Kwa kuwa tabia ya Serikali ya Zanzibar
ya kupuuza vifungu fulani vya Katiba ya Muungano ndiyo iliyokera watu wengi na
hatimaye ikazua hoja ya kutaka Serikali ya Tanganyika, nilidhani kuwa baada ya
Zanzibar kukiri kosa lake na kutoka katika OIC, Serikali zote mbili zingekaa
pamoja na kutazama sehemu nyingine za Katiba zinazopuuzwa ama na Serikali ya
Zanzibar au Serikali ya Muungano. Badala yake Serikali ya Muungano ikiendekeza
Utanganyika, na ikakubali hoja ya Serikali Tatu. Sasa naamini kuwa Serikali ya
Muungano haiwezi tena kufuatilia kwa makini mazungumzo yake na Serikali ya
Zanzibar kuhusu Katiba ya Nchi yetu. Kwa sababu zifuatazo:
Sababu moja kubwa iliyofanya
Viongozi wetu wasitake kuwaudhi "Wazanzibari" katika suala la OIC na
uchaguzi wa Makamu wa Rais, ni umuhimu wa kura za Zanzibar katika kumteua
mwanachama wa CCM kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi ye
yote anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu kupita mengine yote, kuwaudhi
"Wazanzibari" ni dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila njia Ndiyo
maana Viongozi wa Zanzibar walipoomba nia yao ya kuingia katika OIC izungurnzwe
na Kamati Kuu, na baadaye na Halmashauri Kuu ya Taifa, Viongozi wetu waheshimiwa
hawakupenda hata kidogo suala hilo lizungumzwe. Walijua kuwa Zanzibar haiwezi
kuingia katika OIC bila kuvunja Katiba ya Nchi yetu; na kwamba suala hilo
Iikizungumzwa katika vikao hivyo vya Chama, wako Viongozi watakaolipinga, na
wataka urais watapata tatizo: Kupinga au kutopinga, litakuwa suala gumu! Kwa hiyo
wakamshauri Rais lisizungumzwe katika vikao vya Chama, ila yeye mwenyewe
achukue jukumu la kulizungumza na Viongozi wa Zanzibar, Suala likiwa gumu,
usimsaidie Rais, mtupie!
Zanzibar wakaingia katika OIC.
Viongozi wetu wakafanya kila njia ya kufanya kitendo hicho kisijulikane, au
baadaye kushindwa kukificha kipuuzwe. Haikuwezekana. Kikafichuliwa, na ngoma
zikaanza. Hatimaye "Watanganyika" wakachoka na wakaanza kudai
Serikali ya Tanganyika. Kwa mtaka urais hii ilikuwa balaa mpya; maana si 'Wazanzibari"
peke yao ambao wanazo kura za uteuzi wa wagombea urais na baadaye uchaguzi
venyewe;
"Watanganyika" nao
wanazo, tena nyingi zaidi. Kwa Kizungu hali hii huitwa "dilemma"; ni
utatuzi wa uamuzi, kama penye njia panda:
Kifo cha maji kushoto,
Kulia kifo cha moto:
Kukubali, kukataa,
Kila moja ni balaa!
Kote uko hatarini,
Hujui ufanye nini.
Kwa hiyo Waziri Mkuu alipomwambia
Rais kwamba hoja ya Serikali Tatu ikijadiliwa Bungeni, yeye mwenyewe atakuwa na
utatuzi wa uamuzi, alikuwa anajisemea kweli yake. Alikuwa katika hali hii ya
"dilemma". Baadaye, kama tunavyojua, alipoambiwa kuwa asipokubaliana
na wenzake ataachwa katika mataa, aliamua kusarenda na wote wakaunga mkono hoja
ya Utanganyika.
Hawa si watu wajinga, na wala si
wapumbavu; wanajua wafanyalo. Wamefanya uamuzi huu wakijua matokeo yake. Kwa
hawa sasa, makosa ya "Wazanzibari", yawe ya kuvunja Katiba au ya aina
nyingine, kwao sasa ni faraja; ni hoja ya kudai Utanganyika. Hawa hawawezi tena
kutaka makosa hayo yazungumzwe, na yasahihishwe; maana yakisahihishwa, kama
lilivyosahihishwa lile la OIC, msingi wale wa hoja yao utabomoka. Katika hili,
"Wazanzibari" na "Watanganyika", ni mbuya wakuu; ni
washiriki na wabia kwenye mradi ule ule wa kutaka kuvunja Tanzania.
