Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akipokea moja ya mfuko wa saruji kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT-CCM) Sophia Simba ukiwa ni miongoni mwa mifuko 200 sa saruji iliyotolewa na UWT kusaidia maafa Kagera.
Baadhi ya wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT-CCM) wakipakia mifuko ya saruji kwenye gari tayari kwa kupelekwa kwenye ghala la kukusanyia misaada inayyotolewa ili kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi.
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba.
Mkoa wa Kagera bado unaendelea kupokea misaada kutoka taasisi, mashirika ya dini, mashirika binafsi, vyama vya siasa pamoja na nchi mbalimbali ili kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililoathiri maeneo mbalimbali ya mkoa.
Katika kuhakikisha wakazi wa mkoa huo walioathiriwa na tetemeko la ardhi, wadau nchini wanendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii ikiwemo vifaa vya ujenzi, vyakula pamoja na vifaa tiba.
Akikabidhi msaada wa mifuko 200 ya saruji iliyotolewa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT-CCM) Katibu wa umoja huo Amina Makiragi amesema kuwa mchango ni chachu inayolenga kupaza sauti ili kuhamasisha wananchi na wadau wengine kuendelea kutoa misaada yenye lengo la kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Katibu huyo wa UWT-CCM ameipongeza Serikali kwa hatua walizochukua katika kutatua la tetemeko la ardhi kwa umahiri mkubwa na kuanza kuchukua hatua za kurejesha miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za kijamii ikiwemo shule, vituo vya afya na barabara.
Aidha, Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho Sophia Simba amesisitiza kuwa katika maafa yeyote, wanawake na watoto mara kwa mara ndio wamekuwa waathirika wakubwa wa majanga yanayoikumba jamii.
Ili kuhakikisha misaada inayotolewa na wadau mbalimbali nchini, Mwenyekiti Sophia ametoa wito kwa Kamati ya maafa kusimamia misaada hiyo ipasavyo na kuigawa kwa wakati kwa walengwa hasa wahitaji ambao wameathiriwa na tetemeko hilo na kuongeza kuwa ni fahari kuona ghala lipo wazi baada ya misaada iliyokusanywa kupelekwa kwa wahusika.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ametoa shukrani kwa UWT kwa moyo wa kuwajali waathirika wa maafa yaliyotokana na tetemeko la ardhi mkoani humo.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amewaasa wadau wengine kuendelea kutoa misaada na michango yao na kuwahakikishia kuwa misaada hiyo itatumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment