BISMILLAHI RAHMANI RAHIM
TAMKO
LA TAASISI YA MASHEIKH NA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA KUFUATIA
KADHIA YA MAHAKAMA YA KADHI KATIKA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Sekretarieti
ya Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, imekutana leo
Jumapili tarehe 14/09/2014 katika kikao maalumu cha dharura kwa ajili
ya kujadili jambo moja tu, ambalo ni kadhia ya sisi Waislamu kudai
kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini na
mvutano uliojitokeza katika Bunge Maalum la Katiba, kati ya wanaotaka Mahakama ya Kadhi itamkwe waziwazi katika Katiba na wale wasiotaka iingizwe kwenye Katiba ya nchi.
mvutano uliojitokeza katika Bunge Maalum la Katiba, kati ya wanaotaka Mahakama ya Kadhi itamkwe waziwazi katika Katiba na wale wasiotaka iingizwe kwenye Katiba ya nchi.
Baada
ya kutafakari kwa kina hoja za pande zote mbili, Sekretarieti
imejiridhisha kwamba wanaodai Mahakama ya Kadhi iingizwe katika Katiba
ya nchi pamoja na Mahakama hizo kuendeshwa na Makadhi Waislamu katika
kesi za Waislamu zinazohusu ndoa, talaka, mirathi, waqfu, wasia na
malezi ya watoto, wako sahihi kuwasilisha madai hayo.
Waliojenga hoja hiyo wamesukumwa kudai hivyo kutokana na sababu kuu tatu zifuatazo:-
· Kwanza,
Mahakimu wa mahakama za kawaida, wanakosea sana katika kuzitoleoa
hukumu kesi za ndoa, talaka, mirathi n.k za Waislamu kutokana na
kutozijua vizuri sheria husika za Kiislamu ambazo ni pana sana katika
kadhia hizo, na ambazo zinahitaji mafunzo maalum zaidi ya mafunzo ya
sheria za kawaida za kisekula, ili kumuwezesha hakimu wa kawaida kuamua
kwa haki kesi hizo.
· Pili,
Kitabu kinachotumika kutolea hukumu hizo ambacho ni Qur-an
kinamuhitajia Hakimu kukijua vema kukikubali, kukiamini na kukiheshimu.
Jambo ambalo linaweza kupatikana tu kwa Kadhi Muslamu.
· Tatu,
jaribio la Waislamu kuwa na Makadhi wao wenyewe bila ya nguvu za
serikali limeshindikana baada ya hukumu zao kukosa thamani na nguvu za
kisheria mbele ya Mahakama za kawaida hapa nchini.
Kwa kuzingatia hayo, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inatoa Tamko lifuatalo:-
· Kwa
kuwa hivi sasa tumo katika Mchakato wa Kurekebisha Katiba ya nchi, si
kosa kwa Waislamu kudai Mahakama ya Kadhi iingizwe kwenye Katiba kwani
huu haswa ndio wakati muafaka wa kuwasilisha madai hayo.
· Wale
wanaopinga Mahakama ya Kadhi kuingizwa katika Katiba wajenge hoja zenye
mifano iliyo wazi, huku wakizitazama nchi ambazo zimeingiza mahakama
hizo katika Katiba zao, kama vile Kenya, Uganda na hata ndugu zetu wa
Zanzibar kama mifano hai ya jinsi mahakama hizo zisivyovunja mshikamano na umoja wa wanadini mbili mbali wanaoishi pamoja.
· Wenye
hoja ya hofu ya matumizi ya pesa za serikali, zinazotolewa na walipa
kodi wa dini zote kuendeshea Mahakama ya Kadhi kwa ajili ya kesi za
Waislamu tu, tunawaomba wazingatie yafuatayo:-
o Hivi sasa serikali inawalipa fedha zisizo na tija, Mahakimu wanaotoa hukumu kimakosa
katika kesi hizo za Waislamu kutokana na udhaifu wa uelewa wao wa
kitabu cha Qur-an na kuwaacha Waislamu katika hali ya kutoridhika na
mwenendo mzima wa uendeshwaji wa kesi hizo.
o Kama
yalivyopitishwa maamuzi ya kuanzishwa kwa mahakama maalum za Ardhi,
Kazi na Biashara ambazo zimesadia sana katika kupunguza msongamano wa
kesi katika mahakama za kawaida kutokana na maudhui kufanana, uwepo wa
Mahakama ya Kadhi utapunguza sana msongamano mkubwa wa kesi katika
mahakama za kawaida kwa kuzihamishia kesi za aina hiyo katika mahakama
maalum ya Kadhi na hivyo kuharakisha utoaji wa haki kwa ujumla.
Uharakishwaji
wa kuamua kesi, kutokana na hatua hiyo, utaongeza ufanisi wa
uendeshwaji wa mahakama kwa ujumla na mwishowe utapunguza gharama
zitokanazo na mlundikano wa kesi.
o Kuna
hoja inayotolewa kuwa, kwa kuwa serikali haina dini, mahakama za
kusikiliza kesi za kidini zisiingizwe katika Katiba ya nchi kwani jambo
hilo litaingiza udini katika serikali. Ukiiangalia kwa undani utaona
kuwa hoja hii haina msingi kwani ikumbukwe kuwa serikali hiyo hiyo ndio
imetoa uhuru wa wananchi wake kuabudu kwa misingi ya dini zao.
Na
serikali hiyo hiyo ndio huwajengea mazingira wanadini, ya kufanya ibada
zao hizo kwa uhuru na haki kama moja ya wajibu wa serikali.
Ndio
maana serikali hutenga maeneo maalum ya kujenga nyumba za ibada, siku
maalum za kusherehekea sikukuu za kidini, kutia moyo mchango wa viongozi
wa dini katika kujenga maadili mema katika jamii ili wapatikane raia wema, n.k.
Haya
yote yanafanywa na serikali kwa kuheshimu na kutambua umuhimu wa
wanadini kuridhika na uendeshwaji wa dini zao chini ya himaya yake.
o Kama
mahakama ya Kadhi itaingizwa katika Katiba ya nchi na Makadhi wakapata
fursa ya kuhukumu kwa usahihi kesi zao, matarajio ya Waislamu ni
kufurahia na kuridhika na ufumbuzi huo na hivyo kuzidi kujengeka kwa
amani na utulivu katika nchi.
· Taasisi
ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, inawanasihi Waheshimiwa
Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba pamoja na Watanzania wote kwa ujumla
kudumisha umoja wao na wasiigeuze kadhia ya Mahakama ya Kadhi kuwa ndio
“kisu” cha kuukata umoja na Utanzania wao waliodumu nao kwa muda mrefu
na kuishi pamoja kwa amani bila kujali tofauti za dini zao.
· Tunaomba
mjadala huu uendelee lakini uongozwe na busara na hekima na kamwe
asijaribu mtu yeyote kuondoa anachokiona yeye kuwa ni “Udini” kwa
kutumia “Udini”.
· Pamoja
na Waislamu kuwa na dai hilo muhimu la Mahakama ya Kadhi na Wasiokuwa
Waislamu nao kujipanga ili kuhakikisha mahakama hiyo haipatikani,
Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawahimiza
Waislamu wote nchini kuwa na subira pamoja na kujenga imani ya dhati kwa
serikali yao kuwa itawatendea haki, huku wakijipa matumaini kwamba
hakuna safari isiyokuwa na mwisho.
Tamko hili limetolewa na:
Sekretarieti
Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania
No comments:
Post a Comment