Tarehe 24:8: 1993, siku kumi tu baadaye, viongozi wetu wakuu wanapata
ndoto nzuri zaidi, wanasarenda na kupitisha Bungeni hoja "muafaka" ya
kuleta Serikali ya Tanganyika "ndani ya Muungano". Miezi miwili
baadaye, Oktoba, 1993, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, inaandaa
mapendekezo na kuyafikisha mbele ya Halmashauri ya Taifa, kuitaka ikubali
pendekezo la Serikali la kuunda Shirikisho la Serikali Tatu. Abautani zote
mbili, ya Serikali na ya Kamati Kuu, zinafanyika kana kwamba ni mambo ya
kawaida tu: .Bila swali, bila maelezo!
Kukubali kufanywa vikaragosi vya viongozi ni dalili ya woga, si dalili
ya heshima; na woga na heshima ni vitu viwili mbali mbali. Maadili mema
hayatudai tuwaogope viongozi wetu. Na viongozi makini hupenda kupata heshima ya
wananchi wenzao, lakini hawapendi kuogopwa. Kuogopwa ni sifa na ada ya madikteta,
viongozi halisi hawapendi kuishiriki. Kujenga mazoea ya kutii viongozi hata
katika mambo haramu ni dalili ya woga, ni kukaribisha udikteta.
Kamati Kuu ikishakuwa na mshikamano katika jambo lo lote, hata kama
mshikamano huo ni wa bandia, na umetokana na woga, matokeo yake ni yale yale katika
vikao vingine vya Chama. Ni vigumu sana kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kupinga
Kamati Kuu yenye msimamo mmoja, kwa sababu zile zile zinazofanya iwe vigumu
sana kwa Kamati Kuu kupinga viongozi wakuu wenye msimamo mmoja katika suala
lolote. Kupinga viongozi wenye msimamo mmoja kunataka ujasiri mkubwa sana,
maana anayethubutu kufanya hivyo huonekana kama mwasi au msaliti.
Ndiyo maana katika suala la utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais,
nilipotambua kuwa Kamati Kuu itakuwa na msimamo mmoja katika kupendekeza kwa
Halmashauri Kuu ya Taifa, kwamba utaratibu wa sasa uendelee, niliomba nipatiwe
nafasi nami nikatoe maoni yangu mbele ya kikao hicho. Inawezekana kuwa tatizo
la paka kwa panya lingekwisha kama paka angefungiwa kengele shingoni: taabu ni
kumpata panya wa kuifanya kazi hiyo. Na panya watakuwa wajinga sana wakidhani
kuwa paka watajifunga au watafungana kengele shingoni!
Hatuwezi kuachia utamaduni wa woga ukawa ni mbinu au sifa mpya ya
uongozi. Na sasa lazima tukiri kwamba utamaduni huu wa woga unaanza kuwa ni
sehemu ya tatizo letu la kitaifa.
Nilisema awali kwamba nilionana na baadhi ya wabunge wenye hoja ya
Utanganyika. Wale walipokwisha kutoa dukuduku zao kuhusu madhambi ya Serikali,
niliwaambia: "Waheshimiwa wabunge, yale mliyoyasema ni sababu nzuri za
kuchukua hatua za kuwadhibiti viongozi wahusika; kwa nini badala ya kufanya
hivyo mnachukua hatua za kutaka kuigawa nchi yetu?" Jibu lao:
"Viongozi wakisemwa wanakuwa wakali sana!" Viongozi wetu nao
nilipowauliza: "Kwa nini hamkupinga hoja ya wabunge kama tulivyokuwa
tumekubaliana, na badala yake mkaamua kuikubali?" Jibu lao; "Wabunge
hao walipotoka kwako Msasani walikuwa wakali kama mbogo!" Na wajumbe wa
Kamati Kuu ukiwauliza: "Kwa nini hamkukataa pendekezo la Serikali la
kukubali hoja ya SerikaIi Tatu?" Jibu lao: “Wakubwa walikwisha
kukubaliana, sisi tungeweza kufanya nini?" Hata mtu mmoja hakuweza kupaza
sauti na kusema: hivi sivyo? Hii ndio demokrasia mpya na mbinu mpya ya kukabiliana
na Mfumo wa Vyama Vingi? Huko ndiko kwenda na wakati?
Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi
isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona chama kizuri
cha upinzani kinachoweza kuiongoa nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi
ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi.
Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza
kuiongoza nchi yetu badala ya CCM au ambacho kingekilazimisha Chama Cha
Mapmduzi kusafisha uongozi wake kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa
katika uchaguzi ujao.
Lakini bado sijakiona chama makini cha upinzani; wala dalili zozote za
kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila
demokrasia halisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, Chama hili kitazidi kudidimia
chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini, hili
si jambo la kutarajia bila ya hofu na wasi wasi! Wazalendo Watanzania hawana
budi wapende kuona demokrasia halisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi: Hii ina sura
mbili.
Kwanza, ni lazima kurudisha tena uhuru na utaratibu wa kujadili masuaIa
yote makubwa na kufikia uamuzi baada ya mjadala. Viongozi wetu hivi sasa
wanaogopa kutumia nguvu za hoja ili kutoa maamuzi muhimu. Kwa sasa wanatumia
hila zaidi kuliko hoja; vitisho kwao ni mbinu rahisi zaidi kuliko adha ya kutumia
akili na kupata hoja safi ya kumjibu mpinzani katika mjadala. Viongozi hawa
wakipewa nafasi watatumia hoja ya nguvu tu; na hawatakuwa na haja ya kutumia
akili. Kichini chini baadhi yao tayari wameanza kutumia hoja ya vitisho. Na
kama tukiacha utamaduni wa woga ukazagaa tutakuwa tunakaribisha udikteta.
Uhuru hauji wala haudumishwi bila kuwa tayari kulipa gharama zake; na vitu vile vyenye thamani kubwa gharama yake ni kubwa. Chama Cha Mapinduzi lazima kiendelee kujenga utaratibu na utamaduni wa kuchambua masuaIa makubwa katika mijadala, na kufikia uamuzi baada ya uchambuzi na mijadaIa ya kidemokrasia na ya wazi wazi. Na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo vyao lazima waanze kupiga vita utamaduni wa woga na fidhuli ya viongozi.
Uhuru hauji wala haudumishwi bila kuwa tayari kulipa gharama zake; na vitu vile vyenye thamani kubwa gharama yake ni kubwa. Chama Cha Mapinduzi lazima kiendelee kujenga utaratibu na utamaduni wa kuchambua masuaIa makubwa katika mijadala, na kufikia uamuzi baada ya uchambuzi na mijadaIa ya kidemokrasia na ya wazi wazi. Na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo vyao lazima waanze kupiga vita utamaduni wa woga na fidhuli ya viongozi.
Aidha, Chama Cha Mapinduzi hakina budi kitazame upya utaratibu wake wa
kuchagua viongozi wake wakuu. Na muhimu zaidi na la haraka zaidi, Chama Cha
Mapinduzi hakina budi kitazame upya utaratibu wake wa kuteua mgombea wake wa
kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano. Nasema hili ni jambo muhimu na la haraka
zaidi kwa sababu uchaguzi wenyewe ni mwakani tu. Hili lisipofanyika upesi na
kwa makini, yanaweza yakafanyika makosa yatakayofuta kabisa uwezo wetu wa kufanya
hivyo baadaye.
Nina hakika kwamba utaratibu wetu wa sasa wa kuteua mgombea kiti cha
urais sasa umekwisha kupitwa na wakati. Mimi nilikuwa nikiteuliwa na
HaImashauri Kuu ya Taifa baada ya kupendekezwa na Kamati Kuu bila mshindani. Na
ndugu Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa katika mazingira ya siasa ambayo hayakuwa
tofauti sana. Hapakuwa na washindania urais. Ni Kamati Kuu yenyewe iliyoamua ni
nani wafikiriwe; na mmoja wao, nakumbuka, alikuwa hataki hata kidogo; tukalitoa
jina lake.
Lakini sasa mambo ni tofauti. Washindania urais wapo, tena moto moto.
Chama kinajua hivyo, na wananchi wanajua hivyo. Chama Cha Mapinduzi hakina budi
kitafute utaratibu mzuri wa kuwashindanisha wataka urais hawa kwa njia ya wazi
wazi. Tutafanya makosa makubwa tukikubali kuteua mgombea urais kwa kutumia
mzengwe. Njia ya mzengwe ilitufaa tu wakati tulipokliwa hatuna washabiki wa
urais. Na inaweza kufaa kama mnataka kumteua mwenzenu ambaye mnaamini kuwa
ndiye anayefaa, lakini hapendi misukosuko ya kushindania uongozi.
Hivyo sivyo mambo yalivyo sasa. Sasa tunao washabiki, tena washabiki wa
kweli kweli! Kwa hiyo hali ya sasa inataka ushindani wa wazi wazi, na ni vema
Chama Cha Mapinduzi kitafute utaratibu mzuri wa kuwashindanisha hivyo. Ni
muhimu zaidi kuwataka wanachama wa CCM watoe maoni yao kuhusu Rais wetu wa
baadaye, kuliko kuwataka watoe maoni yao kuhusu Serikali ya Tanganyika, jambo
ambalo walikuwa wala hawaIifikirii. Chama kisisite kutafuta utaratibu wa
kushirikisha wanachama katika suala hili, kabla vikao vya juu havijafanya
uamuzi wa mwisho.
Ni vizuri katika suala kama hili mwongozo wa awali ukatokana na
wanachama wenyewe baada ya kupitiwa na wataka urais. Katika uchaguzi wa
madiwani, chama kimeanza kutumia utaratibu wa kutafuta kwanza maoni ya
wanachama kabla ya kuomba vikao vya juu kufanya uteuzi wa mwisho. Utaratibu huu
ni muhimu zaidi kwa kutupatia mgombea urais kuliko mgombea udiwani.
Nchi yetu bado changa. Tusione haya kuendeleza taratibu ambazo
zinaonekana kuwa zinafaa, na wala kubadili zile ambazo japokuwa huko nyuma
zimetufaa, lakini sasa "zimepitwa na wakati." Ndivyo tulivyofanya
kuhusu mfumo wa chama kimoja; tusiogope kufanya hivyo kuhusu mageuzi ya kuleta
demokrasia zaidi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Inawezekana kwamba demokrasia peke yake ambayo kwa sasa itaendelea kuwa
na maana kwa nchi hii wakati tunasubiri kupata mpinzani mzuri na makini nje ya
CCM, ni demokrasia ndani ya CCM. Wanachama wa CCM wana wajibu wa kukitazama
upya chama chao na kuona jinsi ya kuongeza demokrasia ndani yake. Wajibu huu si
kwa chama chao tu, ni wajibu wa uzalendo kwa manufaa ya Tanzania nzima.
Ole wake
Tanzania
Tusipoisaidia!
Niwezalo
nimefanya:
Kushauri na
kuonya.
Nimeonya:
Tahadhari!
Nimetoa ushauri:
Nimeshatoka
kitini;
Zaidi nifanye
nini.
Namlilia Jalia
Atumulikie njia;
Tanzania
ailinde,
Waovu
wasiivunde.
Nasi tumsaidie
Yote tusimwachie!
Amina, tena
Amina!
Amina tena na
tena!
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
SOMA ZAIDI HAPA:

No comments:
Post a Comment