Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George
Simbachawene akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Wakurugenzi wa Halmashauri za
Miji, Manispaa na Wilaya 13 walioteuliwa hivi karibuni. Hafla hiyo ilihudhuriwa
na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Angella Kairuki, Naibu
Waziri Selemani Jafo, baadhi ya wakurugenzi, wafanyakazi kutoka OR-TAMISEMI
pamoja na waandishi wa habari.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki akiongea Wakurugenzi
wapya mara baada ya kuapishwa leo mjini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George
Simbachawene. Kushoto kwa Simbachawene ni Mkurugenzi mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kilimanjaro Bi. Butamo Nuru Ndalahwa.
Baadhi ya Wakurugenzi wa halmashauri wakisaini hati ya kiapo cha maadili ya
utumishi wa umma pamoja na ahadi ya kuwa waaminifu na wazalendo kwa nchi yao leo
katika ofisi za TAMISEMI mjini Dodoma mbele ya Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili
ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Kanda ya Kati Cathlex Makawia.
Na Nasra Mwangamilo- Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene amewaasa Wakurugenzi
wapya kusimamia mapato ya ndani katika halmashauri zao ili waweze kutekeleza
miradi ya maendeleo na kuwahudumia wananchi.
Waziri Simbachawene
amesema hayo leo mjini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha Wakurugenzi wapya
13 walioteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli iliyofanyika katika jengo la Mkapa, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mkoa na Serikali za Mitaa mjini Dodoma. Pamoja na kuapishwa, Wakurugenzi hao
walikula kiapo cha maadili ya utumishi wa umma pamoja na ahadi ya kuwa
waaminifu na wazalendo kwa nchi yao.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Waziri Simbachawene alisema Wakurugenzi hao wanawajibu wa kusimamia
mikataba iliyopo, iliyopita na itakayoingiwa na halmashauri zao ikiwa ni pamoja na kuzingatia masharti ya
mikataba hiyo wakati wa utekelezaji wake. Aidha, aliwahimiza kuwa wawajibikaji kwa
mamlaka waliyonayo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kikatiba.
“Kuanzia leo mnaitwa
viongozi, unapokuwa kiongozi unalazimika kuishi kwa namna tofauti kabla ya
kuapishwa kuwa kiongozi, eneo mnaloenda kufanya kazi ni muhimu na mnaenda
kuongoza taasisi na mnaenda kuwahudumia wananchi moja kwa moja” alisema
Simbachawene.
Waziri Simbachawene
amewaeleza Wakurugenzi hao kuwa unapozungumzia kuondoa umasikini wa wananchi,
Mkurugenzi ndiye anayebeba bendera na dhamana ya kusimamia sekta zote ndani ya
halmashauri ikiwemo afya, kilimo, elimu, maji, uvuvi ambazo zitawaletea hali
bora ya maisha ya wanachi hao.
Katika kuyatekeleza majukumu
hayo, Waziri Simbachawene amewahimiza wakurugenzi hao kufanya kazi na Wizara
zote kwa kufutata sera mbalimbali na miongozo inayotolewa na viongozi wakuu wa nchi
akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Simbachawene
amewataka Wakurugenzi hao kutembelea maeneo yao katika halmashauri zao badala
ya kukaa ofisini kuanzia tarehe 1 hadi 30 kila mwezi ili kujionea changamoto
zinazowakabili wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
“Tokeni ofisini na
tembeleeni maeneo yenu, mna mambo mengi ya kufanya, ni lazima uwajue wananchi, viongozi
unaofanya nao kazi, taasisi na watumishi wako kwa takwimu ikiwezekana kwa
majina” alisisitiza Waziri Simbachawene.
Kwa upande wake
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Angellah Kairuki
amewataka Wakurugenzi hao wafuatilie na kusimamia miradi ya maendeleo iliyopo
ndani ya halmashauri zao kwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa
kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kuhusu watumishi
hewa, Waziri Kairuki amesema kuwa hadi sasa wamebainika watumishi hewa 17,102
tangu kuanzishwa zoezi hilo Machi mosi mwaka huu na kuwaasa wakurugenzi hao
kufuatilia watumishi ndani ya halmashauri zao ili kuondokana na dhana ya kuwa
na watumishi hewa ndani ya halmashauri zao.
Ili kuwa na taarifa
sahihi, Waziri Kairuki amewataka Wakurugenzi hao watumie mifumo sahihi ili
kutoa taarifa sahihi za watumishi na kuondoa dhana ya watumishi hewa ndani ya
halmashauri zao.
Kwa upande wao Mkurugenzi mpya wa halmashauri ya wilaya ya Bukoba
Mwantumu Dau na Frank Bahati wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe wamemshukuru
Rais kwa kuwateua na kuhahidi kutomuangusha ambapo na watawatumikia wananchi
kwa nguvu zao zote katika kuwaletea maendeleo.
Wakurugenzi 13 wa
Halmashauri za Manispaa, Mji na Wilaya walioapishwa na Katibu Msaidizi
Sekretarieti ya Maadili ya Vingozi wa Umma, Ofisi ya Kanda ya Kati Cathlex
Makawia ni pamoja na Godwin Emmanuel Kunambi Manispaa ya Dodoma, Elias R.
Ntiruhungwa Mji waTarime, Mwantumu Dau Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Frank
Bahati Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Hudson Stanley Kamoga Halmashauri ya
Wilaya ya Mbulu, Mwailwa Smith Pangani Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Godfrey
Sanga
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na Yusuf Daudi Semuguruka Halmashauri
ya Wilaya ya Ulanga.
Wakurugenzi wengine
ni Bakari Kasinyo Mohamed Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Juma Ally Mnweke
Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Butamo Nuru Ndalahwa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Waziri Mourice
Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na Fatma
Omar Latu Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment