Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday, 13 September 2014

CHEYO ASEMA, UKAWA WANAPOTOSHA MAKUBALIANO NA RAIS KIKWETE

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ambaye ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ambaye ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo, ameuruka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akisema unapotosha makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa kituo hicho na Rais Jakaya Kikwete.

Akizungumza wakati wa mjadala wa sura mbalimbali za Rasimu ya Katiba Mpya, bungeni Dodoma jana, Cheyo alisema wakati wa mazungumzo hayo yaliyofanyika mapema wiki hii mjini hapa, walikubaliana kuwa mchakato wa kutengeneza Katiba mpya uendelee hadi pale itakapopatikana Katiba inayopendekezwa, tofauti na madai ya Ukawa kuwa moja ya makubaliano ilikuwa ni kusitisha mchakato huo.

Cheyo alisema hayo ikiwa ni siku moja baada ya viongozi wa Ukawa unaoundwa na vyama ambavyo vimesusia mchakato huo, kutaka Bunge hilo lisitishwe kwani si moja ya makubaliano yaliyofikiwa katika kikao hicho cha TCD na Rais.Vyama vinavyounda Ukawa ni Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.

“Tulikubaliana Bunge hili lipate Katiba inayopendekezwa, pia tulikubaliana mchakato ufike mwisho kwa mujibu wa tangazo la serikali GN 2 ambayo ni tarehe nne Oktoba , kura ya maoni ndiyo iahirishwe hadi baada ya uchaguzi mkuu mwakani,” alisema Cheyo.

Alisema Katiba mpya itapatikana kwa mazungumzo na maridhiano na si kwa kutumia njia nyingine zilizo nje ya Sheria ya Mabadilko ya Katiba.

“Katiba itakayodumu ni ya maridhiano lakini haina maana baada ya kukubaliana mtu anang’ang’ania upande wake. Maridhiano ni kukaa na kukubaliana ni mambo gani yanafaa na vitu gani ambavyo vinaweza kuwekwa pembeni kwa sasa lakini baadaye vikaja vikashughulikiwa kwa mazingira ya wakati huo” alisema na kuongeza:

“Kuna video kila mmoja alikuwa anachukuliwa, kweli sasa tumuombe Mheshimiwa Rais ebu tutengenezee kipindi maalum kila mmoja ataonekana alikuwa anasema nini.Tuwe waungwana…yale niliyotangaza kwenye vyombo vya habari, hayo ndiyo makubaliano, hakuna makubaliano mengine ya nje."

“Mkishakubaliana huwezi kwenda tena nje na kuzungumza mengine, maridhiano yanapatikana kwa mazungumzo, kukaa pamoja na kuzungumza  mwisho wa siku kuna kuna mambo mtakubaliana na mengine kuyaacha…kama upo nje kwa sababu, labda unaumwa, au hutaki serikali tatu, au sababu yoyote hiyo ni shida yako ni…Bunge hili haliwezi kuendeshwa na watu walio nje, wanaotaka kutembea barabarani hawatapata kitu, kitakachopatikana ni Katiba,” alisema Cheyo huku akishangiliwa na wajumbe wengi wa kutoka Chama tawala.

Alimsifu Rais Kikwete kwa kukubali kukutana na viongozi wa TCD na kufikia makubaliano hayo.

“Rais Kikwete ni mfano mzuri wa kushauriana, hata wakati mwingine hapaswi, lakini amejiweka chini akakaa kitako na viongozi walio TCD ambao ni pamoja na viongozi wanaojiita Ukawa tukakaa pamoja, mara ya kwanza alitumia saa nne na mara ya pili saa mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametumia muda wake na tukasema haya tunakubaliana.”

Alisema mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya una hatua mbalimbali kwa mujibu wa sheria, hivyo utaratibu huo unapaswa kuachwa kama ilivyopangwa.

“Awamu ya kwanza ilikuwa ni Tume, wamemaliza kazi yao, awamu ya pili ni Bunge Maalum tutamaliza kazi yetu na Bunge hili haliendeshwi na mtu ambaye yupo barabarani, Bunge hili linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na sheria tuliyonayo kwa sasa ni GN 254 ambayo inasema uhai wa Bunge mpaka terehe nne mwezi wa 10 na wote tukakubaliana.Haiwezekani Mheshimiwa Rais akasimama akasema kesho Bunge limesitishwa,” alisema Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa United Democratic (UDP).

Mjumbe mwingine, Rashid Rahi, akichangia mjadala huo, alimtaka Rais Kikwete kutokubali kusikiliza watu wanaotaka mchakato huo usitishwe, kwani inaweza kusababisha Katiba mpya isipatikane.

“Vyama vilivyogomea mchakato havizidi vitano, humu tumo kila makundi tunatengeneza Katiba ya wananchi. Waliogoma hawataki mchakato wa Katiba. Ushauri wangu kwa Rais na kama kuna washauri wake wananisikia wakamwambie ahakikishe mchakato huu unafikia mwisho kabla hajaondoka madarakani, kuna watu wanataka kumkwamisha.”

“Rais Umeanzisha mchakato wa Katiba hakikisha unakamilika katika mikono yako. Kuna watu wanataka ufeli, hawakupendi, wanataka mchakato uishie njiani” alisema.

Rai alitatahadharisha kuwa endapo mchakato huo utasitishwa njiani na kusubiri Rais mpya aje aumalizie kuna hatari ya kutopata Katiba mpya kwania anaweza kuamua kutoendelea nao.

“Hapa kuna mambo mengi tunazungumza ikiwamo kuwa na mgombea binafsi, tuna uhakika gani Rais ajaye atamalizia mchakato huu?” Alihoji.

RATIBA YA BUNGE
KATIBU wa Bunge maalum la Katiba (BMK) Yahya Khamis Hamad, amesema uongozi wa Bunge unaandaa ratiba mpya ambapo itaingizwa mambo yaliyopangwa kufanyika katika siku 27 zilizoondolewa.

Awali, bunge hilo lilitakiwa kumalizika Oktoba 31, lakini baada ya makubaliano yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete na Viongozi wa vyama vya siasa kupitia TDC, uhai wa Bunge ulipunguzwa hadi Oktoba 4 mwaka kama tangazo la serikali inavyotaka.

Akizungumza katika Mahojiano maalum na NIPASHE jana, Hamad, alisema ratiba hiyo mpya siku za majadiliano kuhusu rasimu ya katiba zitapunguzwa hadi kufikia nane, ambapo mwisho itakuwa Septemba 13, mwaka huu siku ya Jumamosi.

Katika katiba ya mwanzo, muda wa majadiliano ulipangwa kwa siku 20, kuanzia Septemba  9 hadi 29, mwaka huu kisha kamati ya uandishi  Septemba 30 na kumaliza Oktoba 6, mwaka huu.

Ratiba hiyo ingewasilisha katiba pendekezi Oktoba 9, kabla ya Oktoba 20 hadi 21, mwaka huu wajumbe kupigia kura kifungu kwa kifungukwa ajili ya kupitisha.

Ratiba hiyo ilionyesha Oktoba 22 hadi 28, mwaka huu wajumbe wangepitisha masharti ya mpito, huku Katibu wa bunge hilo angetumia siku mbili ya Oktoba 29 na 30, mwaka huu kuwasilisha Katiba pendekezi kwa bunge hilo.

Aidha, Oktoba 31, mwaka huu ilipangwa kuwa siku ya mwisho kwa Mwenyekiti kuwasilisha kwa Rais Kikwete, Katiba pendekezi ili kuanza mchakato wa kupigiwa kura na wananchi.

“Kwa sasa tunajipanga kuweka ratiba ambayo mambo hayo yatafanyika katika muda tuliopewa na serikali, kazi ya kupanga inafanywa na Kamati ya Uongizi na ikikamilika tutawapa,” alisema Hamad.

Alisema kilichofanyika ni kuandaa ratiba ya awali inayoishi Oktoba 13, mwaka huu baada ya hapo itatolewa inayoonyesha kazi zitakazofanyika hadi kufikia tarehe ya mwisho.

SIFAHAMU MAKUBALIANO
Hamad, alisema kwamba makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya kisiasa, hayatambui kwa sababu hajapewa taarifa rasmi kufuatana na sheria.

Alisema Bunge hilo haliwezi kusitishwa, wala mchakato huo kuwa na uwezekano wa kurudiwa upya kutokana na sheria iliyotungwa kuanzisha chombo hicho zipo na hakuna kitu kinachoeleza kufanya hivyo.

“Nasikia watu wakisema katika vyombo vya habari kwamba bunge lisitishwe, jambo hilo haliwezekani, kibaya zaidi hata hayo makubaliano mimi siyajui hakuna taarifa yoyote iliyowasilishwa kwangu kuhalalisha makubaliano hayo,” alisema.

Alisema wajumbe wa Ukawa hawatakuwa na nafasi ya kujadili tena mchakato huo kisheria, badala yake kama hawataki katiba hiyo itumike watumie muda wa kupiga kura kuipinga.

Alisema mchakato huo utaendelea kama ulivyopangwa na itakapofika siku ya mwisho katiba pendekezi itakabidhiwa kwa Rais baada ya kupigiwa kura na wajumbe wa Bunge hilo.

WABUNGE WAMESHINDWA KUJADILI
Alisema kupunguzwa kwa muda wa kujadili rasimu, haitaathiri uboreshaji wa katiba pendekezi kwa sababu wajumbe wengi wamejikuta hawana mambo ya kuchangia kama walivyotarajia.

Hamad, alisema katika mjadala huo wajumbe hao walikuwa wakichangia hata kwa mambo waliyokubaliana katika kamati zao.

“Baada ya kugundua jambo hilo tumeamua kwa muda uliobaki tuwaorodheshee mambo yanayoleta utata ambayo hawakupata mwafaka ndani ya kamati, hata hivyo wamekuwa wagumu kufuata,” aliongeza.

KINGUNGE ATAKA UCHUMI
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Kingunge Ngombale-Mwiru, amependekeza Katiba mpya itakayotengenezwa ijenge misingi ya uchumi imara ambao utakuwa suluhisho la matatizo yote ikiwamo umasikini.

Katika mapendekezo yake hayo ambayo pia ameyachapisha na kuyasambaza kwa wajumbe wote wa Bunge Maalum kuwashawishi wakubaliane nayo, anapendekeza  iongezwe sura mpya inayohusu mapinduzi ya kiuchumi, kwa kutumia sayansi na teknolojia ya kisasa katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii.

Kingunge alisema Katiba ijayo ilenge kufanya mapinduzi ya kisasa katika elimu, kilimo na viwanda, vinginevyo Watanzania wataendelea kuwa masikini na wanyonge duniani.

“Tusiandike Katiba ilimradi tu, bali yenye kulenga kuwainua wananchi kiuchumi na yenye kutoa haki za makundi mbalimbali, ingawa haki hizo hata kwenye katiba ya mwaka 1977 wanaozifaidi ni wenye nacho, wale wasiyo na hakika ya chakula cha kesho haki hizo kwao ni hadithi,” alisema.

 “Katika hii iweke misingi ya kujenga uchumi wa kisasa, ukilenga kufanya taifa linalojitegemea na lenye maendeleo linganifu, kwa sasa katika eneo la uchumi nchini, baadhi ya watu wanaendelea huku wengine wakiachwa nyuma na wengine pembeni” alisema na kuongeza:

“Kwa mfano, wakati wengine wanaendelea, wafugaji wenyewe wanahangaika kutafuta malisho na manywesheo ya mifugo yao, wavuvi wameachwa nyuma kiasi kwamba hakuna hata kiwanda kimoja nchini kinachotengeneza vifaa vya uvuvi, vya kisasa.”

Alipendekeza pia iundwe Tume ya Sayansi na Teknolojia na Utafiti, itakayokuwa chombo kikuu cha kuratibu na kuendeleza tafiti mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo ya uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment