Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa mkandarasi anayejenga nyumba za NHC (Town Houses) katika eneo la Jangwani, Manispaa ya Sumbawanga. Kulia kwake ni Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Sebastian Katepa, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ntendo. (Picha zote na brotherdanny5.blogspot.com).
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu (wa tatu kutoka kulia) akifafanua jambo kwa Waziri Lukuvi kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akimsikiliza mkandarasi anayejenga nyumba za NHC Sumbawanga mjini. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, na anayemfuatia ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya, alishindwa kujizuia na kwenda kushiriki ngoma ya Vingwengwe ya kabila la Wafipa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la nyumba za gharama nafuu za NHC leo hii. Hapa anaonekana akiwa amembeba mwanasesere.
Diwani wa Kata ya Katandala, Mhe. Kisabwite (kushoto), anaonekana akifuatilia kwa makini shughuli hiyo.
Waziri Lukuvi akiteta jambo la Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya.
Na Daniel Mbega, Sumbawanga
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Vangimembe Lukuvi, amewataka wananchi kununua nyumba za gharama nafuu
zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) badala ya kujenga wenyewe,
kwani gharama ni kubwa.
Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa
nyumba za makazi Jangwani katika Manispaa ya Sumbawanga leo hii, Mhe. Lukuvi amesema
nyumba zinazojengwa na NHC ni za gharama nafuu na zenye ubora, hivyo ni vyema
kila mwananchi akanunua nyumba hizo kuliko kujenga kwa kuwa zinaweza kuchukua
muda mrefu, kutumia gharama kubwa na ubora hafifu.
“Hizi nyumba, ambazo zinajengwa nchi nzima, ziko wazi
kununuliwa na kila mwananchi, njooni mnunue kwa kuwa mkijenga ninyi wenyewe
gharama yake ni kubwa zaidi na haziwezi kukamilika kwa wakati,” alisema na
kuongeza kwamba, heshima ya mtu, mbali ya kazi na kipato, ni nyumba bora.
Lukuvi amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella
Manyanya, kwa kutenga maeneo kwa ajili ya miradi ya NHC ya nyumba za gharama nafuu
huku akisisitiza kwamba ni vyema maeneo hayo yawe na watu, kwani shirika hilo
linafanya biashara ili kuongeza pato la taifa.
Amezitaka halmashauri zote kutenga maeneo kwa miradi hiyo
ili kujenga nyumba za watumishi wao na wananchi kwa ujumla.
“Tengeni maeneo ili kujenga nyumba za watumishi wenu, lakini
hata wananchi wa kawaida wanaruhusiwa kununua nyumba hizi,” alisema.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Manyanya, alisema
kwamba serikali yake imetenga eneo la ekari 25 katika mji wa Matai kwa ajili ya
mradi wa nyumba hizo za NHC ambazo hazitalipiwa fidia.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, amesema mradi wa nyumba
(town houses) uliozinduliwa ulibuniwa na shirika hilo kwa lengo la kuwapa fursa
watu wa kipato cha kati katika miji mbalimbali kumiliki nyumba.
“Mradi huu ulianza Julai 2014 na utakamilika Julai 2015
ambao utakuwa na nyumba 10 za kuishi familia 20 na zina vyumba vitatu, jiko na
sebule, ambapo utagharimu Shs. 1,532, 872,000,” alisema Mchechu.
Alisema shirika lake lina miradi mbalimbali katika mikoa ya
Rukwa na Katavi ambapo limenunua pia ekari 21 wilayani Kalambo na linakamilisha
kulipia ekari tisa wilayani Nkasi kwa ajili ya kujenga nyumba za gharama nafuu.
“Katika Mkoa wa Katavi tumeshajenga nyumba za gharama nafuu
70 zilizogharimu Shs. 2,346,937,089 katika eneo la Ilembo, Mpanda na
tunaendelea kujenga nyumba 24 kwa gharama ya Shs. 1,212,467,364 za aina hiyo
mjini Inyonga katika wilaya mpya ya Mlele.
“Shirika pia linajenga jengo kubwa la kisasa mjini Mpanda
kwa ajili ya kufanyia shughuli za biashara kwa gharama ya Shs. 3,167,781,000,”
alisema.
No comments:
Post a Comment