Mshambuliaji kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samata ameibuka
shujaa baada ya kuifungia bao Taifa Stars ikilazimishwa sare 1-1 na
Malawi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba, Mwanza jana.
Malawi ilianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa
kupata bao la kuongoza dakika ya tatu lililofungwa na Mihum Mphone
aliyemalizia mpira ulioshindwa kuokolewa na mabeki wa Taifa Stars baada
ya kona ya iliyopigwa na John Banda. Bao hilo liliwaondoa Stars mchezoni
kwani katika dakika 10 za mwanzo ilicheza bila ya malengo na kuwapa
nafasi kubwa Malawi kutalawa mchezo huo.
Dakika ya 14, Samata nusura aisawazishie Stars
baada ya kupiga shuti akiwa nje ya eneo la 18, lililopanguliwa na kipa
Donald Harawa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Thomas Ulimwengu alikosa bao dakika 22, baada ya
shuti lake kuokolewa na kipa Harawa katika uwanja huo uliojaa tope na
maji kutokana na mvua kubwa iliyoonyesha jijini Mwanza.
Malawi ilikwenda mapumziko ikiwa mbele 1-0, pamoja na kutawala sehemu kubwa mchezo hasa katika eneo la kiungo.
Taifa Stars ilirudi kipindi cha pili kwa nguvu
baada ya kocha Mart Nooij kuwapumzisha Haruna Chanongo, Amri Kiemba na
Ulimwengu na kuwaingiza Mrisho Ngassa, Abubakari Salum ‘Sure Boy’, na
John Bocco.
Mabadiliko hayo yaliifanya Stars kutawala katikati
ya uwanja na kuanza kufanya mashambulizi mengi langoni kwa Malawi
walioaamua kucheza kwa kujilinda.
Dakika ya 75 krosi ya Ngassa ilimkuta Samata
aliyepiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuisawazishia Stars
katika dakika 75, bao hilo liliamsha shangwe za mashabiki wa Tanzania
waliojitokeza uwanjani hapo.
Bocco naye nusura apate bao katika dakika 80, baada ya shuti lake kupaa juu kidogo ya lango la Malawi.
Kocha wa Stars, Nooij alisema Malawi ni timu nzuri
ina wachezaji bora, lakini wachezaji wake walifanya kosa kuruhusu
kufungwa bao la mapema.
Naye kocha wa Malawi, Chimuzi Yangi alisema mchezo
ulikuwa mgumu na wachezaji wake walicheza vizuri, ila kosa moja
walililolifanya limewaghalimu.
Kufuzu CHAN 2016
Taifa Stars itaanza kampeni yake ya kusaka kufuzu kwa fainali za
Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) Rwanda 2016 hapo Juni
19-21.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Afrikca (CAF) ratiba ya mashindano hayo itapangwa Aprili 5, jijini Cairo, Misri.
Mashindano ya CHAN yatashirikisha timu 42, ambazo zitapangwa kushindana kutokana na kanda sita za nchi wanachama wa CAF.
Mechi za mtoano zitaanza kuanzia Juni 19-21
zitafanyika hadi Agosti 28-30 ambako zitapatikana timu 15,
zitakazoungana na wenyeji Rwanda tayari kwa fainali zitakazoanza Januari
16 hadi Februari 7, 2016.
Washindi wa fainali tatu zilizopita za CHAN, ni DR Congo (2009), Tunisia (2011) na Libya (2014).
CREDIT: MWANANCHI
Taifa Stars: Mwadini Ally, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Agrey
Morris, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Erasto Nyoni, Mwinyi Kazimoto, Amri
Kiemba, Thomas Ulimwengu/John Bocco (dk. 81), Mbwana Samata na Haroun
Chanongo/Mrisho Ngassa (dk. 59).
Malawi: Mcdonald Harawa, Joseph Kamwendo, John Lanjesi, Harry
Nyirenda, Limbikani Mzava, Chimango Kaira, Francis Mulimbika, John
Banda, Mucium Mhone, Peter Wadabwa na Essau Kanyenda. CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment