Edward Lowassa
Na Moshi Lusonzo
Utafiti
uliofanywa na Taasisi ya Positive Thinkers Tanzania (PTT), umeonyesha
kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anaongoza kati ya wanaotajwa
kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Utafiti huo pia unamuweka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa katika nafasi ya pili.
Matokeo ya utafiti huo yamewapa nafasi za juu wanasiasa hao baada
ya utafiti wa Shirika lisilo lwa kiserikali la Twaweza mwaka jana kumpa
Lowassa nafasi ya kwanza na Dk. Slaa nafasi ya tatu.
Utafiti wa PTT yenye makao makuu jijini Dar es Salaam, matokeo yake
yaliyotangazwa jana yanaonyesha kuwa Lowassa alipata kura 752 kati ya
3,298 zilizopigwa.
Dk. Slaa alipata kura 644 na Naibu wa Fedha, Mwigulu Nchemba 350.
Akitangaza ripoti ya utafiti huo jijini Dar es Salaam, Rais wa
Taasisi hiyo, Tibatizibwa Gulayi, alisema ulifanywa katika mikoa 13 kwa
kuwauliza wananchi kwa njia ya madodoso kisha taarifa zake kuingizwa
katika mfumo wa Elektroniki unaojulikana kama Fast web application
system (FWAS).
Alisema kuwa utafiti huo ulianza Februari, mwaka huu na kumalizika
mwanzoni mwa Machi, mwaka huu na ulihusisha majina wanasiasa 15
wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.
Gulayi alisema wanasiasa wengine waliotajwa na kura zao kwenye
mabano ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba
(294); Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (227); Kiongozi Mkuu wa ACT –
Tanzania, Zitto Kabwe (224); Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe (197); Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (107) na
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta (72).
Wengine ni Naibu waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba (54); Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum),
Profesa Mark Mwandosya (40); Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
(34) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi
(31).
Waliofuatia ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira (16) na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye (10).
Watu ambao walisema hawana mgombea walikuwa 79 wakati waliosema mgombea yeyote atakayegombea ni sawa walikuwa 167.
Katika utafiti huo makundi mbalimbali ya watu wenye umri kuanzia
miaka 18 walihojiwa. Makundi hayo yanahusisha wanafunzi wa shule za
msingi, sekondari, vyuo vikuu, wanazuoni na wananchi wa kawaida.
Gulayi alitaja mikoa iliyohusika kwenye utafiti huo kuwa ni Dar es
Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Tanga, Lindi, Dodoma, Pwani,
Iringa, Kilimanjaro, Shinyanga na Morogoro.
“Watu waliokwenda katika mikoa hiyo walitakiwa kuwahoji wananchi
nani anaweza kutuongoza kwa kuangalia uwezo wa muhusika katika utendaji
wake kwa vitendo, kupambana na ufisadi na Rushwa,” alisema Gulayi.
Hata hivyo, alisema utafiti huo ambao haukuegemea upande wowote wa
kisiasa, ulifanywa kutokana na hamasa za wananchi kutaka kujua hali ya
mtazamo, vigezo na matarajio ya watu katika kumchagua kiongozi wao
katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Alisisitiza kwamba utafiti huo umevunja dhana ya wananchi na
wanasiasa wengi wanaodhani kuwa viongozi wa kisiasa wanategemea idadi ya
wanachama na watu wenye mlengo wa itikadi unaofanana.
Lakini alisema kuwa watu walipiga kura katika utafiti huo bila kujali mtu ana itikadi ya chama gani.
“Wananchi wameanza kupata mwanga na weledi katika kufanya maamuzi
chanya katika kuwachagua viongozi wanaowahitaji,” alisema Gulayi.
Akizungumzia namna utafiti huo ulivyofanyika, Mtafiti na mtaalamu
wa Kompyuta, Facili Boniface, alisema ulichukua muda mfupi baada ya
kutumia mfumo wa FWAS ambao matokeo yake yanapatikana haraka.
Alisema mfumo huo ambao unaweza pia kutumiwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) katika upigaji kura unatoa matokeo ya uhakika bila
kuchakachuliwa.
Utafiti huo ni wa pili kufanyika nchini ambao unaonyesha kuwa
Lowassa anaongoza katika kinyng’anyiro cha urais. Katika utafiti
uliofanywa na Twaweza na matokeo yake kutangazwa Novemba 13, mwaka jana,
ulimtaja Waziri Mkuu Mizengo Pinda kushika nafasi ya pili kwa kupata
asilimia 12 na Dk. Slaa akiibuka watatu kwa asilimia 11.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment