Sensei Mtshali akirekebisha mkanda wa Sensei Florence Kieti kutoka Mombasa, Kenya.
Sensei Mtshali (kulia) akitoa maelekezo.
Wakati
semina ya kimataifa ya Shotokan Karate imeingia katika siku ya tano leo
hii hapa kwenye ukumbi wa Don Bosco, Upanga jijini Dar es Salaam,
tunashuhudia ujio wa mwalimu mkongwe kabisa wa mchezo huo barani Afrika,
Edward Mtshali Sensei (7th Dan) kutoka nchini Afrika Kusini.
Sensei
Mtshali (68) amewasili nchini juzi usiku na kuanzia jana amekuwa
darasani akiwaonyesha makarateka wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini
uzoefu wake katika semina hii ambayo inawahusisha makarateka kutoka
Kenya, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Tanzania Bara na Zanzibar.
Sensei Mtshali ndiye ameshika darasa kwa leo ambapo zaidi ya makarate-ka 50 wanahudhuria.
Mbali ya Mtshali, lakini pia Mkufunzi Mkuu wa JKA/WF-Kenya, David Mulwa Sensei naye ametua nchini kuhudhuria semina hiyo.
Hii
siyo mara ya kwanza kwa walimu hao wawili kuja nchini, kwani wamekuwa
chachu kubwa ya maendeleo ya karate kutokana na msaada wao mkubwa kwa
vijana wa Tanzania.
Wasifu wake
Edward Mtshali Sensei,
au Ed kama anavyoitwa kila mahali, ndiye Mbantu wa kwanza kupewa hadhi
ya kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini wa
Japanese Karate Association (JKA) World Federation (WF). Pia ni Mbantu
wa kwanza kupewa hadhi ya rangi za taifa la Afrika Kusini mara tano
mfululizo. Mara ya kwanza ilikuwa alipocheza dhidi ya timu ya Uingereza
mwaka 1977. Timu ya taifa ya Afrika Kusini ilikuwa ikichaguliwa kutoka
katika timu nne tofauti, Timu ya Wahindi, Machotara, Wabantu na Makaburu
(maarufu Springbok) na Sensei Ed alikuwa karate-ka pekee Mbantu
kuchaguliwa.
Mwaka 1978, alikuwa mmoja wa wachezaji wa timu rasmi ya
Springbok ambayo ilishindana na timu za Ujerumani na Marekani, ambapo
timu ya Marekani ilikuwa na mchezaji, ambaye kwa sasa ni maarufu katika
filamu, Billy Blanks.
Ilikuwa ni katika kipindi hiki ambapo alianza
kucheza akiwa chini ya Sensei Stan, muasisi na Mkufunzi Mkuu wa South
Africa JKA, akiwa pamoja na wanandugu wakungwe wa Geyer.
Mwaka
uliofuata alikuwemo kwenye timu ya taifa ya Afrika Kusini ambayo
ilikwenda Marekani. Katika mashindano hayo, alitwaa tuzo maalum kama
mshiriki wa muda mrefu.
Mwaka 2006, katika mashindano ya ShotoCup
nchini Australia, Sensei Ed alikuwa Mbantu wa kwanza kutwaa Dan ya 7
akisimamiwa na timu ya majaji Wajapani wote kutoka makao makuu ya
Japanese Karate Association (JKA) World Federation (WF). Mpaka sasa yeye
ni Mbantu pekee barani Afrika kuwa na rank hiyo ndani ya JKA. Kwa sasa
Sensei Ed ndiye anayesimamia JKA/WF katika nchi 26 za Afrika Kusini mwa
Jangwa la Sahara.
Alizaliwa Aprili 26, 1948 na mwaka huu ametimiza
miaka 68, lakini ukimtazama unaweza kudhani ana miaka 45 kwa jinsi
alivyo mkakamavu. Amekuwa akicheza karate kwa miaka 50 sasa na
amekumbana na changamoto nyingi.
Mwaka 1968, mkufunzi wake wa kwanza
alikuwa Samuel Maimane, ambaye alikuwa na mkanda wa bluu ambapo
walikuwa wakicheza Shotokan karate. Sababu ya kusema kwamba alifahamu
hiyo ni Shotokan ni kwa vile kitabu walichokuwa wanakitumia kilikuwa
kile kilichoandikwa na Sensei Nishiyama. Ilikuwa ni vigumu wakati huo
kwa Wabantu kupata ujuzi na kupata waalimu wa kuwapandisha madaraja.
Huyo ndiye Sensei Mtshali, japo kwa ufupi tu.
Imeandaliwa na mtandao wa www.maendeleovijijini.blogspot.com
No comments:
Post a Comment