Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe
Na Salome Kitomary
Kiongozi
Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (pichani) na Katibu Mkuu,
Samson Mwigamba, wameweka hadharani mali, maslahi na madeni, ambazo
zitawekwa wazi kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na tovuti
ya chama ili wananchi wasome.
Akihutubia mamia ya wananchi wakati wa uzinduzi wa chama hicho,
Zitto alianza kwa kuweka hadharani mali zake mbele ya mwanasheria wa
chama na kudai kwa undani zitawekwa kwenye mtandao ili kila mwananchi
ajisomee.
Kabla ya kusaini fomu hiyo, Zitto alisema Watanzania
wananyanyapaliwa na kupuuzwa huku uchumi kushikiliwa na wachache na
kwamba kwa sasa ni muda wa uchumi shirikishi kwa wananchi kuwawajibisha
viongozi wao.
Alisema wananchi waikatae Katiba inayopendekezwa kwa kuwa
imeshindwa kuwa na mfumo wa kuwajibisha na uwajibikaji kwa viongozi wa
umma.
Alisema Tanzania inapoteza kiasi cha Sh. bilioni 490 kutokana na
ushuru wa forodha huku kiasi cha Sh. trilioni mbili kila mwaka kikipotea
kutokana na misamaha ya kodi, fedha ambazo zingetatua matatizo ya
watanzania.
Awali, Mwenyekiti wa chama hicho, Anastazia Mghwira, alisema nia ya
chama hicho ni kuhakikisha Taifa kwanza, sasa, leo na kesho ili
kurejesha heshima ya Mtanzania ya undugu na kujali.
Mghwira alisema ni mara ya kwanza kwa chama cha siasa kuongozwa na
mwanamke na kwamba chini ya uongozi wake watahakikisha tafsiri za
rasilimali za Taifa inaonekana katika maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Samson Mwigamba, alisema kwa kipindi
cha miezi saba chama hicho kimejiimarisha na kupata wenyeviti 13 wa
mitaa, vijiji 13, vitongoji 67 na wajumbe wa serikali za mitaa na vijiji
250, hivyo kushika nafasi ya tano kati ya vyama 22 vya siasa.
Mhasisi wa chama hicho, Prof. Kitila Mkumbo, alisema moja ya
matatizo ya vyama vingi vya siasa ni kuchanganya uongozi wa chama na
dola, na kwamba vyama vyenye akili kama ACT kinakuwa na kiongozi wa
chama na viongozi wengine.
Alisema ndani ya chama hicho cheo siyo jambo la msingi sana bali
muhimu ni majukumu na kwamba moja ya kazi kubwa ya kiongozi mkuu ni
kutangaza ilani ya chama na kuwasilisha taarifa kwa Mwenyekiti.
Alisema ndani ya chama hicho iwapo kiongozi atagombea nafasi ya
uongozi na kushindwa atakuwa akijieleza ndani ya kamati kuu na
akishindwa kutoa sababu za msingi atapigiwa kura ya kutokuwa na imani
naye.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment