MSIMAMO WA NDUGU ZITTO KABWE KUHUSU MCHAKATO WA KUANDIKA KATIBA MPYA
(
tarehe 30 Julai, 2014 nilitoa msimamo wangu kuhusu Bunge la Katiba
kwamba liahirishwe mpaka baada ya uchaguzi Mkuu 2015. Pia nilipendekeza
maeneo ya kufanya marekebisho madogo ya katiba ya sasa. Nafurahi kwamba
Bunge sasa litaahirishwa. Nafurahi pia marekebisho yatafanyika.
Nasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa marekebisho hayo yanafanyika
yakiwemo masuala yanayohusu uchumi wa Zanzibar kama Mafuta na Gesi na
Ushirikiano wa Kimataifa. Mchakato utakapoanza upya, wajumbe wa BMK
wachaguliwe na wananchi moja kwa moja na wanasiasa wenye nia ya kugombea
vyeo vinavyotokana na katiba wasiwe wajumbe wa BMK ).
Nilisema haya
"Jana
tarehe 29 Julai, 2014 nimefanya mahojiano katika kipindi cha
PowerBreakFast kinachorushwa na Clouds FM. Baadhi ya vyombo vya habari
vimeandika mahojiano yale. Napenda nitoe ufafanuzi kidogo kuhusu msimamo
wangu kuhusu mchakato wa Katiba.
Kwanza, Mimi
sijawahi kuwa UKAWA wala kundi lolote lile katika Bunge Maalumu la
Katiba isipokuwa kundi linalotaka maridhiano. Msimamo wangu kuhusu
Muungano ni Serikali Tatu Zilizoboreshwa (S3z) ili kuwa na Muungano
imara usio tegemezi wala egemezi kwa Washirika wake.
Pili,
Mimi niliunga mkono ‘protest’ ya baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kupinga lugha za matusi na lugha za kibaguzi zilizokuwa
zinaendelea ndani ya mkutano ule. Vilevile niliunga mkono kwamba Rasimu
inayopaswa kujadiliwa ni Rasimu iliyotokana na Tume ya Marekebisho ya
Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba. Nasisitiza umuhimu wa
kupata Katiba BORA itakayoimarisha DOLA ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Tatu, kwa hali ya sasa kuna mkwamo
katika kupatikana kwa Katiba Bora. Mkwamo unaotokana na kutokuwepo kwa
nia ya dhati ya kupata maridhiano ya pande zinazopingana. UKAWA hawataki
mazungumzo na Viongozi wa Bunge la Katiba badala ya kujenga maridhiano
kila siku wanawabeza UKAWA jambo ambalo kamwe haliwezi kujenga mwafaka.
Ushauri wangu ni kuahirisha mchakato mzima wa kuandika Katiba mpaka
mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Katiba ya sasa ifanyiwe
marekebisho machache kama ifuatavyo;
i) Tume
ya Uchaguzi ili iwe huru na ionekane kuwa huru, ikiwemo kuwaondoa
watumishi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji katika kusimamia
uchaguzi
ii) Kuruhusu mgombea binafsi
iii)
Kuondoa Mafuta na Gesi kama Jambo la Muungano ili Zanzibar ianze mara
moja kusimamia kwa uhuru utafutaji wa Mafuta katika vitalu vilivyopo
upande huo wa Muungano
Mkutano wa Bunge Maalumu
utakaofanyika bila kuwepo kwa maridhiano utakuwa hauna maana yeyote na
itakuwa ni sawa na kupoteza muda na fedha za walipa kodi ambazo
zingeweza kununua madawa vijijini. Mimi binafsi sitahudhuria mkutano wa
Bunge Maalumu kama makundi hasimu hayatakuwa yamefikia maridhiano.
Kabwe Zitto, MB/MBMK"
Sasa tujiandae na marekebisho hayo na tujipange kwa Uchaguzi Mkuu

No comments:
Post a Comment