoka na kuwafuata wenziwe ambao
walikuwa na nguo za kiraia na walimkuta Hassan akicheza pool katika eneo la
Stendi ya zamani wilayani humo. Wakamshushia kipigo cha hali ya juu na kumvuta,
mmoja akimshika mguu wa kulia na mwingine mguu wa kushoto kichwa kikijiburuza
chini umbali wa meta 2000 mpaka karibu na ofisi ya Ushirika ya Urambo na benki
ya NMB ambako walimtupia katika bhajaji hiyo huku mmoja akiwa amemkanyaga
kichwa chake. Kutokana na mateso makali aliyoyapata Hassan alipoteza maisha.
Katika jalada lililofunguliwa kwenye Kituo cha Polisi Urambo maelezo
yaliandikwa amepigwa na wananchi wenye hasira, jambo ambalo si kweli na
lilileta utata kati ya wanafamila na wananchi wa eneo hilo. Hatima yake
haijulikani.
Agosti 30,
2012: Jeshi
la Polisi liliendelea kuandamwa na matukio ya kuua raia baada ya askari wake
wanne, akiwemo Mkuu wa Kituo (OCS) kukamatwa kwa tuhuma za kuvamia nyumba ya
kulala wageni ya Buziku Inn, kujeruhi, kupora mali na kumuua mchimbaji wa
madini.
Tukio hilo lilitokea
katika Wilaya ya Chato, mkoani Geita baada ya askari hao kutuhumiwa kuwavamia
wafanyabiashara wawili waliokuwa kwenye nyumba hiyo, kuwapora Shs. 500,000,
mawe yanayosadikiwa kuwa dhahabu na kuwajeruhi kwa vipigo ambavyo vilisababisha
kifo cha mmoja wao.
Askari waliotuhumiwa kuhusika katika tukio hilo ni wa kituo cha
polisi cha Buziku wilayani Chato ambao waliwavamia David Gilles Vyamana na
Gilbert Ntabonwa, wakazi wa kijiji cha Kakeneno wilayani humo na wazaliwa wa
Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.
Watu hao wanaosadikiwa kuwa ni wachimbaji wadogo
wa dhahabu, kabla ya kukumbwa na mkasa huo, walitokea kijijini kwao Kakeneno na
kuelekea kijiji cha Buziku kwa ajili ya kuburudika na kwamba baada ya kupanga
vyumba katika nyumba hiyo mmoja akiwa chumba namba mbili na mwingine namba
tatu, walimuomba mhudumu kuendelea kuwahudumia vinywaji wakiwa vyumbani.
Majira ya saa 5:30 usiku, polisi walivamia eneo
hilo na kuwaamuru wachimbaji hao kufungua milango ya vyumba vyao. Baada ya watu
hao kukataa kutii amri hiyo huku wakihoji uhalali wa kuwaamuru kufungua milango
wakati wamelala, askari hao walitumia nguvu kubwa na kufanikiwa kuvunja milango
kisha kuanza kuwaadhibu kwa vipigo vikali.
Novemba 29, 2012:
Kijana mmoja huko Tegeta jijini Dar es Salaam alipigwa risasi ya moto na
kufariki na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya polisi kurusha risasi hovyo
wakiwa kwenye operesheni ya kuondoa magari yanayopaki barabarani. Kijana huyo
alikuwa kwenye duka la magodoro akifanya manunuzi.
Februari 27, 2013: Mwalimu wa Shule ya
Sekondari Kitulo, wilayani Makete, Castory Sote Kawambwa (31) mkazi wa Mbalizi
mkoani Mbeya, aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Makete na askari polisi
aliyekuwa zamu kwenye Benki ya NMB. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:30
usiku. Marehemu alifika kwenye eneo hilo la benki akiwa amepanda bodaboda ili
kuchukua fedha kwenye mashine maalum (ATM). Askari polisi aliyefanya mauaji
hayo, PC Gervas Joseph, mwenye namba 9790, alifukuzwa kazi.
Machi
4, 2013: Majira ya saa 6:00 mchana, wananchi
wa Kijiji na Kata ya Mtimbwilimbwi, Tarafa ya Nnyamba, Mtwara Vijijini,
walifunga barabara kutoka Mtwara kwenda Tandahimba na Newala, wakiishinikiza
serikali iharakishe na kusimamia utaratibu wa upatikanaji wa malipo ya pili ya
zao la korosho.
Mkuu wa wilaya alifika kuongea na wananchi, akawa hajatoa majibu yoyote ya kuwaridhisha, wakamzomea, baada ya hapo Mkuu wa Wilaya aliita polisi kuja kuwatawanya wananchi hao kwa mabomu, lakini katika mabomu hayo mwananchi mmoja aliyejulikana kwa jina la Said, mfanyabiashara akapigwa risasi ya moto na kufariki papo hapo.
Baada ya kufariki wananchi walitafuta gari wakapakia maiti, walipokuwa kwenye gari, OCD Tumtufye Mwakajamba akiwa na nguo za kiraia alianza kupongeza jeshi la polisi, na kuwabeza wananchi kuwa wanapenda fujo. Wananchi kwa kuwa hawamfahamu walimpatia kipigo cha kutosha hadi akaokolewa na wanaomfahamu.
Mkuu wa wilaya alifika kuongea na wananchi, akawa hajatoa majibu yoyote ya kuwaridhisha, wakamzomea, baada ya hapo Mkuu wa Wilaya aliita polisi kuja kuwatawanya wananchi hao kwa mabomu, lakini katika mabomu hayo mwananchi mmoja aliyejulikana kwa jina la Said, mfanyabiashara akapigwa risasi ya moto na kufariki papo hapo.
Baada ya kufariki wananchi walitafuta gari wakapakia maiti, walipokuwa kwenye gari, OCD Tumtufye Mwakajamba akiwa na nguo za kiraia alianza kupongeza jeshi la polisi, na kuwabeza wananchi kuwa wanapenda fujo. Wananchi kwa kuwa hawamfahamu walimpatia kipigo cha kutosha hadi akaokolewa na wanaomfahamu.
Mei 10, 2013: Mtoto Deo Yakobo (9) ambaye ni
mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Mturu mjini Tarime, aliuawa
na polisi kwa kupigwa risasi kichwani na kufumuliwa ubongo. Polisi hao walidai
kwamba walikuwa wakiwakamata majambazi wanaoiba na kuua watu mpakani mwa
Tanzania na Kenya.
Juni 19, 2013: Rajabu Wilson (25), mkazi wa kijiji cha Lumbila wilayani
Mbozi mkoani Mbeya, aliuawa na polisi na askari wanne kujeruhiwa vibaya
baada ya wananchi kuwashambulia polisi waliokuwa katika msako wa wahalifu katika Mlima
Senjele majira ya saa 7:00 mchana kwa kilichodaiwa kuwazuia polisi kufanya kazi
yao.
Hitimisho:
Tutaendelea
kushuhudia mauaji ya watu mikononi mwa polisi huku tukidanganywa na ‘tume’
wanazojiundia wenyewe! Naam, ni tume za manyani kuchunguzana waliokula mahindi!
0656-331974
No comments:
Post a Comment