Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina.
Na Thobias Mwanakatwe
Dodoma: Mambo
magumu yameibuka katika suala la kujadili uanzishwaji wa Mahakama ya
Kadhi, baada ya kutokea malumbano makali na vurugu huku idadi kubwa ya
wabunge wakiitaka serikali kuuondoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi
usiwasilishwe bungeni.
Wabunge wengi walisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha mpasuko na kuvunjika kwa amani nchini.
Aidha, wamesema suala la Mahakama ya Kadhi linataka kufanywa kama
mtaji wa kisiasa kwa baadhi ya viongozi wanaotaka kuwania urais katika
uchaguzi mkuu mwaka huu ili kutafuta kura za Waislamu.
Mvutano huo uliibuka jana wakati wa semina ya wabunge kujadili
Muswada wa Sheria mbalimbali wa mwaka 2014 ambao ndani yake kuna
Muswada wa Mahakama ya Kadhi ambao umepangwa kuwasilishwa Aprili Mosi
mwaka huu siku ya kuahirisha mkutano wa 19 wa Bunge.
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina, alisema Kamati ya
Katiba Sheria na Utawala ilipowaita viongozi mbalimbali wa dini
kuzungumzia suala hilo Waislamu walitofautiana katika suala la uteuzi wa
Kadhi kufanywa na Mufti Mkuu wa Tanzania na wakataka waelewane kwanza
kabla ya suala hilo kupelekwa bungeni.
Alisema katika mkutano huo makundi 11 ambayo hayakubaliana na
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), walisema Muswada wa Mahakama
ya Kadhi uletwe bungeni baada ya kuridhiana kwa sababu hawakubaliani na
Bakwata ambalo kiongozi wake ni Mufti Mkuu wa Tanzania.
Walisema maaskofu walisema hawana tatizo na suala la Mahakama ya
Kadhi, lakini isiwe na muundo kama wa mahakama nyingine na kwamba mawazo
ya waasisi wa Taifa, hawakutaka serikali iwe na dini na ndiyo maana
hawakuruhusu mahakama hiyo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Kassimu, alihoji ni kwanini
Mahakama ya Kadhi inataka kuundwa na kupewa jukumu Mufti ambaye anatoka
Bakwata ambayo ni taasisi binafsi na imesajiliwa na Mamlaka ya Rita.
“Bakwata ni taasisi kama zilivyo taasisi nyingine, haikubaliki,
Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi suala la Mahakama ya Kadhi ili Waislamu
wampigie kura kwa sababu anataka kugombea urais mwaka huu,” alisema.
Rukia alisema ni marufuku serikali kuwalazimisha Waislamu kuwa
chini ya Bakwata na kwamba Waziri Mkuu, Pinda anafahamu kwa kina
suluhisho na mvutano huo wa Mahakama ya Kadhi.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR), Moses Machali, alisema suala la
kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kuingizwa katika mfumo wa mahakama
za kawaida inajichanganya na ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Alisema mwaka 2011 Rais Jakaya Kikwete wakati anazindua msikiti wa
Gadaf alisema suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi lisihusishwe na
serikali kwa sababu wapo watu wengine ambao kila mmoja ana imani yake.
Alisema hatua ya serikali kutaka kuuleta muswada huo wakati bado
Waislamu wenyewe hawaelewani ni kuwakosea Waislamu na kwamba inawezekana
Waziri alilizungumzia suala hili sababu ya malengo yake ya urais.
Machali alisema kama muswada huu utapelekwa Bungeni itatoa fursa
kwa madhehebu mbalimbali kila moja kuanzisha mahakama yake hali
itakayoleta machafuko nchini kwa kuwa nchi itakuwa katika mfumo wa
mahakama za dini.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema muswada
unapendekeza kutambua kitu ambacho mfumo wa sheria za nchi hauna na
kwamba uongo unaotumiwa na serikali ndiyo unafanya watu wawe na hofu.
Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM), Ally Kessy, alisema: “Katika nguzo
tano za Kiislamu Mahakama ya Kadhi haipo, nguzo sita za imani pia haipo,
sasa inakuwaje wanadai kitu ambacho hakitambuliki katika nguzo za
kiislamu.”
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, alisema muswada wa Mahakama
ya Kadhi urudishwe ukaboreshwe badala ya kuharakisha kuupeleka bungeni
wakati bado una utata hata kwa waislamu wenyewe.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambali Nyangwine, alisema Muswada wa
Mahakama ya Kadhi usimamishwe ukafanyiwe utafiti kwanza kwa sababu
ndani ya Waislamu wenyewe hawaelewani.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema Wabunge
wasipokuwa makini na suala la Mahakama ya Kadhi, Bunge litaingia katika
historia kuvunjika kwa amani.
Selasini alisema serikali iachane na kutoa ‘jini’ lililofungiwa na
waasisi Mwalimu Nyerere na Karume na kwamba tukifanya mchezo nchi
itabaki katika vipande vipande.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa, alisema jambo
hili litaligawa Taifa na kwamba waasisi hawakuwa wajinga walipokataa
serikali isiwe na dini.
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa, alisema nchi
inaelekea kubaya kwani msingi wa kuleta Mahakama ya Kadhi ni kutaka
kuwachota Waislamu kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Serikali kama imedhamiria kuleta Mahakama ya Kadhi ilete katika
utaratibu mzuri, lakini kwa huu utaratibu ni unafiki na mwenyezi Mungu
hapendi unafiki, tusiwahadae Waislamu,” alisema.
Khalifa alisema kwa hali ilivyo muswada huo haujaiva na kwamba usiletwe bungeni hadi hapo serikali itakapojipanga vizuri.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alisema suala
la imani siyo la chama cha kisiasa kwani suala la Mahakama ya Kadhi
litaipeleka nchi kubaya na inawezekana ikawa ndio mwisho wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
“Mnataka kutuvurugia nchi sababu ya kutafuta kura za Waislamu, kwa
hili Waziri Mkuu umechemka sana, nalisema hili kwa sababu wewe Waziri
Mkuu ndiye uliyeahidi kuleta bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi,”
alisema.
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jafo, alisema yasifanyike masikhala mswaada huyo uwasilishwe bungeni.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Mchungaji Lackison Mwanjale,
alisema serikali ikajipange upya katika suala la Mahakama ya Kadhi kabla
ya kuuleta bungeni muswada kwani bado suala hilo halieleweki kwa jamii.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Martaza Mangungu, alisema
hakubaliani na suala la Mufti kupewa jukumu la kuchagua Kadhi Mkuu
wakati Waislamu wengi hawakubaliani na Bakwata ambayo inaongozwa na
Mufti.
Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa, alisema muswada wa
Mahakama ya Kadhi wapelekewe wahusika kabla ya kuletwa bungeni ili
wajadiliane na kukubaliana mambo ya msingi wanayoona yatawafaa katika
uanzishwaji wa mahakama hayo.
Mbunge wa Igunga (CCM), Dk. Peter Kafumu, alisema serikali
imeshindwa kusimamia vizuri suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi
kwa kushindwa kuwaelimisha wananchi jambo hilo.
Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahaya Kassim Issa, alisema Waislamu
wanataka Mahakama hiyo kwa kuwa wanakosa haki hivyo serikali iruhusu
kuanzishwa kwake.
PINDA: TUTAFAKARI UPYA
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akihitimisha mjadala huo alisema
kulingana na maoni yaliyotolewa na Wabunge ameelewa kwamba bado hakuna
maelewano miongoni mwa Waislamu wenyewe na pia hakuna uelewa wa jamii
kuhusu suala hilo.
Alisema mambo yaliyowasilishwa kuhusiana na muswada huo ni maamuzi
ya Bunge Maalum la Katiba na siyo yake, bali anabebeshwa msalaba tu kwa
sababu alikuwa anaiwakilisha serikali.
Pinda alisema kutokana na hali hiyo, serikali itakaa kushauriana
tena na Spika pamoja na Rais waone wafanye nini katika jambo hilo.
VIJEMBE NA MATUSI
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, wakati akichangia
hoja hiyo alishindwa kuvumulia baada ya baadhi ya wabunge kuingilia
mchango wake kwa kumzomea na kusema maneno yaliyomuudhi na kuamua
kuwatolewa maneno ya kuudhi (matusi).
Mbunge wa Fuoni (CCM), Said Mussa Zubeir, aliwaita baadhi ya
wabunge walikuwa wakimzomea wakati akizungumza kuwa ni ‘wapumbavu’.
Wakati wa majadiliano hayo ilipofika saa 8:17 wakati Mbunge wa
Kisarawe, Jafo akiendelea kuchangia kulitokea vurugu ambazo nusura
wabunge wapigane huku baadhi yao wakiamua kutoka ukumbini.
Kutokana na kutokuwapo hali ya utulivu ukumbini, baadhi ya askari
pamoja na maofisa usalama waliokuwapo nje, walilazimika kuingia ndani
kuhakikisha amani haivunjiki.
Spika wa Bunge, Anna Makinda, alituliza vurugu ukumbini kwa kuwataka wabunge wawe wavumilivu wakati wenzao wakichangia.
Katika majadiliano wabunge zaidi 30 walichangia na zaidi ya 20
walikataa muswada wa Mahakama ya Kadhi usiwasilishwe Bungeni siku ya
Jumatano wiki hii.
Kabla ya kuanza majadiliano, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia,
alitoa hoja kwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Katiba, Sheria na
Utawala, William Ngeleja, kwamba wakati wa majadiliano waandishi wa
habari wasiwepo ukumbini kwa kile alichoeleza ni unyeti wa jambo hilo.
Hata hivyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Kessy, alisema kama
waandishi wataondolewa ukumbini naye atalazimika kuondoka huku
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, akisema hakuna sababu ya
kuwaondoa waandishi kwa sababu jambo linalojadiliwa wananchi wanataka
kulifahamu kupitia vyombo vya habari. Masaju akichangia wakati wa kujibu
hoja za wabunge, alisema suala la mahakama ya kadhi halina tatizo wala
halivunji katiba kama ilivyoelezwa na baadhi ya wabunge na kuwataka
wabunge wamuheshimu wakati ana-zungumza.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment