Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Na Restuta James
Wakati wadau wa habari wakimwomba Spika wa Bunge, Anne Makinda (pichani), atumie busara kuishauri serikali iwasilishe miswada miwili ya habari ya mwaka 2015, wa Haki ya Kupata Taarifa na ule wa Huduma za Vyombo vya Habari kwa kawaida, Spika Makinda amesema ombi hilo amelipeleka kwenye kamati husika ya Katiba, Sheria na Utawala.
Aidha, Spika Makinda amesema wadau wowote wenye maoni kuhusu miswada hiyo waiwasilishwe kwenye Kamati hiyo ya Bunge.
Spika Makinda aliyasema hayo kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa
baada ya NIPASHE kutaka kujua kama mapendekezo hayo ya wadau yanaweza
kusikilizwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, miswada hiyo itawasilishwa Jumanne ijayo chini ya hati ya dharura.
Kwa mujibu wa maombi hayo, wadau hao ambao wamejichimbia Dodoma
tangu Jumamosi iliyopita wamemuomba Spika kutumia madaraka yake kama
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi kuishauri serikali kuwasilisha miswada
hiyo katika utaratibu wa kawaida ili kutoa fursa kwa wananchi kutoa
maoni yao kabla ya kupitishwa kuwa sheria.
Barua pia imeandikwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ni
Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, ikimuomba naye aone umuhimu wa
wananchi kushiriki kutoa maoni katika miswada hiyo kabla ya kupitishwa
na Bunge kwenye mkutano wa 19 unaoendelea mjini Dodoma.
Naye Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe,
ameandikiwa barua na wadau hao wakimuomba atumie nafasi yake kama
msemaji mkuu wa kambi hiyo bungeni kuishauri serikali iwasilishe miswada
hiyo chini ya mfumo wa kawaida na siyo chini ya hati ya dharura kwani
unawanyima wananchi fursa ya kutoa maoni yao kwenye miswada hiyo kabla
ya kupitishwa na Bunge.
Tangu serikali iseme kuwa inakusudia kuwasilisha miswada hiyo chini
ya hati ya dharura, wadau wa habari wamekuwa wakiomba ibadili msimamo
kwani kufanya hivyo kutawanyima wananchi fursa ya kutoa maoni juu ya
miswada hiyo kabla ya kuwa sheria.
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, kwa niaba ya Mbowe, amesema amepokea barua ya wadau.
Alisema jana kuwa kwa niaba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni, ametambua na kukubali ombi hilo na Kambi Rasmi ya Upinzani
itatoa ushauri huo kwa Serikali na kusimamia utekelezaji wake.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment