Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja
Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akiongea na wawakilishi wa familia waliopoteza
ndugu zao (hawapo pichani) kwa tetemeko la ardhi lililotokea mapema Septemba 10
mwaka huu Bukoba mjini wakati wa kukabidhiwa rambirambi iliyotolewa na Serikali
milioni 17 pamoja na kampuni ya simu ya Halotel ambayo imetoa shilingi milioni
15. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Maafa.
Yusta Jonas mkazi wa
Hamugembe Manispaa ya Bukoba akipokea rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambayo imetolewa na Serikali pamoja na
kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
Mzee Vedasto Kato kutoka mtaa
wa Hamgembe Manispaa ya Bukoba akipokea rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambayo imetolewa na Serikali pamoja na
kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja
Jenerali Mstaafu Salum Kijuu (katikati aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja
na wawakilishi wa wanafamilia waliofiwa na ndugu zao wakati wa tetemeko la
ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu.
(Picha na
Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba)
Na
Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba
Familia 15 zilizofiwa na ndugu
zao 17 wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani wa Kagera zimepokea
rambirambi ya jumla ya shilingi milioni 32 ikiwa ni mkono wa faraja kwa msiba
uliwafika familia hizo na taifa kwa ujumla.
Rambirambi hiyo imetolewa mjini
Bukoba na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kwa niaba ya
Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya simu za mkononi nchini ya Halotel ili
kuwashika mkono wafiwa hao kwa kupoteza ndugu na jamaa zao.
Katika rambirambi hiyo, Serikali
imetoa shilingi milioni 17 na kampuni ya simu ya Halotel imetoa shilingi milioni
15 ambapo kila familia ya mfiwa amepokea shilingi 1,000,000 kutoka Serikalini
na shilingi 885,000 kutoka kampuni ya Halotel.
Hatua hiyo inapelekea kila familia
ya mfiwa kupokea jumla shilingi 1,885,000 ambapo familia mbili zilizopoteza
ndugu zao wawili wawili wamepokea jumla ya shilingi 3,770,000 ikiwa ni rambirambi
kwa kila ndugu aliyefariki wakati wa tukio hilo la tetemeko la ardhi.
Akikabidhi rambirambi hiyo kwa
familia hizo, Mkuu wa Mkoa wa huo akiwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa mkoa Meja
Jenerali Mstaafu Kijuu amesema kuwa Serikali imetoa rambirambi hiyo kwa lengo kuwapa
pole wafiwa hao kutokana na kuwapoteza ndugu na jamaa zao wakati wa tetemeko hilo
lililotokea Septemba 10, mwaka huu.
Katika kuwahakikishia usalama na
utunzaji wa fedha walizopokea wafiwa hao, Mkuu wa mkoa huo amewaasa wasikuwa na
akaunti wafungue akaunti katika benki yeyote ili waweze kuziweka fedha hizo walizopokea
ili kuwahakikishia usalama badala ya kutembea nazo mkononi.
Wawakilishi wa familia
zilizopokea rambirambi hiyo ni pamoja na Vedasto Katto (Hamugembe), Geofrey
Gerald (Mafumbo), Alex Felix (Hamugembe), Orestus Aron (Hamugembe), Justa
Mkalisa Jonas (Hamugembe), Albert Tibangayuka (Barabara ya Sokoine), Sheikh
Mikidadi Abdallah (Hamugembe) na Maria Stella John (Hamugembe).
Wanafamilia wengine waliopokea
rambirambi ni Swidick Miyonga (Hamugembe), Jackson Evason (Rwamishenye), Jasson
Rugemalila (Rwome), Augustine Muhigi (Rwome), Edson S. Rwetabula (Kashenye),
Anitha Evalista (Omurushaka) na John Mulokozi Kahangwa (Kanyigo-Kikukwe).
Aidha, mkuu huyo wa mkoa ameishukuru
Kampuni ya simu ya mkononi ya Halotel kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika
kutoa rambirambi na kuwafuta machozi familia za marehemu hao na kuwahakikishia
kuwa Serikali inathamini mchango wao kwa jamii.
Akitoa neno la shukrani mara
baada ya kupokea rambirambi hiyo kwa niaba ya wafiwa wenzake, Mzee Vedasto Kato
kutoka mtaa wa Hamgembe Manispaa ya Bukoba ametoa shukrani kwa Serikali
inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona haja ya kuwashika mkono
baada ya kupoteza ndugu zao.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutujali
wafiwa tuliopoteza ndugu zetu wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea katika
mkoa wetu mwezi huu na kutuonea huruma katika kipindi hiki kigumu
kilichotuachia majonzi makubwa katika familia zetu” alisema mzee Vedasto.
Mzee Vedasto amesema kuwa hatua
iliyochukuliwa na Serikali katika kuwapa mkono wa pole imewapa faraja na ameiomba
Serikali kuendelea kuwajali wananchi wake kama ilivyokuwa kwao.
Tetemeko la ardhi lilitokea
mkoani Kagera mapema mwezi huu, limesababisha vifo ambapo wananchi 17
waliopoteza maisha yao, majeruhi 440 ambao walitibiwa katika vituo mbalimbali
vya afya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Pamoja na rambirambi hiyo, Serikali
pia iliwahudumia marehemu waliopoteza uhai wakati wa tukio hilo kwa kutoa
majeneza pamoja na usafiri wa kusafirisha miili ya marehemu hao kutoka Bukoba
mjini hadi kwenye maeneo ambayo familia zao walipo ambapo yalipofanyika maziko
ya wapendwa wao.
No comments:
Post a Comment