Lakini hata kama wangekuwapo
mawaziri ambao si "Watanganyika", bali ni Watanzania halisi
wanaopenda kukaa na Watanzania wenzao wa Visiwani ili kuzungumza masuala ya
Katiba, hawawezi kufanya hivyo chini ya uongozi wa sasa wa Serikali ya
Muungano. Katiba inayozungumzwa ni Katiba hii ya sasa, ya muundo wa Serikali
Mbili. Hoja ya Utanganyika ilipoletwa Bungeni Serikali ilikuwa tayari imeteua,
au inakusudia kuteua, Kamati ya kutazama migogoro ya Katiba iliyopo hivi sasa
kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, na kufanya mapendekezo ya
kuiondoa.
Tulitazamia kuwa serikali ya
Muungano itapinga hoja ya Utanganyika, na kuwaarifu Wabunge kwamba Kamati hiyo
itapokamilisha kazi yake Serikali itafikisha mapendekezo yake Bungeni. Badala
ya kufanya hivyo, Serikali ya Muungano ikaamua kuwa mfumo wa Serikali Mbili
haufai, kinachofaa ni mfumo wa Serikali Tatu. Hivi sasa sera ya Serikali ya
Muungano ni muundo wa Serikali Tatu.
Itawezekanaje Serikali hiyo hiyo
ikae chini na Serikali ya Zanzibar kuzungumzia umuhimu wa kutii, au jinsi ya
kurekebisha muundo wa Serikali Mbili? Kwao Katiba hiyo inachongojea ni kufutwa
tu. Mapendekezo ya Kamati ya Ndugu Shellukindo na wenzake hayana maana tena kwa
Serikali hii. Serikali ya sasa inachosubiri na inachokishughulikia ni
Shirikisho la Serikali Tatu- kwa kweli kufa na kuzikwa kwa Tanzania. Hawana
uhalali, wala uwezo, wala nia ya kuzungumza Muungano wa Serikali Mbili. Kwa
kweli jambo moja ambalo waheshimiwa hawa wamefaulu ni kufanya watu waache
kabisa kuzungumza Katiba ya sasa na mambo mengine yale muhimu, na wabaki
kumkimbiza sungura wa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano".
Maadamu matatizo halisi ya
Muungano hayazungumzwi wala hayashughulikiwi, watu wenye nia mbaya, wa Bara na
Visiwani, wanaopenda kuitumia hali hiyo kuivunja nchi yetu wanaendelea kufanya
hivyo. Na wale, wa huku na huku, wanachocheana kama mifukuto ya shetani. Na
hiyo inawafanya hata watu wasio na nia mbaya, ila ni wajinga tu, waamini kuwa inafaa
wote tushiriki na tujiandae kuivunja Tanzania tusije tukashtukia kuwa Tanzania
imevunjika na tumeachwa katika mataa! Anayedhani kuwa viongozi wetu ni wajinga
yafaa akachunguzwe akili zake! Wanajua wafanyalo.
Nimesema awali kwamba
"Wazanzibari" na "Watanganyika" ni marafiki wakuu. Matendo
ya "Wazanzibari" ni kisingizio kizuri cha matendo ya "Watanganyika":
na matendo ya "Utanganyika" ni kichocheo cha ukabila wa upande wa
pili. Wenyewe wanauita "Utaifa", na ni sawa maana ni wa kupinga
Utanzania. Serikali yenye msimamo wa Utanganyika haiwezi kukaa na Serikali ya
Zanzibar kuzungumza katiba hii ya Serikali Mbili. Hilo linaweza kufanywa na
Serikali mpya y a Jamhuri ya Muungano: Serikali inayokubali na kuheshimu Katiba
tuliyo nayo.
Serikali inayokubali na kuheshimu Katiba tuliyo nayo. Selikali ya sasa haina uhalali wala uwezo wala nia ya kuizungumza, ukiacha mazungumzo ya kuitia maji ili kuwafurahisha "Wazanzibari", au kuifuta ili tulete Shirikisho la Serikali Tatu na hivyo kuwafurahisha "Watanganyika".
Serikali inayokubali na kuheshimu Katiba tuliyo nayo. Selikali ya sasa haina uhalali wala uwezo wala nia ya kuizungumza, ukiacha mazungumzo ya kuitia maji ili kuwafurahisha "Wazanzibari", au kuifuta ili tulete Shirikisho la Serikali Tatu na hivyo kuwafurahisha "Watanganyika".
REJEA:
NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
No comments:
Post a Comment