Na Julius Mathias, Mwananchi
Dar es Salaam. Profesa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Peter Kopoka amebanwa na uongozi wa chuo hicho kutokana na kushiriki maandamano ya kwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kumshawishi achukue fomu ya kugombea urais.
Profesa huyo akiwa na wahadhiri pamoja na watu wengine walioelezwa kuwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma walifanya maandamano hayo Machi 22, mwaka huu.
Kutokana na tukio hilo, uongozi wa Udom umemtaka ajieleze kwa nini ameshiriki harakati hizo za kisiasa huku akijua kuwa ni mtumishi wa umma anayepaswa kuwahudumia watu wenye itikadi tofauti.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula alisema kwa kuwa jambo hilo lilionekana kukiwakilisha chuo katika masuala ya siasa, uongozi ulilazimika kumhoji mhadhiri huyo.
“Ametuandikia barua ya kujieleza na kubainisha kuwa alikwenda yeye binafsi na siyo kama mwakilishi wa chuo. Lakini mambo haya ni magumu sana kutofautisha. Mimi kwa mfano, siwezi kwenda sehemu halafu nikasema sikwenda kama mkuu wa chuo kwa sababu siwezi kutofautisha hilo. Lakini tumechukua maelezo yake na tumeyahifadhi,” alisema Profesa Kikula.
Kuhusu wanafunzi wanaodaiwa kushiriki harakati hizo kutoka chuoni hapo, alisema hakuna wanachoweza kufanya kwa sababu mbili kubwa. Kwanza, ni vigumu kuwatambua waliofanya hivyo na pili walifanya hivyo nje ya chuo, jambo linalowezekana.
“Maandamano hayo yalifanyika mtaani. Huko walikuwa wanavunja sheria za nchi, kama hayakufuata sheria, Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kudhibiti au kuruhusu jambo kama hilo kufanyika,” alisema. Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Profesa Kopoka alikiri kuandika barua hiyo na kueleza kuwa alichokifanya ni kutekeleza haki yake ya uraia ya ushiriki katika utawala wa haki na demokrasia nchini.
“Nimefanya hivyo. Nilikwenda kutokana na imani yangu kutokana na vile ninavyomfahamu Lowassa. Sikuwa peke yangu. Ni kama ilivyoripotiwa, walikuwapo pia wahadhiri kutoka vyuo vikuu vya Mtakatifu Yohana (St. John) na Mipango,” alisema Profesa Kopoka.
Alisema pamoja na kufanya hivyo, suala hilo halijaathiri utendaji wake wala mkataba wake wa ajira.
Mfululizo wa kukanusha
Siku nne baada ya maandamano hayo, viongozi wa Serikali za wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali walijitokeza na kukanusha habari hiyo kwa maelezo kuwa waliofanya hivyo hawakuwa wanafunzi na wala suala hilo halikupata baraka kutoka vyuoni.
Katika taarifa ya pamoja ya marais wa serikali za vyuo vikuu hivyo vilivyomo mkoani humo iliyosomwa na Rais wa St. John, Daniel Daniel imepinga kushiriki kwao na kubainisha kuwa waliofanya hivyo ni watu wa mtaani.
“Tunapenda kukanusha kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma kwa ujumla wetu hatukuhusika na jambo lile na kama viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya mkoa huu wa Dodoma, tunapinga na kulaani kitendo cha watu wachache kwenda kutuingiza sisi wanafunzi wa vyuo vikuu katika jambo ambalo halituhusu na wala siyo lililotuleta hapa Dodoma,” alisema Daniel.
Walisema watu waliokusanyika nyumbani kwa Lowassa walijumuisha wamachinga, wenyeviti wa jumuiya za wazazi pamoja na wanafunzi wachache kutoka vyuoni ambao walifanya hivyo kutoka mtaani yalikoanzia maandamano hayo.
Walieleza kuwa: “Idadi ya watu waliojikusanya nyumbani kwa Lowassa haizidi 230. Idadi ya wanafunzi waliokuwapo kwenye tukio lile hawazidi 150. Idadi hii ni sawa na asilimia 0.4 ya wanafunzi wote wanaosoma vyuo vikuu vya Dodoma.”
Wanafunzi hao ni kundi la pili kupinga ushiriki wake katika maandamano yaliyoripotiwa kufanya hivyo baada ya Sheikh wa Wilaya ya Bagamoyo, Abdulkadir Mohammed Ramiya kukanusha taarifa ya masheikh 50 kutoka wilayani mwake kwenda kwa Lowassa kumuomba kuchukua fomu ya urais pia. Mapema wiki hii, iliripotiwa kuwa masheikh 50 kutoka Bagamoyo walifunga safari mpaka Area D, Dodoma yalipo makazi ya Lowassa na kumtaka agombee urais na kisha kumkabidhi kiasi cha Sh700,000 za kuchukulia fomu husika.
Siku chache baadaye, Sheikh Ramiya alikanusha taarifa hizo na kueleza kuwa kati ya masheikh 50 waliokwenda huko hapakuwa na hata mmoja kutoka wilayani mwake.
Makundi ya kushawishi
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na makundi mbalimbali yanayoripotiwa kwenda Dodoma na kumshawishi Lowassa kugombea nafasi hiyo ikiwa ni kutekeleza kauli aliyowahi kuitoa Rais Jakaya Kikwete katika kilele cha sherehe za kuanzishwa kwa CCM mwaka huu kuwa wanaostahili kugombea wapo kimya na wanahitaji kuambiwa wafanye hivyo.
Baadhi ya makundi yaliyofanya ushawishi huo mpaka sasa, ukiacha jumuiya ya masheikh kutoka Bagamoyo na wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma, ni pamoja na Jumuiya ya Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste na umoja wa madereva bodaboda kutoka Mbarali mkoani Mbeya.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda wa Polisi Dodoma, David Misime alisema “Sijaelewa unauliza nini,” kisha kutaka simu.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment