Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday, 18 September 2014

UTALII WATOWEKA TANGA! MAPANGO YA AMBONI YAGEUZWA MACHIMBO YA MAWE

Mapango ya Amboni ambayo ni sehemu ya kumbukumbu ya historia ya Tanzania na dunia kwa ujumla.

Na Raisa Said, Tanga

Huwezi kupata uhondo kwa kusimuliwa pekee, kilichopo katika Mapango ya Amboni kinavutia ukiyaona kwa macho yako mwenyewe. Ni maajabu ya Mwenyezi Mungu yaliyosheheni ndani ya kivutio hicho cha utalii.
Ukipata mtu mahiri wa kusimulia na aliyetembelea mapango hayo na
kujifunza kwa umakini, ama kwa hakika utatamani kufanya jitihada za hali na mali ili nawe ufike kujionea kwa macho na pengine utatamani kufahamu zaidi chanzo na historia ya makumbusho hayo ya asili.
Hata hivyo, mapango hayo sasa hivi yanakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo za barabara mbovu inayokwenda mapangoni pia, uchimbaji na upasuaji mawe ambao unatishia uwepo wa mapango hayo.
Mhifadhi wa Mapango hayo, Jumanne Maburi anasema watu wanalipua miamba kwa ajili ya kupata mawe yanayochomwa kutengeneza chokaa, “Watu wanatumia baruti kulipua miamba na kishindo chake hutingisha miamba katika mapango na kuleta athari ambazo kwa muda mrefu zinaweza kuyaharibu.”
Maburi anasema athari hizo zinaweza kuikosesha Serikali mapato zaidi ya Sh20 milioni kutokana na wageni wa ndani ya nchi ambao hulipa Sh1,000 yanayopatikana kwa mwaka . Wageni kutoka nje ni Sh20,000.
Jambo la kushangaza ni kwamba, Serikali ambayo ina mpango wa kuboresha hadhi ya mapango hayo, ndiyo inayotoa leseni kwa watu ambao wanalipua miamba hiyo. Anashauri watu watafute njia mbadala za kuingiza kipato au kwenda sehemu nyingine mbali na mapango hayo ili kuyanusuru.
Kuhusu barabara, anaishauri Serikali kuifanyia maboresho ili kuwavutia wageni. Anaishauri pia kuhamasisha uwekezaji hasa katika malazi na chakula ili wageni watumie muda mwingi katika eneo hilo.
Maburi anasema pamoja na changamoto hizo, uongozi wa mapango hayo umeboresha mazingira ikiwamo kutumia taa za kisasa tofauti na zamani ambapo walitumia vijinga vya moto ambavyo vilikuwa vinatumiwa na wenyeji.
Mapango ya Amboni ambayo yamewaduwaza hata wageni kutoka nchi zilizoendelea yametokana na mabadiliko ya nguvu za asili zilizobadilisha maumbile ya miamba ya chokaa katika kipindi cha Jurasiki, takriban miaka milioni 150 iliyopita.
Mapango hayo yaliyoko katika eneo la Kiomoni, Kata ya Kiomoni katika Tarafa ya Chumbageni wilayani Tanga, ni eneo zuri kwa kupumzikia na pia kwa shughuli nyingine kama za utafiti wa kihistoria, kijiografia na kijiolojia.
Yako umbali wa kilometa nane kutoka Tanga Mjini kupitia barabara kuu inayoelekea Mombasa.
Kwa mujibu wa utafiti, eneo hilo la mapango lilikuwa chini ya maji miaka milioni 20 iliyopita.
Awali, eneo hilo lilikadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 234 lenye mazingira ya miamba ya chokaa.
Miamba ya chokaa kwa asili huundwa na madini ya kashiamu kabonate; miamba hii ni migumu kumomonyolewa na maji ya kawaida, lakini si rahisi kuyeyushwa na maji yenye kiasi kidogo cha tindikali ya kaboni.
Maburi anasema maji hayo yenye tindikali husababisha mabadiliko kidogo pindi yanapoteremka kuelekea ardhi.
Baadhi ya mambo ambayo huwezi kuamini kwa kusimuliwa ni ramani ya Afrika iliyojiunda kutokana na uwazi wa mapango na jiwe lililojichonga na kutengeneza picha ya kichwa cha simba, ambavyo vyote vipo kwenye mlango wa kuingilia katika mapango hayo.
Baadhi ya picha nyingine zilizojichora juu na pembeni mwa miamba ni sanamu la Bikira Maria na Msikiti, ambavyo kila kimoja kimekaa upande wake na alama tosha za kuashiria kuwa ni picha uionayo mbele yako, huku msikiti ukiwa na baadhi ya michoro inayoonekana kusomeka kama kitabu cha Quran na kwa Bikira Maria kukiwa na alama ya kitabu kama Biblia iliyofunuliwa.
Mengine ni pamoja na bawa la ndege lililojichonga na kutengeneza picha halisi ya ndege ambayo unapoiona kabla ya kusimuliwa, unaweza kuhisi ni ndege aliyefia au kunasa mahala hapo siku za nyuma.
Pamoja na hayo, pia kuna picha za mamba, unyayo wa tembo, Mlima Kilimanjaro, mlango wa ndege ya abiria, kochi lililojichonga mfano sofa, na kinachovutia zaidi ni picha ya chui iliyojichora juu ya mwamba na unyayo wa kiatu. Ila mwisho wa yote ni njia nyembamba.
Vilevile, ndani ya mapango hayo kuna simulizi za Osale Otango (Samuel Otango) na Paulo Hamis ambao walikuwa wakitumia kituo namba tatu ndani ya mapango hayo kama sehemu ya kujificha kati ya mwaka 1952 na 56 walipokuwa wakiendesha harakati za ukombozi wa watu weusi kutoka kwa walowezi na wakoloni wa kipindi hicho.
Pia kuna njia zilizomo mapangoni humo zinazoelekea Mombasa, Maweni na Mkoa wa Kilimanjaro.
Hata hivyo, hadi hii leo haijulikani mapango hayo yaligunduliwa lini, bali taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba watu wa makabila yaliyoishi jirani na eneo hilo, Wabondei, Wasambaa, Wadigo na Wasegeju wamekuwa wakiyatumia kwa ajili ya matambiko ya mizimu tangu karne ya 16.
Eneo hilo la mapango kwa wakati huo likijulikana kama la mzimu wa mabavu na sasa, pia hutumiwa na baadhi ya watu wanaoamini nguvu za mizimu kutoka sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki ambao huja kuomba na kutambika katika vijipango mbalimbali vilivyopo.
Serikali iliyachukua mapango hayo kutoka kwa iliyokuwa Kampuni ya Kigeni ya Amboni Limited, mwaka 1922. Kampuni hiyo pia ilikuwa ikimiliki mashamba ya mkonge katika maeneo ya Tanga na ilikuwa ikiyatumia mapango hayo kama sehemu ya kupumzikia.
Baadhi ya vivutio vingine ni maeneo yaliyotengwa maalumu kwa ajili ya kuomba au kutambikia mizimu. Ukifika maeneo hayo, utaona vitu vingi vinavyohusiana na imani za kijadi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi waliotembelea mapango hayo, Janet Aaron na Benita Tendwa wa Shule ya Sekondari ya Tanzania Adventistya Usa River, Arusha waliwataka Watanzania kuyatembelea kujionea maajabu na kusaidia katika kuyahifadhi.
Mwalimu wa shule hiyo, Clement Mgweno alitoa wito kwa jamii kujitokeza kupata fursa ya kutembelea mapango ya Amboni ili kujifunza mambo ya asili na kuona vivutio vilivyomo ndani ya mapango hayo.

No comments:

Post a Comment