Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Mohamed Aboud Mohamed
Na Abdulla Ali na Rahma
Khamis, Maelezo-Zanzibar
Wananchi wana haki ya
kuwauliza Wawakilishi wao kuhusiana na Fedha wanazozipatiwa kutoka Serikalini kwa
ajili ya maendeleo ya Majimbo yao.
Hayo ameyaeleza Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Mohamed Aboud Mohamed
wakati akijibu swali la mwakilishi wa nafasi za wanawake Mhe. Shadya Mohammed Suleiman
katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
alipotaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa wale wote walioshindwa
kuwasilisha ripoti zao za fedha za majimbo yao.
Amesema Wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi wanatakiwa kuwasilisha kwa wakati ripoti za matumizi ya fedha za
Majimbo yao wanazopatiwa na Serikali ili kuimarisha maendeleo ya wananchi wao.
Aidha amekiri kuwa hadi
sasa Majimbo mengi bado hayajafanya marejesho ya matumizi ya fedha za mfuko wa Mwaka
wa fedha 2013/2014.
“Hata hivyo napenda
kutoa pongezi zangu za dhati kwa waheshimiwa wawakilishi wa majimbo 3 ambayo ni
Mtoni, Donge na Chambani pamoja na Kamati zao kwa kufanya marejesho kwa Mwaka 2013/2014
kwa wakati”, ameeleza Waziri Mohamed.
Amesema kuwa Serikali kupitia
Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais inawataka waheshimiwa kutekeleza matakwa ya Sheria
ili lengo lililokusudiwa kufikiwa kwa nia ya kuwaletea maendeleo wananchi
katika maeneo yao.
Vilevile Waziri huyo
amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia njema kwa wananchi wake na
ndio maana wawakilishi wao wa majimbo wanapewa kipaombele cha kupatiwa fedha za
Mfuko wa Jimbo ili ziwasaidie katika matatizo yao madogomadogo lakini kwa
masikitiko makubwa wawakilishi hao wanashindwa kuwasilisha ripoti zao za fedha
hizo jambo linalopelekea kurejesha nyuma maendeleo ya wananchi na Taifa kwa
ujumla.
Hata hivyo amefahamisha
kuwa serikali imejiwekea kuleta maendeleo katika majimbo yake yote bila ya
kuangalia kuwa majimbo hayo yanaongozwa na vyama pinzani au chama tawala.
No comments:
Post a Comment