Huko nyuma nimetumia maneno
mwelekeo wa Chama bila maelezo. Inafaa sasa nieleze maana yake. Ili kusisitiza
umuhimu wake. Kujenga nchi si jambo rahisi. Kujenga Tanganyika tuliyorithi, iwe
Taifa moja imara lisingekuwa jambo rahisi. Tulikuwa tumeanza. Na kujenga
Zanzibar tuliyorithi, iwe taifa moja imara, isingekuwa kazi rahisi.
Mimi naamini kuwa kutokana na
historia yake, ya nyuma na ya karibu, kuifanya Zanzibar kuwa Taifa moja imara,
kungekuwa kazi ngumu zaidi kuliko kuijenga Tanganyika na kuyafanya makabila yake
kuwa kitu kimoja. Lakini hatukuruhusiwa kujua. Historia haikuturuhusu kujenga
Tanganyika kuwa Taifa, wala kujenga Zanzibar kuwa Taifa. Wa Bara tulikuwa raia
wa Tanganyika huru tangu tarehe 9 Desemba, 1961 mpaka tarehe 26 Aprili, 1964;
muda wa miaka miwili, na miezi minne, na siku kumi na saba, ukiihesabu na siku
ya tarehe 26 Aprili, 1964.
Mimi nilikuwa Rais wa Tanganyika
kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne na siku 17 hizo hizo. Wala historia
haikuturuhusu kujenga Zanzibar iwe Taifa. Uhuru wa kutoka kwa mkoloni
ulipatikana tarehe 10 Desemba, 1963: na Mapinduzi ya kung'oa usultani wa
Mwarabu yalifanywa tarehe 12, Januari 1964. Hatukujenga nchi mbili. Badala yake
tukafanya kitendo cha pekee katika historia nzima ya Afrika huru.
Tanganyika tuliyokomboa kutoka
kwa Wakoloni, lakini hatukuiunda, mipaka yake ni ya kurithi; na Zanzibar' tuliyonyakua
kutoka kwa Wakoloni na Masultani wa Kiarabu, lakini hatukuiunda, mipaka yake ni
matokeo ya unyang'anyi na unyang'au wa Waingereza na Wajerumani,
tukaziunganisha zikawa nchi moja. Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika
historia ya Afrika huru. Nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka katika
Ukoloni. Tanzania ni ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada
ya kukomboa sehemu zake ilivyo kutoka katika ukoloni.
Wako Watanzania wa ajabu kabisa
wanaosema kuwa uamuzi huo, au vyombo vilivyotumiwa, au njia iliyotumiwa, au
vyote, havikuwa halali. Hao hawana shaka na uhalali wa Tanganyika, ambayo
iliunganishwa na Wajerumani, na ikamegwa-megwa na Waingereza na wenzao. Kwa hao
kama Rwanda na Burundi na Tanganyika zisingetengwa na mabeberu, tukazirithi
kama zilivyokuwa chini ya Wajerumani, wasingeushuku uhalali wa nchi Moja hiyo.
Lakini kama baada ya uhuru, Rwanda na Burundi na Tanganyika zingeamua kuungana
ziwe Nchi Moja, kwa utaratibu wo wote ambao zingekubaliana,
"Wazalendo" hawa wangesema muungano huo si halali!
Pwani ya Tanganyika na Zanzibar
ya sasa zilikuwa pamoja kwa muda mrefu sana kabla ya kutengwa na Wakoloni
Waingereza na Wajerumani.
Kama zingebaki zimetengana, kwa "wazaIendo" hao hiyo ingekuwa ni halaIi, maana zilitengwa kwa hila na mitutu ya bunduki za Mabwana. Lakini uamuzi wa Tanganyika huru na Zanzibar huru kuungana, na hivyo kuwaunganisha tena ndugu waliokuwa wametengwa na Mabeberu, tendo hila kuna viongozi wetu wanaosema kuwa halikuwa halali.
Kama zingebaki zimetengana, kwa "wazaIendo" hao hiyo ingekuwa ni halaIi, maana zilitengwa kwa hila na mitutu ya bunduki za Mabwana. Lakini uamuzi wa Tanganyika huru na Zanzibar huru kuungana, na hivyo kuwaunganisha tena ndugu waliokuwa wametengwa na Mabeberu, tendo hila kuna viongozi wetu wanaosema kuwa halikuwa halali.
Hatukutafuta maoni ya watu kwa
njia ya demokrasia wanayoijua wao. Wajerumani na Waingereza walitafuta maoni ya
wazee wetu kwa mtutu wa bunduki! Hiyo iIikuwa halali. Nchi walizoziunda kwa
njia hizo zilikuwa halali. Tunatakiwa tujivunie Utanganyika na Uzanzibari
uliopatikana kwa njia hizo; lakini tuuonee haya Utanzania, tunda la uhuru wetu
wenyewe.
Sikuamini kuwa wakoloni walifaulu kiasi hiki katika kuzinywesha kasumba na kuzitawala akili za baadhi yetu!
Sikuamini kuwa wakoloni walifaulu kiasi hiki katika kuzinywesha kasumba na kuzitawala akili za baadhi yetu!
Nilitoka nje ya mstari. Narudia:
Tulikuwa Nchi Mbili, lakini kwa hiari yetu wenyewe, tukaamua kuwa Nchi Moja.
Kwa sabaabu ambazo nimezieleza mara nyingi, na kama hapana budi nitaendelea
kuzieleza, tukakubaliana kuwa ni Muungano wa Serikali Mbili. Aidha, tulikuwa na
vyama viwili vya ukombozi, TANU na ASP. Na ni vizuri kuendelea kuwakumbusha wale
ambao wangependa tusahau, kwamba TANU na ASP vilikuwa yyama vya ukombozi,
havikuwa vyama vya uongozi.
Hatua ya pili katika historia ya
kuijenga Nchi yetu, tuliichukua tarehe 5 Februari, 1977, miaka 13 baada ya Muungano.
TANU na ASP, Vyama vyetu vya Ukombozi, ambavyo vilijua kuwa Umoja ni silaha
kubwa ya Ukombozi, viliungana vikawa chama kimoja, Chama Cha Mapinduzi, CCM
chama ambacho kina nasaba inayofanana na nasaba ya Tanzania. Tanzania ni
Tanganyika na Zanzibar, na CCM ni ASP na TANU.
Sitaki kusema kuwa CCM nayo ni lulu
ya Afrika, lakini naeleza tu mwelekeo wa historia ya nchi yetu na vyama vya
ukombozi wetu. Tuliokwisha kuunganisha nchi mbili zikawa nchi moja, sasa
tukaunganisha vyama viwili vikawa chama kimoja. Hiyo haikuwa hatua ndogo hata
kidogo katika kujenga nchi yetu. Kuna nchi gani nyingine zilizofanya hivyo?
Vyama tunavyoviona katika Bara letu siku hizi vinashindwa hata kuunganisha
mbinu tu, ili viweze kushinda wapinzani wao katika uchaguzi. TANU na ASP vilikuwa
vyama viwili na vyote vikitawala. Vikajiua kwa hiari iIi vizae chama kimoja
kiongoze na kuendeleza historia ya nchi yetu.
Tumejenga nchi ambayo ilikuwa
inaheshimiwa duniani kote, ndani na nje ya Afrika. Mwaka huu tumetimiza umri wa
miaka thelathini. Kama si maajabu haya yaliyozushwa bure na viongozi wetu
watukufu, ilitupasa kushangilia sana umoja wa nchi yetu, na kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutufikisha hapa salama.
Tungali na Serikali Mbili, lakini
tuna Serikali moja tu ya Muungano. Na nani hawezi kuona kwamba hapo haja ya
kubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali Mbili itakapodhihirika,
historia ya Nchi yetu na mwelekeo wa chama chetu vitatuongoza kwenye muundo wa
Serikali moja? Kitu kimoja ambacho hatuwezi kutazamia ni kwamba siku moja Nchi Moja
hii itakuwa nchi mbili, kwa uongozi wa CCM. Lakini hiyo ndiyo shabaha ya kuwa
na Serikali ya Tanganyika. Na hata kama wajinga na wapumbavu hawatambui hayo,
bado hayo ndiyo yatakayokuwa matokeo ya ujinga wao: ukifufua Tanganyika, utaua
Tanzania. Kwa uongozi wa CCM?
Ila narudia tena,
Niliyokwisha kunena,
Sera hii, nilisema,
Si ya umma ni ya chama,
Ni Sera ya Viongozi,
Wa Chama Cha Mapinduzi,
Na waungao mkono,
Uvunji wa Muungano.
Chama hiki Mapinduzi,
Kimeleta mageuzi,
Si Chama pekee tena,
Viko aina aina
Na Chama Cha Mapinduzi,
Watambue Viongozi,
Ni Chama cha Muungano,
Si Chama cha Utengano.
Kama mwanachama wake,
Hazipendi sera zake,
Atoke, asichelewe,
Aanze chake mwenyewe.
Kama viongozi wetu,
Hawapendi sera zetu,
Watoke waende zao,
Waanzishe vyama vyao.
Viko vyama bozibozi,
Vyatafuta viongozi,
Waende waviongoze,
Na hiki tukipongeze
WASlTEKE CHAMA NYARA,
WAKILAZIMISHE SERA,
AMBAZO KATU SI ZAKE,
NI ZA WAPINZANI WAKE
HASA KAMA SERA KAMA ZINO
ZA KUVUNJA MUUNGANO
CHAMA CHA MAPINDUZI kitakapobadili sera yake ya Muungano wa Serikali Mbili, sera yake mpya itakuwa sera ya Muungano wa Serikali moja. Chama Cha Mapinduzi chenye wanachama wenye akili, na ukweli, na ujasiri, hakiwezi katu kukubali sera ya serikali tatu, kikijua wazi wazi kwamba matokeo na shabaha ya sera hiyo ni kuiua, na kuizika Tanzania. Chama Cha Mapinduzi kikiwa na msimamo huo, na wala kisiuonee haya, Tanzania itadumu.
CHAMA CHA MAPINDUZI kitakapobadili sera yake ya Muungano wa Serikali Mbili, sera yake mpya itakuwa sera ya Muungano wa Serikali moja. Chama Cha Mapinduzi chenye wanachama wenye akili, na ukweli, na ujasiri, hakiwezi katu kukubali sera ya serikali tatu, kikijua wazi wazi kwamba matokeo na shabaha ya sera hiyo ni kuiua, na kuizika Tanzania. Chama Cha Mapinduzi kikiwa na msimamo huo, na wala kisiuonee haya, Tanzania itadumu.
REJEA:
NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
No comments:
Post a Comment