JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU WAJUMBE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUTOKA CCT
Jumuiya
ya Kikristo Tanzania (CCT) inachukua fursa hii kuvishukuru vyombo
mbalimbali vya habari kwa jinsi ambavyo vimekuwa vikitoa taarifa
mbalimbali kuhusu kazi na matamko ya CCT. Kuhusiana na mchakato wa
kuandikwa kwa Katiba mpya, CCT inaamini kuwa suala hili ni la MARIDHIANO
na sio la ubabe wa kikundi au chama fulani cha siasa.
Kama
ambavyo ilitangazwa na Mhe. Rais Januari 2014 kuwa Taasisi mbalimbali
zipeleke mapendekezo ya wajumbe wanaoweza kuteuliwa kuwa wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba, CCT ilipeleka mapendekezo ya wajumbe tisa na
kati ya hao Mhe. Rais alimteua mjumbe mmoja tu ambaye ni Bibi Esther
Msambazi. Mjumbe huyu aliyeteuliwa ni Mkristo wa kawaida (lay Christian)
na wala si Kiongozi wa Dhehebu lolote la Wanachama wa CCT na pia hata
sio Mzee wa Kanisa analotoka bali Mkristo mwaminifu wa kawaida. Huyu
ndiye mwakilishi wa CCT kwenye Bunge Maalum la Katiba. Viongozi wengine
wa Dini ya Kikristo (Maaskofu na Wachungaji) waliopo katika Bunge hilo
HAWAKUTUMWA NA CCT na wala CCT haina taarifa ni vipi walichaguliwa kuwa
wajumbe wa Bunge hilo Maalum.
Aidha,
pia Jukwaa la Wakristo Tanzania haliwatambui Viongozi hao kwani Jukwaa
hilo linaundwa na Taasisi za TEC, CCT, PCT na SDA. Kutokana na misingi
ya imani ya taasisi hizi kwa umoja wake, Viongozi wakishakubaliana jambo
fulani kwa pamoja na kwa umoja wao wanalisimamia na kulitekeleza. NDIYO
YAO NI NDIYO NA HAPANA NI HAPANA kwa kuwa hawana ndimi mbili na wala
hawatumikii Mabwana wawili. Kwa mantiki hiyo, CCT ikiwa mmoja wa taasisi
zinazounda Jukwaa la Kikristo Tanzania inaendelea kusisitiza kuwa
msimamo wa viongozi wa dini kama ulivyotolewa na Jukwaa la Kikristo
Tanzania kuhusiana na Maoni waliyopeleka kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya
Wananchi chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Warioba na Matamko
waliyotoa ni sahihi na itaendelea kuyasimamia na kuyasambaza hadi
yamfikie kila Mkristo ili wananchi wa Tanzania wapate Katiba
wanayoitaka. Aidha, Viongozi hao wa Jukwaa la Wakristo Tanzania haliwezi
kutafuta maoni ya Viongozi wa Dini walioko katika Bunge Maalum la
Katiba kwa sababu hawawatambui kama wawakilishi wa taasisi zao na hivyo
kukataa kwa nguvu zote yale ambayo viongozi hao waliopo Bungeni watakuwa
wakiyasema. Mwisho kabisa tunawaomba viongozi hao wajiulize, “hivi sisi
tumetumwa na tunamwakilisha nani humu Bungeni?”
Imetolewa leo September 05, 2014
Na: JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA

No comments:
Post a Comment