Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani imetishia kuvifutia usajili vyama vyote vya kijamii vinavyokiuka kanuni na sheria kuanzia Oktoba mwaka huu.
“Sababu zitakazofanya chama kifutwe kutoka katika daftari la msajili wa vyama vya kijamii ni kufanya shughuli tofauti na zile zilizoandikishwa katika katiba ya chama husika,” alisema Nantanga.
“Pamoja na hiyo, hata vile visivyowasilisha taarifa za utendaji kazi, mapato na matumizi ya fedha zake sambamba na kutolipa ada za mwaka kwa wakati, navyo vitakuwa katika mkumbo huo.
“Wizara itachapisha majina ya vyama vyote vya kijamii vilivyo katika daftari la kudumu la msajili ili kutoa nafasi ya miezi mitatu kwa vyama hivyo kujitathmini kabla utekelezaji haujafanywa.”
Daftari hilo kwa sasa lina vyama 9,554 vya kijamii nchini vinavyojumuisha vyama 956 vya kidini na vingine 8,598. Taarifa hiyo inasema kuwa kila chama kinatakiwa kuhakikisha kuwa kinatekeleza matakwa yote ya kisheria yanayokiongoza kama inavyotakiwa.
“Zoezi hili litawezesha uanzishwaji wa mfumo wa kisasa wa taarifa za pamoja (database) utakaoboresha mawasiliano kati ya msajili na vyama husika. Pia itajumuisha uhakiki wa vyama hivyo na kuviondoa visivyostahili,” alisema.
Baadhi ya vyama hivyo vimedaiwa kubadili katiba zao pasipo kuridhiwa na msajili, jambo linalochangia kutotambuliwa kwa shughuli zake mpya zilizoainishwa na katiba hizo.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment