Edward Lowassa
Sasa ni dhahiri kwamba ushawishi wa kumtaka Edward Lowassa, awanie urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umezidi kiasi cha makundi ya wanachama wa chama hicho kupigana vikumbo nyumbani kwake wilayani Monduli wakimtaka ajitokeze wakati ukifika.
Jana makundi hayo yalifika Monduli kwenye makazi ya Lowassa ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo, yakiwa na fedha walizosema ni kwa ajili ya kumpa ili akachukue fomu ya kuwania urais kupitia CCM wakati ukifika.
Kundi la kwanza lililopiga hodi nyumbani kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani mjini Monduli jana kumshawishi na kumkabidhi fedha za kuchukulia fomu, ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Arumeru.
Kundi hilo mbali ya kumshawishi Lowassa ajitose kwenye mbio za urais kwa sababu anatosha kwenye kiti cha urais, walimkabidhi mchango wa Sh. milioni moja za kuchukulia fomu ya urais kupitia CCM.
Akizungumza katika ghafla hiyo fupi nyumbani kwa Lowassa, John Ole Saitabau, ambaye ni mwenyekiti mstaafu wa halmashauri ya Meru, alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona Lowassa anatosha.
“Sisi tumekuja hapa kukushawishi uchukue fomu ya kuwania urais kupitia chama chetu, uwezo huo unao .... Tanzania inakuhitaji,” alisema.
Naye Mjumbe wa NEC, Mathias Manga, alisema zaidi ya asilimia 75 ya wajumbe wa NEC wanamshawishi Lowassa awanie urais.
Kundi la pili lililofika nyumbani kwa Lowassa jana ni la marafiki wa Lowassa Kanda ya Kaskazini, lililojumuisha zaidi ya watu 500 kutoka kada mbalimbali, wakiwamo walemavu wa macho, maalbino, ambao walimkabidhi Lowassa Sh. 2,567,600 za kuchukua fomu ya urais.
Makundi hayo kutoka mikoani yaliwasili jana nyumbani kwake, kijiji cha Ngarashi, wilaya ya Monduli, baada ya kufanya maandamano makubwa yaliyoanzia njia panda ya Monduli, wakiimba nyimbo za matumaini kwamba ‘Wewe ni tumaini la walio wengi Tanzania, maamuzi na matumaini mapya, Watanzania wako nyuma yako’.
Makundi hayo yaliyoongozwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Matemu, Mratibu wa Marafiki wa Lowasa Kanda ya Kaskazini, Noel Nnko, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkoa wa Arusha, Robnson Meitinyiku, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, Fred Mushi, Askofu wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, Christoher Madilu ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na Abdalah Sadick kutoka mkoa wa Manyara.
Katika risala iliyosomwa na Protas Soka, kundi hilo linalojumuisha vijana kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, walisema Watanzania wanamuhitaji Lowassa.
“Kwa lugha nyingine Mheshimiwa Lowassa sasa tunakuomba utangaze nia ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2015, wewe ni tumaini la walio wengi Tanzania,” alisema.
Kundi hilo pia lilipaza sauti kwa kulaalani vitendo vya mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na kwamba watasimama kidete kuhakikisha ukatili huo una tokomezwa.
Mbali na pilikapilika za jana nyumbani kwa Lowassa, Jumamosi iliyopita (juzi) uongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma) ulimtembelea Lowassa nyumbani Monduli, nao walimkabidhi Sh. milioni moja za kuchukulia fomu kuwania urais kupitia CCM.
Mwenyekiti wa Shiuma, Matondo Masanja, akisoma risala yao kwa Lowassa, alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kumuona ndiye mtu sahihi kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
“Tumejiridhisha juu ya uongozi wako ndani ya chama chako na katika serikali, utumishi wako uliyotukuka, uwajibikaji na uzalendo wako hususan katika kuwakomboa Watanzania na kuondoa umasikini,” alisema.
Pamoja na fedha hizo, pia walimkabidhi kadi ya uanachama wa Shiuma, wakisema Lowassa ameonyesha kuwa ni mwenzao.
Viongozi wa shirika hilo ambalo makao yake yako Mwanza waliongozana na wenyeviti wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM) kata za wilaya za Nyamagana, mkoani Mwanza.
Wenyeviti hao nao pia walimtaka Lowassa atangaze nia. Walisema Lowassa ndiyo tegemeo la vijana wanaokabiliwa na tatizo kubwa la ajira.
“Umekuwa huchoki kupigia kelele tatizo la ajira kwa vijana ... tunakuomba kuyakubalia maombi yetu na tunakuahidi kuwa tuko nyuma yako kwa hali na mali kuhakikisha kuwa unapata ushindi mkubwa,” alisema Ahmed Misanga, Mjumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya Nyagamana.
Akizungumza baada ya kupokea maombi hayo, Lowassa aliwashukuru kwa imani kubwa waliyoionyesha kwake na kuwaambia wamuombe Mungu ili jambo hilo liende salama.
Alisema anaendelea kumuomba Mungu amjaalie atimize ndoto yake ya safari ya matumaini.
Aidha, alisema anajivunia mafanikio aliyoyapata wakati akiwa mdhamini wa Umoja wa Vijana wa CCM kwa kusimamia umoja huo kupata kitega uchumi kikubwa, ambacho ni jengo lililoko katika makao makuu ya umoja huo jijini Dar es Salaam.
WENGINE WALIOMWENDEA LOWASSA
Tayari viongozi wa serikali, chama na wafugaji wa wilaya Mkinga walimchangia Lowassa Sh. 200,000 za kuchua fomu ya urais.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment