Mdau wa Sanaa Henry Mdimu (Kulia) akisisitiza umuhimu wa kuwa na mitandao ya kijamii kwa wasanii (hawapo pichani) katika Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Kushoto ni Afisa Sanaa wa BASATA, Augustino Makame.
Wadau wa Sanaa pamoja na Wasanii wakipata elimu kuhusu Nafasi ya Mitandao ya Kijamii katika Kukuza Sekta ya Sanaa kwenye mapema wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA.
Na
Mwandishi Maalum
Wasanii wamesisitizwa juu
ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwani waandaaji wa matamasha na
matukio mbalimbali ya kisanaa sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakiitumia katika
kuwapa kazi.
Akizungumza kwenye Jukwaa
la Sanaa lililofanyika mapema wiki hii kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam, mdau wa Sanaa
Henry Mdimu alisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona wasanii wakitumia kurasa
zao kuonesha mambo binafsi kama ya mapenzi na matusi wakati zinapaswa kutumika
kwa ajili ya kazi zao za Sanaa na kuwasiliana na mashabiki wao.
Alisisitiza kwamba si kila
kitu kinapaswa kuwekwa kwenye kurasa za kijamii za wasanii na kwamba lazima
wasanii wajifunze kutenganisha maslahi au masuala yao binafsi dhidi ya yale ya
wapenzi wao na kwamba Sanaa iko kwa ajili ya walaji na si wasanii pekee.
“Wasanii hawana budi
kuelewa kuwa hawatengenezi sanaa au kurasa za mitandao ya kijamii kwa ajili
yao. Wanaitengeneza ili kuwasiliana na mashabiki wao kuhusu kazi wazifanyazo na
kutafuta fursa za masoko na kazi nje. Lazima waelewe mapromota wa kimataifa
hutumia sana kurasa hizi katika kutoa fursa” alisisitiza Mdimu.
Aliongeza kwamba, msanii
yeyote anayefanya kazi ya Sanaa kama kazi yake lazima afikirie kutumia mitandao
hii ya kijamii kiweledi katika kujitangaza kwani kutokufanya hivyo ni bora
kufanya kazi nyingine maana hiyo ndiyo njia kuu kwa sasa ya kujitangaza na
kupata fursa za maonesho mbalimbali ya kimataifa kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Afisa Sanaa
kutoka BASATA, Augustino Makame alisema kwamba Baraza limekuwa mstari wa mbele
kusisitiza matumizi sahihi ya teknolojia za kupashana habari muiongoni mwa
wasanii na kwamba sasa ni muda wa wasanii kuona umuhimu wa mitandao hii ya
kijamii na kuitumia ipasavyo katika kukuza Sanaa zao.
No comments:
Post a Comment