Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday, 16 March 2015

MAPYA YAFICHUKA MABEHEWA FEKI TRL

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe

Mapya yanazidi kuibuliwa juu ya sakata linaloiandama Kampuni ya Reli Limited (TRL) ya uingizaji mabehewa feki nchini, sasa ikifahamika kuwa hata Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), haikushirikishwa kwenye manunuzi hayo.
 
Kufichuka kwa ukweli huo, ndiko sasa kunaongeza hali ya wasiwasi ndani ya TRL na kuna uwezekano mkubwa sakata hilo litaibua mjadala katika mkutano wa 19 wa Bunge unaotarajiwa kuanza kesho mjini Dodoma.
 
 Ukweli huo uliwekwa wazi mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luaga Mpina, wakati wa kikao cha kamati yake na PPRA.
 
 Mpina alitoboa siri hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao baina ya kamati yake na PPRA.
 Alisema kamati yake iliwahoji PPRA kuhusu ushiriki wao kwenye ununuzi wa mabehewa hayo na kubaini kuwa mamlaka hiyo haikushirikishwa.
 
 “Tunashangaa kwamba hata PPRA hawakushirikishwa kwenye mchakato wa ununuzi wa mabehewa hayo. Hadi sasa ninapozungumza hawajawahi kuitwa kushuhudia mabehewa 150 yaliyobainika kuwa ni feki,” alisema Mpina.
 
 Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa, alisema hali hiyo inaonyesha mambo kufanywa kinyume cha taratibu katika mchakato mzima wa ununuzi wa mabehewa hayo, hali aliyosema imechangia kuingiza hasara serikali kwa kununua mabehewa feki.
 
 Ili kulishughulikia suala hilo sawa sawa, mbunge huyo alisema kamati yake inatarajia kukutana na uongozi wa PPRA chini ya mkurugenzi wake, Laurent Shirima Ijumaa wiki hii mjini Dodoma, kwa ajili ya kupata taarifa zaidi kuhusu ununuzi wa mabehewa hayo feki.
 
 Wakati huo huo, kamati iliyoudwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, imewasilisha taarifa ya uchunguzi wake kwa Bodi ya Wakurugenzi wa TRL kama walivyoagizwa na Waziri wa sasa wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ambaye anatarajiwa kukabidhiwa ripoti hiyo leo.
 
 Mabehewa hayo yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan Engineering and Industrial Limited ya India ikishirikiana na kampuni moja nchini inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja jina kwa sasa linasitiriwa. Mfanyabiashara huyo amekuwa akijihusisha na biashara nyingi za kulaghai mashirika ya umma na kujipatia ukwasi wa kupindukia.
 
 Waziri Sitta ambaye alichukua hatua ya kusimamisha uingizaji wa mabehewa mengine 124 yaliyosalia hadi hapo atakapopata taarifa ya uchunguzi ya mabehewa ya awali ambayo yamebainika kuwa feki, amekwisha kuweka wazi kwamba hatakuwa na simile kwa yeyote atakayehusika na kadhia hiyo hata kama ana madaraka makubwa kiasi gani.
 
 Mabehewa hayo yaligundulika kuwa mabovu baada ya kufanyiwa majaribio baadhi yalianguka kwa kukosa ‘stability’ yakiwa relini.
 
 Habari za ndani ya TRL zinasema kuwa, mabehewa hayo yaliyopokelewa na Dk. Mwakyembe Julai 24, mwaka jana, hayakupitiwa na jopo la mafundi wa TRL ili kuthibitisha ubora wake. 
 
 Ingawa Dk. Mwakyembe amekuwa akijiweka mbali na sakata hilo na kueleza kuwa alijua tatizo mapema ndiyo maana akaagiza kamati ichunguze, hataweka wazi ilikuwaje kwenda kuyapokea kwa mbwembwe wakati hakuwa na ripoti kamili ya ubora wake na ufuataji wa sheria ya manunuzi katika kutoa kandarasi hiyo kwa kampuni ya India kwa kushirikiana na mfanyabiashara huyo.
 
 Dk. Mwakyembe aliyapokea mabehewa hayo kwa bashasha, huku akieleza kuwa ununuzi wake ni utekelezaji wa mpango wa serikali wa ‘Matokeo Makubwa Sasa (BRN)”, ambao umelenga kuhakikisha reli inahimili usafirishaji wa abiria na mizigo nchini.
 Menejimenti ya TRL imetajwa kwa nyakati mbalimbali na vyanzo vyetu ndani ya TRL kuwa  na mikono katika kashfa hiyo.  
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment