Na Abdulla Ali na Rahma
Khamis, Maelezo-Zanzibar
Kuongezeka kwa biashara
ya vilevi (Baa) katika mji wa Zanzibar kunatokana na tamaa za wamiliki wa
maeneo kwa kuuza kiholela bila ya kujua lengo la mnunuzi na athari zinazoweza kujitokeza
katika jamii.
Haya yameelezwa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji
Omari Kheri katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji
wa Zanzibar wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Mhe. Jaku
Hashim Ayoub alipotaka kujua kuwa Serekali imewaambia nini wananchi wa
Jimbo la Kiembe Samaki kuhusiana na tatizo hilo.
Aidha amesema biashara
ya vileo nchini Zanzibar inaendeshwa kwa kufuata Sheria ya Vileo ya 1928, ambayo
ndiyo iliyoweka utaratibu wa ukataji wa leseni na adhabu kwa wanaokwenda kinyume
na taratibu za leseni hizo.
Amesema kila Mwaka kabla
ya kutolewa leseni mpya kwa vilabu vya vilevi (Baa) hutolewa matangazo ili wale
wenye pingamizi za kuwepo kwa Baa kupeleka pingamizi zao katika mamlaka ya
utoaji wa leseni na hatimaye hutakiwa kufika katika vikao vya majadiliano na
wajumbe wa mahakama ya vileo.
Hata hivyo Waziri huyo amesema pamoja na kuwepo Sheria hiyo
kwa muda mrefu na kufanya kazi hadi leo bila ya kua na matatizo makubwa, hivyo
niwazi kuwa inahitaji marekebisho ili iendane na hali halisi ya sasa.
Waziri Kheri ameeleza
kuwa Ofisi yake imewasiliana na Tume ya Kurekebisha Sheria ili kuifanyia
mapitio na kuipendekeza sheria mpya itakayowasilishwa barazani hapo kwa ajili
ya kujadiliwa na hatimae kuweza kutumika kama sheria iliyo kamili mara baada ya
kupitishwa na wajumbe wa Baraza hilo.
“Nashukuru Tume
imeshakamilisha kazi hiyo na kutupa Rasimu ya Sheria mpya baada ya kushauriana
na wahusika wengine na Ofisi yangu inaifanyia kazi na muda si mrefu Mswada wa
Sheria hiyo utaletwa katika Baraza lako tukufu.”Waziri amesema.
Akifafanua kuhusiana na
Baa amefahamisha kuwa Jimbo la Kiembe Samaki kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo Baa
kumi na moja (11) ambazo zote hizo zimepewa leseni kwa mujibu wa taratibu za
kisheria, na Ofisi hiyo haina taarifa za kuwepo kwa Baa ambazo hazina leseni na
zinazofanya kazi ndani ya Jimbo la hilo.
Ametanabahisha kuwa kwa
mujibu wa sheria hiyo adhabu ya kuendesha biashara hiyo bila ya leseni ni faini
au kifungo au vyote 2 kisichozidi miezi 12 na Mahakama imepewa uwezo wa
kisheria wa kufilisi vinywaji vyote vitakavyokutwa ndani ya Baa isiyo na
leseni.
Waziri Kheri amewataka wananchi pamoja na kuwaomba Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi kutumia utaratibu uliowekwa kisheria kwa ajili ya
kutoa malalamiko yao ili yapatiwe ufumbuzi kwa wakati na hatimae kuweza
kuondokana na kero ndogondogo zinzowakabili wananchi katika makaazi yao.
No comments:
Post a Comment